Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Naogopa kukutana na tuliyefahamiana kwa simu

May 17th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nahitaji ushauri wako tafadhali. Kuna msichana fulani tuliyejuana kupitia kwa simu na tumekuwa tukiwasiliana kwa miezi miwili. Sasa tumepanga kukutana lakini nimeingiwa na woga, sijui tukionana nitaanzia wapi.

Kupitia SMS

Hizo ni hisia za kawaida zinazompata mtu anapoenda kukutana na mwingine kwa mara ya kwanza hasa kwa mazungumzo ya kimapenzi. Ukweli ni kuwa ni lazima mkutane tu ndipo muweze kupiga hatua katika uhusiano wenu. Unahitaji kujipa ujasiri tu na kukutana naye. Uzuri ni kuwa hali hiyo itatoweka baada yenu kukutana na kuanzia hapo itakuwa rahisi.

Jamaa ameniambia ananipenda, lakini mimi sijasoma

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 26 na nina mtoto ambaye nilimpata nikiwa shuleni na ikabidi niache masomo. Kuna mwanamume anayenitaka na ingawa mimi pia nampenda, ninahofia uhusiano wetu kwa sababu amesoma sana kunishinda. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni jambo la kawaida na muhimu kwa mtu kuwa na tahadhari maishani na ninaelewa hofu yako. Hata hivyo, kuna usemi kuwa, akipenda, chongo huita kengeza. Maana hasa ya usemi huu ni kuwa mtu akipenda kwa dhati kamwe hawezi kuona kasoro za mpenzi wake. Kama mwanamume huyo anajua kiwango chako cha elimu na kwamba una mtoto dob ado anasisitiza kukupenda, inaonekana ana mapenzi ya dhati. Hakuna maamuzi ya hakika katika mahusiano, mpe nafasi.

 

Kuna aliyenionya niachane na mpenzi, nifanyeje?

Kwako shangazi. Nina mwanamume mpenzi wangu ambaye tumepenga kuoana. Juzi mwanamke fulani alinipigia simu akanionya eti niachane na mpenzi wangu akidai ni wake. Nilimuuliza mpenzi wangu akasema mwanamke huyo ni rafiki tu. Tangu kisa hicho mpenzi wangu amekuwa kimya kwa karibu wiki mbili sasa. Je, ananichezea?

Kupitia SMS

Sitaki kukuchafua roho, lakini nahisi kuwa mpenzi wako huyo ana mwingine na amekuwa akikuhadaa. Sababu ni kwamba tayari umepigiwa simu na mwanamke mwingine akidai kuwa huyo ni mpenzi wake ingawa amekana na kudai ni rafiki tu. Isitoshe, tangu kisa hicho ameacha kuwasiliana nawe. Hiyo si kawaida kwa mtu anayempenda mwenzake. Ushauri wangu ni kuwa wewe pia unyamaze tu wala usimtafute. Ikipita miezi miwili bila kukupigia simu ujue mpenzi wake hasa ni huyo aliyedai kuwa ni rafiki yake.

 

Nasikitika huenda hanipendi tena!

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 19 na kijana mpenzi wangu ana miaka 24 na tumekuwa wapenzi kwa karibu miezi sita sasa. Tatizo ni kuwa hajali mahitaji yangu, nikimuomba pesa huniambia eti mimi bado ni mdogo sihitaji pesa. Siku za hivi majuzi ameanza kupuuza simu zangu nikimpigia na pia SMS. Nimeanza kuhisi ni kama hanipendi tena lakini ananizungusha tu hataki kunimbia ukweli. Nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Wewe ni mtu mzima sasa na mpenzi wako kukwambia huhitaji pesa ni sawa na matusi. Mapenzi ya dhati ni wahusika kusaidiana kwa hali na mali ili kuyadumisha. Kama unavyosema, tabia ya mwenzako ni dalili kamili za mtu ambaye ameamua kujiondoa katika uhusiano lakini hataki kumwambia mwenzake. Acha kumtafuta, kama anakupenda atakutafuta mwenyewe na akifanya hivyo mpe masharti yako ya kuendelea na uhusiano huo.

Mie nimependana na aliyenizidi umri kwa miaka kadhaa, sijui ni vyema?

Shikamoo shangazi! Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 17 na nimependana na mwanaume ambaye si rika yangu, amenizidi umri kwa miaka kadhaa. Hiyo ni sawa?

Kupitia SMS

Jibu langu ni kwamba hiyo si sawa hata kidogo. Sababu ni kwamba wewe bado ni mtoto na ingawa hujasema, ninaamini kuwa bado ungali shuleni. Katika umri wako huo huna uwezo wa kuelewa masuala ya mapenzi na ushauri wangu ni kuwa usubiri uwe mtu mzima na kama unasoma ukamilishe masomo yako. Mbali na hayo, umri haufai kuwa kikwazo katika uhusiano.