Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nasikia mpenzi ni mkarimu anagawa asali bila choyo!

August 30th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Ni miezi miwili sasa tangu niingie katika uhusiano na mwanamke ambaye nampenda sana. Hata hivyo, nimepata habari kutoka kwa watu wanaomfahamu vyema kwamba ni mkarimu sana kwa wanaume na wamekuwa wakimtumia na kutoweka. Nifanyaje?

Kupitia SMS

Uamuzi wako utategemea tu ushahidi ulionao kuhusu mienendo ya mwanamke huyo. Huwezi kutegemea fununu kwa sababu zinaweza kuwa za kweli ama za uongo. Jipe muda umchunguze mwenyewe kimya kimya umjue vizuri ili ufanye uchukue hatua inayofaa. Inawezekana wanaoeneza uvumi huo wanaonea wivu uhusiano wenu.

 

Shangazi hafurahii wapenzi ninaopata

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 26 na bado sijaolewa ingawa nimekuwa na wachumba kadhaa. Ninaishi na shangazi yangu ambaye hajaolewa na kila mchumba ninayepata yeye humkataa akidai hanifai. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Umekosea kumruhusu shangazi yako akuamulie kuhusu mwanamume anayekufaa maishani. Wewe ni mtu mzima na unafaa kuamua mwenyewe kuhusu mume unayemtaka. Isitoshe, huyo shangazi yako hajaolewa kwa hivyo sidhani ana uwezo wa kujua mwanamume anayekufaa na asiyekufaa.

 

Adai kunipenda na nilimfumania na kipusa mwingine

Kwako shangazi. Kuna mwanamume ambaye ameniandama kwa muda akitaka tuwe wapenzi ingawa bado sijaamua kuhusu ombi lake. Lakini nimegundua kuwa ananihadaa tu kwani juzi nilipomfumania na msichana mwingine. Baadaye alinitumia ujumbe wa SMS akiomba nimsamehe na kusisitiza kuwa ni mimi tu anayependa. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Hata kama unafikiria kumsamehe, ni muhimu kwanza ujue iwapo kuna chochote kinachoendelea kati yake na msichana uliyewapata pamoja. Ni baada ya hapo ambapo utaweza kufanya uamuzi wa busara.

 

Mume amepunguza mahaba kwangu

Vipi shangazi? Nimeolewa na nimebarikiwa na mtoto mmoja. Mume wangu alikuwa akinionyesha mahaba ya hali ya juu siku za kwanza za ndoa yetu. Lakini amebadilika sana siku hizi ni kama kwamba hana hisia kwangu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Maisha ya ndoa ni sawa tu na mlima, yana kupanda na kushuka. Ni hali ya kawaida miongoni mwa watu wengi kwa mapenzi kati yao kupungua jinsi wanavyoendelea kuishi pamoja na kuzoeana. Ni wakati huo ambapo wahusika wanafaa kuwa wabunifu katika kutafuta mbinu za kuchochea mahaba ili kudumisha ndoa.

 

Sioni penzi hili likidumu

Shikamoo shangazi! Mwanamume tunayependana anafanya kazi mbali. Ninampenda sana lakini nahofia kuwa uhusiano wetu hautaenda mbali kwa sababu imekuwa shida kupata usaidizi wake ninapouhitaji. Nishauri.

Kupitia SMS

Hiyo ni mojawapo ya changamoto za uhusiano kati ya mtu anayeishi mbali na mwenzake. Kuna baadhi ya watu wanaofaulu kudumisha uhusiano kama huo na hatimaye kufunga ndoa ilhali wengine hulemewa na kutafuta maisha kwingine. Kauli yako inaonyesha umeanza kulemewa na una haki ya kujiondoa katika uhusiano huo iwapo unahisi hauna manufaa kwako.

 

Hanionyeshi mapenzi

Kwako shangazi. Kuna mwanamume ambaye nimempenda kwa moyo wangu wote, huu sasa ni mwaka wa pili. Yeye pia ananiambia ananipenda lakini ameshindwa kunionyesha penzi lake kwa vitendo. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Hujaelezea unatarajia vitendo gani kutoka kwa mwanaume huyo ili kuthibitisha penzi lake kwako. Kama unajua unachotaka na hujamwambia, hakuna jinsi ambavyo ataweza kujua. Ni muhimu umwelezee.

 

Nimpende yupi sasa?

Kwako shangazi. Nimependana na mwanamume tunayefanya kazi pamoja na amekuwa akigharamia mahitaji yangu yote. Shida ni kuwa kuna mwanamume mwingine ambaye tumezaa mtoto pamoja na bado ananipenda. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Hiyo yako ni tabia ya mtu asiye na msimamo. Sielewi ni kwa nini uliamua kuanzisha uhusiano mpya ukijua una mpenzi ambaye umezaa naye. Itabidi uamue anayekufaa kati yao ili utulie kwake.