Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Natamani mume ila naogopa sana kuolewa tena

October 10th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nina umri wa miaka 30 na nina mtoto mmoja. Nilikuwa nimeolewa lakini nikamuacha mume wangu baada ya kugundua kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine. Muda si mrefu nilipata habari kwamba amemuoa mwanamke huyo. Natamani sana kuwa na mume lakini naogopa kujipata katika hali hiyo tena. Nishauri.

Kupitia SMS

Maisha ya ndoa yanaweza kuwa magumu hasa mmoja wa wahusika akiwa mtu asiye mwaminifu. Hatua uliyochukua baada ya kugundua kuwa mume wako hakuwa mwaminifu ndiyo iliyofaa kwa hivyo usijute. Ninaelewa kuwa uliingiwa na woga baada ya kisa hicho lakini pia kumbuka kuwa wewe bado ni mchanga na si vyema kuendelea kuishi maisha ya upweke. Fungua moyo wako tena kwa lengo la kupata mume mwingine kwa sababu si wanaume wote walio na tabia sawa na ya mume wako wa awali. Pili, kuwa na subira unapotafuta. Kila la heri.

 

Alidai kabila ni kero kwake, sasa ataka turudiane lakini mie nimepata mwingine

Shikamoo shangazi! Nilimuacha mwanamume aliyekuwa mpenzi wangu mwaka uliopita aliponiambia kuwa hawezi kuoa mwanamke kutoka jamii tofauti na yake. Nilishangaa juzi aliponitembelea kazini kwangu kuniomba turudiane. Nilipomuuliza kuhusu msimamo wake uliotufanya tuachane aliniambia kuwa amebadili nia. Bado nampenda lakini nimepata mwingine ingawa tumejuana kwa muda mfupi tu. Nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Inaonekana mwanamume huyo ameweka kwenye mizani mapenzi na asili ya kijamii akagundua kuwa mapenzi yana uzito zaidi. Hiyo ndiyo maana ameamua kubadili msimamo wake wa awali na kurudi kwako. Unasema kuwa bado unampenda kwa hivyo itabidi uchague kati yake na uliye naye. Kama utamchagua yeye, hakikisha amekuelezea vizuri ni kwa nini ameamua kubadili nia kuhusu tofauti yenu ya kijamii.

 

Nina hofu huenda nimeambukizwa HIV

Hujambo shangazi? Nimekuwa na uhusiano kwa miezi kadhaa sasa. Juzi mwanamume rafiki yangu aliniambia kuwa mwanamume aliyekuwa na uhusiano na mpenzi wangu ana virusi. Kama hiyo ni kweli, inawezekana mpenzi wangu aliambukizwa na nahofia mimi pia ameniambukiza kwa sababu tumekuwa tukirusha roho bila kinga. Nina wasiwasi sana, tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Ni hatari kwa mtu kufanya maamuzi kutokana na habari ambazo hazijathibitishwa. Utakosea kwa kukata kauli kuwa mpenzi wako aliambukizwa virusi na tayari amekuambukiza. Utaweza kujua hali yako tu ukipimwa na ushauri wangu ni kuwa ufanye hivyo mara moja. Ni muhimu pia umpashe habari hizo mpenzi wako ili naye apimwe ajue hali yake.

 

Ametoweka baada ya kumfahamisha nina mimba, nifanyeje?

Shikamoo shangazi! Nimekuwa na uhusiano na mwanamume fulani na amekuwa akiniahidi kuwa atanioa. Nimegundua hivi majuzi kwamba nina mimba yake na nilipomwambia akatoweka na kukatiza mawasiliano. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ni wazi kwamba mwanamume huyo ameamua kukutoroka baada kugundua una mimba yake kwa sababu hataki kuwajibika kulea mtoto. Wewe pia ulikosea kupata mimba nje ya ndoa. Jitayarishe tu kulea mwanao peke yako kwani baba yake amekukwepa.

 

Tulikosana na mimi nimeomba radhi, lakini binti hataki kabisa mambo yangu

Vipi shangazi? Kuna mwanamke aliyekuwa mpenzi wangu lakini tukakosana. Bado moyo na mawazo yangu yako kwake na juzi nilimpigia simu kumuomba msamaha ili turudiane. Lakini alinionya nimkome na nisiwahi tena kumpigia simu. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Uhusiano wa dhati hutokana na kila mmoja kuwa na hisia kwa mwenzake. Kama mwanamke huyo hana hisia tena kwako na amekwambia uwache kumfuata, huwezi kubadili msimamo wake hata kama bado unampenda. Ushauri wangu ni kuwa uondoe mawazo na moyo wako kwake na utafute mwingine.