Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nikiomba pesa sipewi, lakini 'atachafua' meza baa

April 3rd, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nina uhusiano na mume wa mtu na tunapendana sana. Lakini nikitaka msaada wa pesa kutoka kwake huwa anaona vigumu. Hata hivyo tunapoenda nje kwa burudani huwa anatumia pesa nyingi kwa chakula na vinywaji. Je, ananipenda kweli ama ananitumia?

Kupitia SMS

Mtu anayekupenda anafaa kuwa tayari kukusaidia kwa hali na mali. Kama huyo wako anashughulikia kiu ya pombe pekee, basi fikiria tena kwani huenda ni kweli anakutumia.

 

Anifuatafuata na simtaki, nifanyeje?

Kwako shangazi? Kuna mwanamume ambaye amekuwa akinitaka lakini mimi simtaki. Sijui alivyopata nambari yangu ya simu na amekuwa akinisumbua kwa SMS za kimapenzi. Nimemkanya lakini hataki kusikia. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Kama umemkataa kupitia kwa SMS na hataki kusikia, mtafute umwambie uso kwa uso kwamba humtaki na akome kukufuata. Muonye pia kwamba akiendelea utapiga ripoti ashtakiwe kwa kukuhangaisha kimapenzi.

 

Eti alitaka tu mtoto sasa hana haja nami

Kwako shangazi. Nimeoa kwa miaka miwili sasa na tumejaliwa mtoto mmoja. Tangu tupate mtoto huyo, mke wangu amegeuka sana hana shughuli nami. Juzi nilimuuliza akasema hana hisia zozote kwangu eti alitaka tu nimpe mtoto. Matamshi yake hayo yameniuma sana moyoni. Nishauri.

Kupitia SMS

Iwapo amekwambia wazi kuwa hana hisia kwako, hiyo ina maana kuwa hana manufaa kwako kama mke na nakutahadharisha kuwa hali itazidi kuwa mbaya jinsi miaka inavyosonga. Mnaweza kukubaliana muachane utafute mke bora tu uendelee kugharamia malezi ya mtoto wenu.

 

Shangazi nisaidie kutafuta mchumba

Shangazi pokea salamu zangu. Mimi nina umri wa miaka 26 na niko tayari kufunga ndoa. Ninajua unapokea jumbe nyingi za wanawake wanaotaka kuolewa. Tafadhali nisaidie kutafuta mchumba.

Kupitia SMS

Mapenzi na ndoa ni suala la kibinafsi kwa hivyo mtu ndiye anayejitafutia mke au mume. Ni kweli ninapokea jumbe za wanawake na wanaume wanaotafuta wachumba lakini siwezi kukuchagulia kwa sababu wewe ndiye unajua sifa za mwanamke unayetaka awe mke wako.

 

Napenda wanawake sana ila bado singo

Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 40 na bado sijaoa. Shida yangu ni kuwa ninapenda sana wanawake na sidhani nitaweza kutulia hata nikioa. Nishauri.

Kupitia SMS

Wewe ni binadamu wala si mnyama na unafaa kudhibiti hisia za mwili wako. Kama huwezi, basi utaishi bila mke kwa sababu hakuna mwanamke mwenye akili zake timamu ambaye atavumilia tabia yako hiyo.

 

Amekataa nichote maji, sijui fomu gani

Nina mpenzi ambaye tumekuwa pamoja kwa miaka mitatu sasa na tunafanya mambo yote pamoja isipokuwa tu amekataa nichote maji. Nimejaribu kila mbinu nimeshindwa. Sijui ana mpango gani.

Kupitia SMS

Nijuavyo ni kwamba subira inavuta heri. Kama mnashirikiana kwa mambo mengine yote, tosheka kwa hayo kwanza kwani kuna mambo ambayo hayahitaji pupa. Kumbuka kuwa mvumilivu hula mbivu.

 

Anung’unika jembe fupi, halilimi vizuri

Shangazi nina mpenzi tunayependana sana na tumechumbiana kwa nia ya kufunga ndoa hivi karibuni. Tatizo ni kuwa amekuwa akinung’unika kuhusu jembe langu fupi akisema linashindwa kulima vizuri. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Kwanza, ondoa fikira kwamba shida hiyo inatokana na jembe lako fupi. Sababu ni kuwa kuna walio na majembe makubwa ambao pia wanashindwa na kazi. Kuna usemi kuwa mchagua jembe si mkulima. Unachofaa kufanya ni kujifunza mbinu ya kulitumia kutekeleza kazi hiyo kikamilifu. Itakuwa vyema zaidi ukimshirikisha mwenzako.