Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Namzimia kipusa fulani lakini wala hana habari

February 27th, 2020 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nina jambo ambalo linanitatiza moyoni. Kuna mwanamke fulani ambaye amenasa moyo wangu na ninatamani sana awe mpenzi wangu lakini yeye hajui. Nampenda sana na sijui nitaanzia wapi ili tuwe na uhusiano. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Unakubali mwenyewe kuwa mwanamke huyo hajui kuwa unampenda na sijui unatarajia nani amwambie. Wewe ndiye unayemtaka na hakuna jinsi anavyoweza kujua hadi utakapomwambia. Usipomwambia utaendelea kutamani tu hadi atakaponyakuliwa na mwanamume mwingine.

 

Nahisi yake na ya ‘ex’ wake hayajaisha

Hujambo shangazi? Nina mpenzi na ninampenda kwa dhati. Kuna mwanamke ambaye amekuwa akimpigia simu mara kwa mara na nimekuwa nikishuku kuwa ni mpenzi wake wa zamani kutokana na mazungumzo yao. Nimevumilia kwa muda sasa na juzi nilimkabili nikamuuliza. Alikubali kuwa wameanza kuwasiliana tena lakini bado hawajaamua kurudiana. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Palipo na moshi pana moto. Mpenzi wako amerudiana na huyo wake wa zamani lakini aliamua kwamba hatakwambia wazi ila kupitia kwa ishara. Hiyo ndiyo sababu amekuwa akizungumza naye kwa simu huku ukisikia ili upate kujua kinachoendelea. Mbinu yake hiyo imefaulu kwa sababu umejua kupitia mazungumzo yao na ulipomuuliza akakubali mara moja. Itabidi ukubali kuwa uhusiano wenu umefikia kikomo.

 

Nimemzalia ila sioni akiwa na haraka kunioa

Hujambo shangazi? Nimekuwa na mpenzi kwa miaka mitatu sasa. Nilihamia kwake baada ya kumzalia mtoto mwaka uliopita na tumekuwa tukiishi kama mume na mke. Wazazi na jamaa zake wananijua lakini sioni akiwa na haraka ya kwenda kwetu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Hatua ambazo wewe na mume wako mmechukua ni kinyume na utaratibu. Kwanza mlikosea kuzaa kabla hamjaoana. Pili, ni makosa kuanza kuishi pamoja kama mume na mke ilhali wazazi wako hawajui. Inaonekana mume wako alitosheka baada ya kukupeleka kwao na ndiyo maana hashughuliki kwenda kwenu. Wazazi wako wakijua umeolewa bila kuwajulisha hawatafurahia. Ni juu yako umsukume mume wako akajitambulishe kwa wazazi wako kama mojawapo ya hatua za kuhalalisha ndoa yenu.

 

Kama ananipenda anavyodai, mbona basi hanitafuti?

Kwako shangazi. Kuna mwanamume anayetaka tuwe wapenzi. Ameungama kuwa ananipenda kwa moyo wake wote na kunihakikishia kuwa hana mwingine. Mimi pia nina hisia kwake na niko tayari kukubali ombi lake. Lakini nimekawia kumwambia hivyo kwa sababu mara nyingi mimi ndiye ninayemtafuta kwa simu. Je, ananipenda kweli?

Kupitia SMS

Mapenzi ya dhati hayaonyeshwi kwa maneno pekee bali pia kwa vitendo. Jinsi pekee ya kujua iwapo mtu anakupenda au la ni kupitia kwa maneno na vitendo vyake. Huenda mwanamume huyo hataki kukusumbua sana kwa simu huku akingojea jibu lako. Kama wewe pia unampenda, basi mwambie hivyo. Utaweza tu kuthibitisha mapenzi yake kwako mkianza uhusiano.

 

Kipenzi kumbe ni binti ya mwalimu wangu niliyemwogopa sana!

Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 26. Nimegundua kuwa msichana mpenzi wangu ni binti ya mwanamke aliyekuwa mwalimu wangu katika shule ya msingi. Namheshimu sana mwalimu wangu huyo na sijui itakuwaje akijua. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Mbali na heshima uliyo nayo kwa mwalimu wako, hamna uhusiano mwingine wowote wa damu wala ukoo. Kwa sababu hiyo mapenzi yako na binti yake ni halali na hayawezi kuondoa heshima yako kwake. Hasa, uhusiano wenu unafaa kuzidisha heshima hiyo kwani huenda baadaye atakuwa mama mkwe wako. Hilo kamwe lisikutie shaka.