Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Naona aibu kutembea na mke wangu anayenizidi umri

June 4th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nina umri wa miaka 32 na nimeoa mwanamke aliye na umri wa miaka 40. Nilimuoa akiwa na watoto watatu kutokana na uhusiano wa awali na sasa ana mimba ya mtoto wangu. Ingawa ninampenda sana, ninaona aibu kuonekana naye hadharani kwa sababu ya tofauti kubwa ya umri kati yetu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ninaamini ulimuoa mwanamke huyo kwa hiari yako kutokana na mapenzi yako kwake wala hukulazimishwa. Kwa sababu hiyo, huna sababu ya kuona aibu kutembea naye hadharani kwani ndiye chaguo la moyo wako. Bila shaka watu wataongea lakini mwishowe watachoka na kunyamaza.

 

Miye mwanafunzi ila mpenzi ataka asali

Shangazi pokea salamu zangu. Nina umri wa miaka 18 na mimi ni mwanafunzi wa shule ya upili. Kuna kijana tunayependana na ameniambia yuko tayari kunioa nikimaliza masomo. Lakini pia amekuwa akitaka nimtembelee nyumbani kwao tukifunga shule ili aonje asali. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Nimesema mara nyingi kwamba masomo na mapenzi hayatangamani na ukijaribu ni lazima utapoteza moja. Tayari mahaba yamekuchanganya na ndiyo maana umekuja kwangu ukitaka ushauri. Ni kwa njia hiyo ambapo masomo yatakuponyoka kwa sababu hutaweza kumakinika. Hali itakuwa mbaya zaidi ukikubali wito wa mpenzi wako huyo kwani akionja hiyo asali tu utaingiwa na kichaa. Masomo ni muhimu zaidi kwako kwa sasa kwa hivyo yazingatie zaidi na uachane kabisa na mapenzi hadi utakapomaliza.

 

Kidudumtu anatuchonganisha na mpenzi wangu!

Hujambo shangazi? Nina mpenzi ambaye tunapendana kwa dhati. Hata hivyo, kuna rafiki yake ambaye anataka tuwe na mpango wa kando lakini nimekataa. Sasa ameapa kutumia njia yoyote ile kuvunja uhusiano. Juzi alimwambia mpenzi wangu eti ameonja. Mpenzi wangu ameamini na sasa ameamua kuniacha. Nimemwelezea nia ya rafiki yake lakini amekataa kunisikia akisema rafiki yake huyo hawezi kumdanganya. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Sielewi ni kwa nini mpenzi wako anamwamini zaidi rafiki yake kuliko wewe hivi kwamba ameamua kuvunja uhusiano wenu kwa kutegemea udaku wake licha ya wewe kumwelezea ukweli wa mambo. Hata hivyo, kama ameamua muache aende. Wanaume wapo wengi, utapata mwingine mpendane hata zaidi.

 

Nina udhaifu wa kutema wanaume punde baada ya kuanza uhusiano

Shikamoo shangazi! Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 20 na nina shida na wanaume. Shida yenyewe ni kuwa siwezi kudumisha uhusiano na mwanamume kwa zaidi ya mwezi mmoja. Ghafla huanza kumchukia kisha ninamuacha. Sielewi ni kwa nini, nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Hujaelezea hali yako hiyo imeathiri uhusiano wako na wanaume wangapi. Hata hivyo, sidhani kuwa hiyo ni shida hasa. Inawezekana kuwa hakuna kati ya uliokutana nao ambaye alikuwa chaguo la moyo wako na ndiyo maana mahusiano yenu hayakudumu kwa sababu roho yako iliwakataa. Ni jambo la kawaida kwa mtu kuvunja mahusiano kadhaa kabla ya kumpata mwenzake wa maisha. Kuwa na subira na hatimaye utafaulu.

 

Nikiona wanaume huwa ninaingiwa na kichefuchefu

Mambo shangazi? Nina umri wa miaka 24. Nilikuwa na mwanamume mpenzi wangu niliyempenda kwa moyo wangu wote lakini tulikosana na tukaachana mwaka uliopita. Tangu wakati huo sitaki hata kuongea na mwanamume yeyote. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Ingawa hujafafanua, inaonekana kuna jambo baya ambalo mwanamume huyo alikutendea na ambalo lilivunja uhusiano wenu. Ni kwa sababu hiyo ambapo unahisi kama kwamba una kisasi na wanaume wote. Hata hivyo, wewe bado ni mdogo kiumri na ninaamini unahitaji mwanamume katika maisha yako. Jipe muda moyo utulie kisha uufungue tena ili kutafuta mpenzi mwingine.