Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nakereka jamani, mke ana kizee hawaishi kupigiana simu

September 12th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nimeoa na ninampenda sana mke wangu. Ninamtosheleza kwa mahitaji yake yote nyumbani na pia chumbani. Lakini kuna jambo moja analofanya na nahisi ananikosea. Amekuwa akimpigia simu mzee waliyekuwa marafiki kitambo ambaye si wa rika lake. Kitendo chake hicho kinaniumiza sana moyoni. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Ni makosa kwa mtu kuendelea kuwasiliana na mpenzi wake wa zamani iwapo tayari amepata mwingine. Kama hujamwambia, mwelezee unavyohisi kuhusu jambo hilo. Mwambie kama bado anamtaka huyo wake wa zamani akwambie ukweli ili muachane roho safi badala ya kuendelea kuhangaisha moyo wako.

 

Ameahidi kunioa!

Shikamoo shangazi! Nina mpenzi ambaye tumekuwa pamoja kwa miaka mitatu sasa ingawa bado ni mwanafunzi, anamaliza shule ya upili mwaka huu. Ninampeda kwa moyo wangu wote na ameniahidi kuwa atanioa. Nishauri.

Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, ninaelewa kuwa wewe na mpenzi wako hamna tatizo lolote katika uhusiano wenu, mambo yanawaendea sawa tu. Kwa sababu hiyo sijui unataka ushauri gani kutoka kwangu ila tu kuwatakia heri mipango yenu itimie jinsi mnavyotaka.

 

Hajatamka kuwa naye ananipenda

Kwako shangazi. Nina mpenzi ambaye tumekuwa pamoja kwa miaka miwili sasa. Mimi nimemwambia mara kadhaa kwamba nampenda lakini yeye hajawahi kuniambia. Sielewi jinsi anaweza kuwa na mapenzi kwangu na hataki kuniambia kuwa ananipenda. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Nashindwa kuelewa jinsi mlivyoanza uhusiano wenu kama hajawahi kukwambia anakupenda. Hiyo ina maana umekuwa ukimsukumia penzi lako tu na hujui anakupenda ama hakupendi. Chukua hatua sasa umuulize ili ujue msimamo wake usije ukawa unapoteza wakati wako kwa mtu asiye na haja nawe.

 

Amegeuka kinyonga hataki harusi

Kwako shangazi. Mimi na mwanamke mchumba wangu tulikuwa tumeahidiana kufunga ndoa mapema mwaka huu. Sasa mwenzangu amebadili nia ghafla ananiambia nisubiri kwa miaka miwili zaidi. Nahisi kuwa huo ni muda mrefu sana sidhani nitaweza kusubiri. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Hujaelezea mchumba wako amekupa sababu gani ya kusukuma mbele ndoa yenu. Akikuelezea na uhisi kuwa ana sababu nzuri, itakuwa vyema usubiri iwapo ndiye umechagua kuwa mwenzako maishani. Ukionelea anakuchelewesha bila sababu na huwezi kusubiri, itabidi umwambie ukweli ili akupe ruhusa utafute aliye tayari kuolewa.

 

Adai namridhisha lakini jicho la nje bado limemzidi!

Shangazi hujambo? Nimekuwa katika ndoa kwa miaka mitano sasa na tumejaliwa watoto wawili. Tunapokula vya chumbani mume wangu husema namridhisha lakini ninashangaa kwamba bado anatembea nje. Nishauri.

Kupitia SMS

Iwapo una hakika kuwa mwenzako anatembea nje ya ndoa, mketishe chini umuulize sababu. Anatafuta nini huko nje kama anakiri mwenyewe kuwa unamridhisha? Mwambie wazi kwamba huwezi kuvumilia tabia hiyo na kwamba akiendelea utamuachia hao anaowafuata huko nje.

 

Alilala kwangu siku moja tu, sasa anadai ana mimba yangu

Hujambo shangazi. Msichana fulani rafiki yangu alinitembelea na alipochelewa tukalala kwangu. Nina mchumba na uhusiano wetu unajulikana na wazazi na tunaweza kuoana wakati wowote. Sasa huyu msichana rafiki yangu anadai ana mimba yangu. Mimi siwezi kumuoa kwa sababu simtaki na pia siamini kama kweli mimba hiyo ni yangu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Mambo ni mawili. Inawezekana kuwa msichana huyo alipolala kwako alikuwa na mimba ama awe aliipata siku hiyo. Jinsi pekee ya kujua ukweli ni kusubiri hadi mtoto azaliwe kisha mpimwe ili ijulikane kama ni wako au la. Ukipata ni wako utagharamia malezi kama hutaki kumuoa mama yake.