Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nikimuoa anaweza kumrudia mumewe baadaye?

May 31st, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

MAMBO shangazi? Nimempendana na mwanamke aliyeachana na mume wake. Alirudi kwao na mtoto ambaye amezaa na mwanamume huyo na ameapa kwamba hatawahi kumrudia. Wazazi wetu wanafahamu kuhusu uhusiano wetu na wanaunga mkono mpango wetu wa kuoana. Hofu yangu ni kwamba ninaweza kumuoa kisha abadili nia baadaye arudi kwa mume wake. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, inaonekana kuwa mwanamke huyo ameamua kwamba ndoa yake ya awali imekwisha na anataka kuanza maisha mapya ya ndoa. Si jambo la kawaida kwa mwanamke kuacha ndoa akiwa na watoto kwa sababu si jambo rahisi kuwalea peke yake. Kama mnapendana na uko tayari kumuoa pamoja na mtoto wake sioni tatizo lolote. Isitoshe, unasema mmepata radhi za wazazi wenu na pia ameapa mwenyewe kuwa hatamrudia mumewe. Kuwa na imani.

 

Nilimwahidi nitakuwa wake, sasa hisia hazipo

Hujambo shangazi? Nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na kijana fulani na nimekuwa nikimuahidi kuwa tutaoana nikimaliza masomo. Hatimaye nimemaliza masomo lakini sidhani nitaweza kutimiza ahadi yangu kwake kwa sababu sina hakika kuhusu hisia zangu kwake. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Licha ya kwamba ulikuwa umemuahidi ndoa kijana huyo, una haki ya kubadili nia kwa sababu huwezi kumpenda kama huna hisia kwake. Ni muhimu umwambie ukweli ili aondoe mawazo yake kwako.

 

Nataka sasa tugeuze stori iwe ya mapenzi

Vipi shangazi? Kuna msichana ambaye tumekuwa marafiki wakubwa na siku za hivi majuzi nimeanza kuwa na hisia kwake; nataka tuwe wapenzi. Nilimdokezea jambo hilo lakini amekuwa akipinga ingawa shingo upande akidai tumezoeana kama marafiki na anaona vigumu kugeuza urafiki huo kuwa mapenzi. Nathamini urafiki wetu kwa hivyo sitaki kumsukuma sana. Hata hivyo, bado ninaona matumaini. Nishauri.

Kupitia SMS

Mara nyingi mahusiano ya kimapenzi hutokana na watu kuwa marafiki kwanza na hatimaye wapenzi. Hata kama anakupenda hawezi kukubali ghafla tu kwani hiyo si kawaida ya wanawake. Ndiyo maana unasema anapinga shingo upande. Ushauri wangu ni kuwa umpeleke taratibu tu, kama ana hisia kwako hatimaye atameza chambo.

 

Nashangaa mabinti wathamini pesa sana!

Shikamoo shangazi! Mimi ni mwanamume na nimehitimu umri wa kuwa na mpenzi. Nimekuwa nikitafuta mwanamke wa kuoa lakini nimeshangaa kwamba siku hizi wanawake wengi wanathamini pesa zaidi ya mapenzi. Je, nitaweza kupata mwanamke anayenipenda bila kuweka pesa mbele?

Kupitia SMS

Ni kweli kuwa wanawake wa siku hizi wameweka mbele pesa na hawajali kamwe kuhusu umuhimu wa mapenzi ya dhati. Hiyo ndiyo mojawapo ya sababu za ndoa nyingi kusambaratika kwa sababu zilijengwa kwa msingi wa pesa badala ya mapenzi. Hata hivyo, usikate tamaa kwani bado kunao wachache wanaoelewa umuhimu wa mapenzi ya dhati. Ushauri wangu ni kuwa utafute bila kuonyesha pesa zako ili utakayempata ujue amekubali kwa kukupenda wala si kwa ajili ya pesa.

 

Nawindwa kimapenzi hata na walimu wangu

Shikamoo shangazi! Mimi ni msichana mwanafunzi wa shule ya upili. Kuna shida ambayo ninataka unitatulie. Baadhi ya walimu wangu wa kiume na wanafunzi wenzangu wamekuwa wakiniandama wakitaka tuwe wapenzi. Nimewaambia sitaki lakini hawaachi kuniandama. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hiyo ni changamoto kubwa kwa wasichana kama wewe walio na msimamo mkali kuhusu wanachotaka maishani. Nitakwambia ukweli, kwamba wanaume wataendelea kukuandama maishani na huwezi kuwazuia. Hata hivyo, usikubali kabisa kuwapa nafasi. Shikilia msimamo wako huo hadi utakapomaliza masomo na kuwa tayari kwa uhusiano ndipo uchague. mwenyewe anayekufaa.