Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nataka mke ahamie mashambani lakini amekataa

March 18th, 2020 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nilimpa mimba mwanamke mpenzi wangu na nikamuoa kwa sababu nampenda kwa dhati. Ingawa nimeajiriwa, mshahara wangu ni mdogo na nimeanza kulemewa kugharamia maisha yetu mjini. Nimemshauri mke wangu aende kwetu mashambani lakini amekataa akidai hataki kuwa mbali na familia yake. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Mke wako anakuhitaji katika maisha yake kila wakati. Hiyo ndiyo maana anakwambia hataki kuishi mbali nawe. Huko mashambani unakotaka aishi kuna wanaume wanaotegea wanawake walio na upweke ambao waume zao wanaishi mijini. Ni muhimu kuishi karibu na familia yako. Tafuta namna ya kugharamia maisha yao. Kama mke wako hana kazi, mtafutie biashara hata kama ni ndogo tu ili kuongezea mapeto yenu.

 

Anasema atajiua kwa kuwa nimemuacha ilhali niligundua ana mpenzi mwingine

Vipi shangazi? Naomba ushauri wako. Kuna mwanamke ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka miwili na nimegundua ana uhusiano wa kisiri na mwanamume mwingine. Nimeamua kumuacha na sasa amekuwa akinitumia SMS akiniambia nikimuacha atajitoa uhai. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Iwapo umethibitisha kuwa mwanamke huyo ana mpenzi wa pembeni, asikuhangaishe kwa vitisho vyake eti atajiua. Kama anakupenda kiasi cha kujitoa uhai hangekuwa na uhusiano wa pembeni. Mpuuze na uendelee na maisha yako.

 

Mume atishia kuniua baada ya kuachana naye, nisaidie

Vipi shangazi? Mimi nilikuwa nimeolewa lakini niliachana na mume wangu hivi majuzi. Hatukuwa tumepata mtoto wala hajanilipia mahari. Tangu tuachane amekuwa akitishia kuniua. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hujaelezea kilichowafanya muachane wala sababu zake za kukutishia maisha. Hata hivyo, hakuna mtu aliye na haki ya kumtishia maisha mwenzake hata kama amemkosea nini. Usipuuze vitisho vyake hivyo kwani huenda akavitekeleza asipokanywa. Piga ripoti kwa polisi ili achukuliwe hatua za kisheria na kukomeshwa.

 

Nimemzuzua mume wa wenyewe sasa ataka kunioa…

Vipi shangazi? Kwa miaka miwili sasa nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamume ambaye ameoa. Penzi letu limenoga sana na anasema atamuacha mke wake ili anioe. Ingawa nampenda, nia yangu si kuvunja ndoa yake. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Usiseme kwamba huna nia ya kuvunja ndoa ya mwanamume huyo kwani uliivunja siku uliyokubali kuanzisha uhusiano naye ukijua vizuri kuwa ni mume wa mwenyewe. Kama si wewe kuingia katika maisha yake, hangewazia kumuacha mke wake. Inaonekana umemzuzua kimapenzi na kiasi cha kumfanya afikirie kuacha familia yake. Kama kweli unajali ndoa yake, mwambie hivyo kisha uvunje mara moja uhusiano huo na ukatize kabisa mawasiliano kati yetu.

 

Simtaki lakini hasikii!

Shikamoo shangazi! Kuna mwanaume ambaye amekuwa akinitaka kimapenzi ilhali mimi sina hisia kwake. Nimemwambia mara nyingi kuwa siwezi lakini hataki kuelewa. Nililazimika kuhama nyumba nilimokuwa nikiishi kwani alikuwa akija kwangu karibu kila siku. Sasa amebaki kunisumbua kupitia kwa simu akidai eti hali wala halali kwa sababu yangu. Tafadhali nishauri kuhusu jinsi ninavyoweza kumuepuka.

Kupitia SMS

Mwanamume huyo ataendelea kukusumbua kwa tu bora tu ana nambari yako ya simu. Jinsi pekee ya kuepuka simu zake ni kubadilisha nambari yako na uhakikishe hutampa mtu anayeweza kumpatia.

 

Hapokei simu zangu

Shikamoo shangazi! Nina uhusiano na msichana aliyemaliza shule ya upili mwaka jana. Tumekuwa tukiwasiliana kwa simu mara kwa mara lakini amekatiza mawasiliano ghafla, nikimpigia simu au kumtumia ujumbe hajibu. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni jambo la kawaida kwa mtu kubadili msimamo kuhusu mambo mbalimbali yakiwemo mahusiano. Inawezekana kuwa mwenzako ameamua kujiondoa katika uhusiano huo na ndiyo maana amekatiza mawasiliano. Kama amekataa kujibu simu, mtafute umuulize kinachoendelea.