Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Ndiye wangu wa kwanza na nimegundua ni mkware wa kutupwa

February 20th, 2020 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nimekuwa na mpenzi kwa karibu mwaka mmoja. Amekuwa akiniahidi kuwa atanioa ingawa bado hajanitambulisha kwa wazazi wake. Pili, nimegundua kwamba yeye si mwaminifu kwangu. Juzi nilimfumania mahali akiwa na mwanamke mwingine na nilipomuuliza akaungama kuwa huyo pia ni mpenzi wake. Ndiye mpenzi wangu wa kwanza na tukio hilo limeniumza sana moyoni. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Si jambo la kawaida kwa mtu kufumaniwa kisha kukubali makosa yake mara moja. Hali kwamba mpenzi wako aliungama papo hapo ni ishara kuwa imekuwa tabia yake kuwahadaa wanawake huku akiwatumia vibaya. Ninaelewa unavyohisi baada ya kujua kuwa umechezewa. Lakini huo kamwe si mwisho wa maisha yako. Ondoa kabisa mawazo yako kwake ndipo uweze kumsahau.

 

Hawezi kupata mtoto tena na hilo lanikwaza

Habari zako shangazi? Nilimuoa mke wangu akiwa na mtoto ambaye alizaa na mpenzi wake wa awali. Tumeishi pamoja kwa miaka minne sasa na hajapata mtoto mwingine. Tuliamua kutafuta msaada kutoka kwa mtaalamu wa afya ya uzazi na ikagunduliwa kuwa hawezi kupata mtoto tena. Nilitamani sana kuwa na watoto wangu na hali yake hiyo imenivunja moyo. Nafikiria kuoa mwanamke mwingine ingawa sijamwambia. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hali ya mke wako ni majaliwa tu, sio kupenda kwake. Inaweza kumpata mtu yeyote awe ni mwanamke ama mwanamume. Kwa sababu hiyo, usimchukie wala kumuacha kwa sababu hiyo. Mapenzi ya dhati yanavumilia hali yoyote ile. Ni bahati kwamba mna mtoto ingawa si wako kumzaa. Kama umeamua kuoa mke mwingine, usifanye hivyo kwa jinsi ambayo itamuumiza moyoni mke wako. Ni muhimu umhusishe kikamilifu kupitia mashauriano na makubaliano.

 

Alinikosea wiki mbili zimepita hatujaongea

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 30 na nimekuwa na mpenzi kwa mwaka mmoja sasa. Hata hivyo, alinikosea majuzi na kwa wiki mbili sasa hatujaonana wala kuzungumza. Amekuwa akinipigia simu na kunitumia SMS akiomba msamaha lakini nimeshindwa kumjibu. Sijui nitafanya nini kwani nampenda kwa dhati na sidhani itakuwa rahisi kupata mwingine kama yeye. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Unasema kuwa mpenzi wako alikukosea lakini hujaelezea hasa alikukosea kwa njia gani hivi kwamba hata hutaki kuzungumza naye. Kwa upande mwingine, unakubali kuwa bado unampenda. Nijuavyo ni kwamba hakuna kosa lisiloweza kusamehewa. Jipe muda wa kutosha utathmini moyo wako uone kama unaweza kumsamehe ili mrudiane. Ukiamua kuwa huwezi kumsamehe ni vyema pia umwambie badala ya kumnyamazia.

 

Nilipekua simu yake nikakuta jumbe tele za wanaume wengine

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 25 na nimekuwa na mpenzi kwa mwaka mmoja sasa. Nampenda sana lakini imebidi nimuache. Sababu ni kuwa amekuwa akipigiwa simu na wanaume wanaodai kuwa wapenzi wake na nikimuuliza anakana. Hatimaye nilipata nafasi ya kukagua simu yake na nikapata jumbe za kimapenzi kati yake na wanaume wengine watatu. Amejaribu kuniomba msamaha akitaka turudiane lakini siwezi kumwamini tena. Nishauri.

Kupitia SMS

Iwapo umethibitisha kupitia kwa simu yake kwamba mpenzi wako ana uhusiano na wanaume wengine, sidhani ungependa aendelee kukuchezea hata kama unampenda. Kama kweli anathamini uhusiano wenu, angeacha tabia hiyo mara tu ulipomshuku badala ya kukana na kusubiri uthibitishe. Unaweza kumsamehe lakini shida ni kuwa amezoea tabia hiyo na huenda itakuwa vigumu kwake kuacha. Ni heri umuondoe kabisa katika maisha yako.

 

Nimegundua mke anagawa asali nje

Shangazi pokea salamu zangu. Mimi nimeoa lakini nimegundua kuwa mke wangu ana mpango wa kando. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Chunguza ujue sababu yake ya kuwa na uhusiano nje ya ndoa. Labda kuna mahitaji fulani ambayo wewe kama mume wake umeshindwa kumtimizia na amelazimika kutafuta msaada kutoka nje.