Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nashuku huyu mwanachuo hanipendi kwa dhati

June 18th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Kuna kijana mwanafunzi mwenzangu katika chuo kikuu ambaye amekuwa akiniambia ananipenda. Mimi pia nina hisia kwake. Hofu yangu ni kuwa huenda hanipendi kwa dhati na pengine ananichezea tu. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Mtu akimpenda mwingine humwambia na kijana huyo tayari amefungua moyo wake na kukueleza anavyohisi. Kama wewe pia unampenda na hakuna jambo linaloweza kukufanya umshuku, basi mwamini kwa sasa.

 

Rafiki adai mpenzi wangu ananisaliti

Hujambo shangazi? Nina uhusiano wa kimapenzi na mwanamume ambaye ninamwamini sana. Hata hivyo, nimeingiwa na baridi baada ya rafiki yangu kuniambia anashuku kuwa ana mwingine. Sijawahi na siwezi kumsaliti kimapenzi na nitashangaa sana nikijua kuwa habari hizo ni za kweli. Nishauri.

Kupitia SMS

Si jambo la busara kumhukumu mtu kutokana na maneno ya kuambiwa tu bila ushahidi wa kutosha. Madai kumhusu mpenzi wako hayana msingi kwani unasema rafiki yako anamshuku tu, hana hakika wa jambo hilo. Ni muhimu uchunguze wewe mwenyewe madai hayo ili ujue iwapo ni ya kweli ama ni uzushi wa mtu anayetaka kuharibu uhusiano wenu.

 

Nimeomba swahiba anisaidie kutafuta mchumba, sijui nimefanya vyema?

Kwako shangazi. Mimi bado sijapata mpenzi ingawa kuna wanaume kadhaa ambao wamekuwa wakinitaka lakini bado sijaamua moyoni ni nani kati yao anayenifaa. Mwanamke rafiki yangu amejitolea kunisaidia kuchagua. Kuna makosa?

Kupitia SMS

Mapenzi yanatokana na hisia za mtu binafsi. Haiwezekani kwamba kinachovutia macho na moyo wako ndicho kinachovutia macho na moyo wa rafiki yako kwa sababu nyinyi ni watu tofauti. Kwa sababu hiyo, sidhani litakuwa jambo la busara kwako kumtegemea akuchagulie mpenzi. Ninaamini kuwa moyoni mwako una sifa za aina ya mwanamume ambaye ungependa kuishi naye. Iwapo ni kweli, basi tumia sifa hizo kuchagua mmoja miongoni mwa wanaokutaka.

 

Nahisi nimeuteka moyo wake kwa jinsi anavyonitupia jicho, nifanye nini?

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 25 na sina mpenzi. Kuna mwanamume tunayefanya kazi pamoja ambaye ameteka hisia zangu kimapenzi. Ninaamini yeye pia ananipenda kutokana na jinsi anavyoniangalia ninapokuwa karibu naye. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Mapenzi yanaweza kutambuliwa kutokana na ishara za kimwili kati ya wahusika. Hata hivyo, hilo huwa halitoshi hadi siku kila mmoja anapoungama kwa mwenzake kuwa anampenda. Kuwa na subira, kama yeye pia anakupenda, siku hiyo itafika.

 

Nasononeka kwani kipusa adai haelewi hisia zangu!

Kwako shangazi. Kuna mwanamke ambaye tumekuwa marafiki wakubwa kwa miaka kadhaa sasa. Nimegundua kuwa ninampenda na sasa ninataka tuwe wapenzi. Nimemdokezea kuhusu hisia zangu kwake lakini anajifanya haelewi. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ninaamini mwanamke huyo ana akili timamu kwa hivyo sielewi unamaanisha nini ukisema anajifanya kuwa haelewi unayomwambia. Mimi nahisi kuwa hataki uhusiano wa kimapenzi kati yenu lakini anashindwa kukwambia kutokana na kwamba nyinyi ni marafiki wakubwa.

 

Amenivunja moyo kwa kuvuruga penzi letu la miaka minne

Shikamoo shangazi! Nimekuwa na mpenzi mmoja tu maishan. Nimeshtuka sana kugundua kuwa mwanamume ambaye nimemwamini kwa miaka minne ya uhusiano wetu ana mpenzi mwingine. Nimevunjika moyo sana, sijui nitafanya nini. Nishauri.

Kupitia SMS

Ninaamini kwamba umezungumza na mwanamume huyo na ukathibitisha kwamba ana mpenzi mwingine. Kama ndivyo, itabidi uachane naye na uendelee na maisha yako.