Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nataka kuomba kipusa wangu pesa lakini naogopa

October 25th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nina mwanamke mpenzi wangu ambaye tunapendana sana. Kuna wakati ambapo huwa ninaishiwa sana na pesa lakini naogopa kumuomba hata kama ninajua ako nazo. Je, ni makosa kwa mwanamume kumuomba pesa mpenzi wake?

Kupitia SMS

Kuishiwa si hatia, ni hali ya kawaida ya maisha. Hakuna asiyeweza kupatikana na shida ya pesa, awe mwanamume au mwanamke. Maana ya mapenzi ya dhati ni wapendanao kusaidiana kwa hali na mali. Hutakosea kwa kumfahamisha mpenzi wako kuhusu hali yako ya kifedha. Hiyo hasa itakuwa jinsi nyingine ya kujua iwapo kweli anakupenda.

 

Tuligombana vikali nikamwambia heri tuachane, sasa ataka kunipeleka kwao

Habari zako shangazi? Ni mwaka mmoja sasa tangu nianzishe uhusiano wa kimapenzi na mwanamume fulani. Lakini juzi tuligombana niliposikia kuwa ana mwingine ingawa alikana. Nilimwambia tuachane akakataa. Sasa anataka kunipeleka kwao. Lakini nashangaa, huyo mwanamke mwingine naye atampeleka wapi? Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Kosa ambalo limesababisha ugomvi kati yako na mpenzi wako limetokana na maneno ya kusikia tu, huna ushahidi wowote. Kabla hujamhukumu zaidi, ni vyema kwanza ujue maneno hayo yalitoka kwa nani na aliyatoa kwa nia gani. Sababu ni kwamba kuna watu ambao raha yao ni kudunga sumu urafiki, uhusiano na ndoa za watu wengine ili kuwatenganisha. Mpenzi wako amekana madai hayo na pia amethibitisha kuwa wewe ndiye wake kwa nia yake ya kukupeleka kwao nyumbani kukutambulisha rasmi kwa wazazi na jamaa zake wengine. Unataka nini zaidi? Kama unataka kudumisha uhusiano wako, jiepushe na udaku.

 

Ameniambia ana virusi japo miye sina, ni vibaya tuendelee?

Kwako shangazi. Mwanamume ambaye tumekuwa wapenzi kwa mwezi mmoja sasa aliniambia mwenyewe juzi kwamba ana virusi vya Ukimwi. Tumekuwa tukitumia kinga lakini pia niliamua kupimwa na nikapatikana kuwa niko sawa. Alisema aliamua ni vyema nijue kwa sababu ananipenda. Mimi pia nampenda na sina mpango wa kumuacha kwa sababu ya hali yake. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Hatua ya mpenzi wako ya kufichua hali yake kwako ni thibitisho kuwa anakupenda kwa dhati. Kuna watu wengi wanaoshindwa kufanya uamuzi kama huo wakihofia kwamba wataachwa. Kama umeamua kwamba mtaendelea na uhusiano wenu, ni muhimu mtafute ushauri kutoka hospitalini ili mjue jinsi ya kuendesha uhusiano wenu na labda baadaye katika ndoa bila yeye kukuambukiza.

 

Mama mkwe hanipendi, sina raha

Kwako shangazi. Nimekuwa katika ndoa kwa miaka mitatu na nina mtoto mmoja. Hata hivyo, sina raha katika ndoa yangu kwani mama mkwe ananichukia sana. Sijui kiini cha chuki yake kwangu kwani sijawahi kumkosea. Jambo linalonitatiza moyoni zaidi ni habari kwamba anamtafutia mume wangu mke mwingine. Mume wangu anamsikiliza na kumwamini sana mama yake na nahofia kuwa muda si mrefu ndoa yangu itatumbukia nyongo. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Iwapo hiyo hasa ndiyo hali halisi ya mambo, nahisi kuwa ndoa hiyo inaelekea ukingoni na una kila sababu ya kuwa na hofu. Kama tatizo pekee lingekuwa ni chuki ya mama mkwe, ungesuluhisha hilo kwa kuishi mbali kidogo naye ili kuepuka kero zake. Lakini kama mume wako anafuata ushauri wake na kuna mpango wa kumtafutia mke, basi hapo kuna shida. Ushauri wangu ni kuwa uketi chini na mume wako mjadili mambo hayo kwa uwazi ili mjue mapema mwelekeo wa ndoa yenu ya kufanya maamuzi yanayofaa.

 

Nimegundua mke ana dume la pembeni

Shangazi pokea salamu zangu. Mimi nimeoa lakini nimegundua kuwa mke wangu ana mpango wa kando. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Chunguza ujue sababu yake ya kuwa na uhusiano nje ya ndoa. Labda kuna mahitaji fulani ambayo wewe kama mume wake umeshindwa kumtimizia na amelazimika kutafuta msaada kutoka nje. Kama hakuna anachokosa, basi hiyo yake ni tamaa na ni hatari kuishi na mtu kama huyo hasa enzi hizi za Ukimwi.