Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Namtamani huyu binti lakini nasubiri anitongoze

October 14th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nina umri wa miaka 20 na kuna mwanamke ambaye amenasa hisia zangu. Amenizidi umri kwa miaka kadhaa na hiyo ndiyo sababu ninachelea kumfungulia moyo wangu. Ninaamini kuwa yeye pia ananipenda na nimekuwa nikingojea kwa matumaini kwamba atapiga hatua ya kwanza kuhusu jambo hilo. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Mwenye kiu ndiye huingia kisimani. Ingawa unasema unaamini mwanamke huyo pia anakupenda, si jambo la kawaida kwa mwanamke kuwa wa kwanza kuelezea mapenzi yake kwa mwanamume. Mapenzi hayajui umri. Weka kando woga ulio nao kisha umkabili umwelezee ukweli wa moyo wako. Kama yeye pia ana hisia kwako, atasalimu amri mara moja.

 

Mbona kipusa hulala fofofo baada ya mechi chumbani?

Hujambo shangazi? Nina mwanamke mpenzi wangu ambaye tunapendana sana. Hata hivyo, kuna jambo fulani ambalo nimeshuhudia wakati wa shughuli zetu chumbani. Kupaa na kushuka tu yeye hulala usingizi mzito kwa karibu saa nzima. Sijui ni kwa nini wala sijawahi kumuuliza. Ni kwa nini?

Kupitia SMS

Hiyo ni hali ya kawaida ambayo hutokea, sio tu kwa mwanamke, bali pia kwa mwanamume mhusika. Hisia hizo za unyonge wa mwili na usingizi hasa hutokana na hali ya kutosheka na shughuli hiyo. Hali inayokuwepo kabla ya shughuli hiyo huwa sawa na dhoruba kali inayovuma baharini. Baada ya kuitamatisha, hali hiyo hutulia na kualika usingizi.

 

Amerejea kwa wake wa kale, sasa sili silali, jamani mie nasononeka!

Kwako shangazi. Mwaka mmoja uliopita nilikutana na mwanamke fulani muda mfupi tu baada ya kuachwa na mpenzi wake na nikampenda. Alikubali tuwe wapenzi na nikamkubali pamoja na mtoto aliyekuwa amezaa na mpenzi wake huyo. Nilishangaa juzi aliponiambia mpenzi wake amemuomba warudiane na akakubali. Ameniacha hali mbaya hata kula na kulala ninashindwa. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Unasema ulikutana na mwanamke huyo muda mfupi tu baada ya kuachana na mpenzi wake. Hiyo ina maana kuwa alikukubali kutokana na hali yake hiyo kwa sababu alihitaji mtu wa kumuondolea upweke. Ni wazi kuwa wakati wote ambao mmekuwa pamoja moyo wake haujatoka kwa mpenzi wake na ndiyo maana hakusita kurudi kwake alipopata nafasi hiyo. Kubali kuwa amerudi ulipo moyo wake na utafute mwingine.

 

Analia unyumba unampa maumivu tele, sijui nimsaidie vipi, au kunani?

Habari zako shangazi? Ni miezi sita sasa tangu nilipooa. Tatizo ni kwamba tunaposhiriki mambo ya chumbani mke wangu hulalamika kwamba anahisi maumivu. Mara nyingi amekuwa akikataa shughuli hiyo kutokana na hali hiyo. Je, shida inaweza kuwa nini?

Kupitia SMS

Hali kama hiyo inaweza kutokea kama ulimuoa mke wako akiwa bikira ama hamkuwa mkishiriki tendo hilo mara kwa mara. Kama ndivyo, itabidi umpeleke taratibu tu na muda si mrefu atazoea. Pamoja na hilo, ningewashauri pia umpeleke kwa daktari wa masuala ya uzazi ili akaguliwe kuona iwapo ana tatizo tofauti.

 

Hanionyeshi mahaba, sasa nashindwa ikiwa ananipenda ingawa anadai hivyo

Hujambo shangazi? Nina tatizo katika uhusiano wangu wa kimapenzi na nakuomba unipe ushauri kuhusu jinsi ya kulitatua. Nampenda sana mpenzi wangu lakini yeye hanionyeshi mapenzi ya dhati ingawa huwa ananiambia ananipenda. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hujasema ni mambo gani ambayo unatarajia mpenzi wako akufanyie ndipo uamini kuwa anakupenda kwa dhati. Kama yapo na mpenzi wako anayajua, labda ni mambo ambayo anaona vigumu kuyafanya. Kama hajui ni vyema umwelezee ayajue ili naye akwambie iwapo ataweza au la.