Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nakerwa na mke wangu, anamtii mamake zaidi!

August 13th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHANGAZI pokea salamu zangu. Mimi nimeoa na nampenda sana mke wangu. Tatizo pekee ni kuwa mke wangu anamsikiza sana mama yake mzazi kuliko mimi na hali hiyo mara kwa mara imesababisha ugomvi kati yetu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Mke wako anafaa kuelewa kuwa mamlaka ya wazazi wake kwake yalimalizika siku uliyomtoa nyumbani kwao ukampeleka nyumbani kwako. Kwa sasa yuko chini yako na ni wajibu wake kukuheshimu na kuwa mtiifu kwako. Mwelezee hayo na umwambie achague kati yako na huyo mama yake. Akichagua mama yake, hiyo itakuwa na maana kuwa hana haja na ndoa.

 

Mwanafunzi mwenzangu ameahidi kunioa nikubali penzi lake?

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 19 na ninasoma shule ya upili. Kuna kijana tunayesoma pamoja ambaye ananitaka kimapenzi na ameahidi kunioa. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Maisha ni safari ya hatua kwa hatua, kila jambo na wakati wake. Nyinyi ni wanafunzi na huu si wakati wa kufikiria kuhusu mapenzi na ndoa bali ni wakati wa kusoma. Malizeni masomo kwanza.

 

Ananitoroka na sijui nimekosea wapi

Kwako shangazi. Msichana ambaye tumekuwa wapenzi kwa muda wa miezi sita ameanza kunikwepa katika siku za hivi majuzi. Sijamkosea kwa lolote na sielewi kiini cha tabia yake hiyo. Nishauri.

Kupitia SMS

Uhusiano wa kimapenzi ni chaguo la mtu na kila mhusika ana haki ya kuendelea nao ama kujiondoa. Inawezekana kuwa mwenzako ameamua kukatiza uhusiano huo lakini anashindwa kukwambia. Itakuwa vyema umuulize ili ujue mpango wake.

 

Nampenda sana lakini yeye hanipendi

Shikamoo shangazi! Nina mpenzi ambaye nampenda sana lakini yeye hanipendi. Nifanye nini?

JOHN, Kitale

Sielewi ilikuwaje mkawa wapenzi ilhali unasema mwenzako hakupendi. Hiyo ina maana kuwa wewe ndiye unayetaka uhusiano huo kwa lazima ilhali mwenzako hana shughuli nawe. Kwa nini uendelee kunapoteza wakati wako ukitafuta mapenzi kwa mtu asiye na hisia kwako?

 

Nilimuacha lakini ningali namtamani

Kwako shangazi. Kuna jambo ambalo naomba unishauri. Nilikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamume fulani lakini nikagundua alikuwa na uhusiano wa pembeni na rafiki yangu wa karibu. Nilimuacha lakini bado nampenda. Sijui nitafanya nini.

Kupitia SMS

Nashangaa kwamba unahangaisha moyo wako kuhusu mwanamume uliyemuacha kwa sababu hakuwa mwaminifu kwako. Iwapo una sababu nzuri ya kuamini kuwa ameacha tabia hiyo na yuko tayari mrudiane, basi mtafute mzungumze.

 

Ananipenda hata watu wa kanisa lao wanifahamu lakini…

Hujambo shangazi? Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 25. Kuna mwanamume ambaye tumejuana kwa miezi miwili sasa na ananiambia ananipenda; hata amenitambulisha kwa watu wa kanisa lake. Ingawa hivyo, simwamini. Naomba ushauri wako.

NANCY, Ruiru

Hujaelezea ni kwa nini unamshuku mwanamume huyo. Iwapo huna sababu nzuri, ninaamini kuwa shaka yako imetokana na hali kwamba bado ni mgeni kwako ikizingatiwa kwamba mmejuana kwa miezi miwili pekee. Iwapo wewe pia una hisia za kimapenzi kwake, ushauri wangu ni kuwa ujipe muda wa kutosha kumfahamu vyema ndipo uweze kufanya uamuzi unaofaa.

 

Ni mrembo ila amenizidi kwa umri

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 28. Kuna mwanamke fulani mrembo sana ambaye amevuta hisia zangu na ninaamini yeye pia ananipenda. Tatizo pekee ni kuwa amenizidi umri kwa miaka mingi. Nishauri.

Kupitia SMS

Hisia za kimapenzi ni suala la moyoni na zinakiuka mipaka mingi ukiwemo umri. Kama kweli umetathmini moyo wako na umetosheka kuwa huyo ndiye anayekufaa maishani, umri haufai kuwa kizingiti. Na iwapo unahisi kuwa umri utakuwa kikwazo, basi achana naye utafute mwingine. Chaguo ni lako.