Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nataka kutafuta sponsa wa majukumu tu si mapenzi

January 21st, 2020 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Tafadhali nahitaji ushauri wako. Mwanamume mpenzi wangu ananipenda sana na amejitolea kwa hali na mali kudumisha mapenzi yetu. Hata hivyo, mahitaji yangu ya kifedha yamekuwa mengi na yameanza kumlemea. Nafikiria kutafuta mwingine wa kunifaa kwa njia hiyo tu bila kujali hisia zangu kwake. Hofu yangu ni kuwa mpenzi akijua ataniacha. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Nitakwambia ukweli. Hiyo yako ni tamaa na tamaa ilimuua fisi. Unakubali mwenyewe kuwa mpenzi wako anajaribu awezavyo kukutimizia mahitaji yako ya kifedha kwa lengo la kudumisha uhusiano wenu. Huo si wajibu wake kwa sababu wewe ni mpenzi tu si mke wake. Iwapo kweli unampenda kama unavyodai, hufai kuwa na uhusiano wa pembeni kwa manufaa ya pesa. Uhusiano unaolenga pesa pekee bila kujali mapenzi ni ukahaba. Punguza mahitaji yako na utosheke na anachokupa.

 

Mimi na mpenzi wa kwanza tumejaribu kuachana lakini wapi, japo sote tuko na familia sasa

Kwako shangazi. Nimeolewa na nina watoto wawili. Hata hivyo, nimeshindwa kuachana na mpenzi wangu wa kwanza ambaye pia ana familia. Kwa miaka kadhaa sasa, tumekuwa tukiendesha uhusiano wetu pembeni na hofu yangu kubwa ni kwamba mume wangu ama mke wake atagundua. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Huo ni mchezo hatari kwa watu walio katika ndoa. Mimi kamwe siwezi kuunga mkono uhusiano wa aina hiyo kwani huo si uhusiano bali ni usaliti na ulaghai wa kimapenzi. Hujaelezea ni kwa nini mwanamume huyo hakukuoa wewe iwapo mnapendana namna hiyo. Kama unathamini ndoa yako, huna budi kuvunja mara moja uhusiano huo kwani siku moja utagunduliwa tu.

 

Nimemuingiza boksi baada ya kumrushia mistari kwa muda mrefu, lakini sasa ninashuku kiini chake kunikubali

Vipi shangazi? Kuna mwanamke ambaye nimemtongoza kwa karibu miaka mitatu na hatimaye akakubali. Hata hivyo, ninashuku iwapo kweli ananipenda kwani nimemuomba mara kadhaa anitembelee kwangu lakini amekuwa akinizungusha tu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kuna watu wanaochukua muda mrefu kufanya maamuzi. Umesema kuwa imekuchukua miaka mitatu kumshawishi awe mpenzi wako na huenda hali ikawa hiyo hiyo kabla hajakubali kufika nyumbani kwako. Kuwa na subira.

 

Rafiki kanifichulia jinsi dume langu limeishi kunihadaa na vimada, sasa huyo ataka tuwe wapenzi

Kwako shangazi. Mwanamume mpenzi wangu ambaye ninamwamini sana amenivunja moyo. Kuna rafiki yake ambaye amekuwa akiniambia kuwa si mwaminifu kwangu lakini sikuamini. Sasa nimeamini baada ya kunitumia kwa simu picha za mpenzi wangu akiwa na wanawake wengine katika sehemu tofauti za burudani. Ananiambia ananipenda na anataka niachane naye kisha tushikane tuwe wapenzi. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Iwapo picha ulizotumiwa ni za kweli, basi umepata ushahidi wa kutosha wa kuonyesha kwamba mpenzi wako si mwaminifu, anakucheza na wanawake wengine. Hata hivyo itakuwa muhimu umkabili ili ujue ukweli wa picha hizo. Labda rafiki yake ametumia ujanja fulani kuharibu uhusiano wenu ndipo akupate.

 

Niliyezaa naye hapo zamani amekataa kabisa nisimuone mtoto wangu

Shangazi ni matumaini yangu kwamba wewe ni mzima. Nilikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke fulani na tukazaa mtoto pamoja. Baadaye tuliachana na akaolewa na mwanamume mwingine. Ninampenda sana mtoto wangu lakini mwanamke huyo amekataa naye. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Mlipomzaa mtoto, mwanamke huyo alikuwa mpenzitu, hakuwa mke wako. Hali kwamba ameolewa na mwanamume mwingine, mtoto huyo sasa ni wake na mume wake na huna haki wala mamlaka yoyote juu yake ingawa ni wako kumzaa. Ungekuwa na haki kwake tu kama ungekuwa umemuoa mama yake wakati alipozaliwa.