Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Niliacha mume wangu, nikashikana na rafikiye

September 5th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nina umri wa miaka 28 na tuliachana na mume wangu miezi sita iliyopita tukiwa na mtoto mmoja. Sina mpango wa kurudiana naye na kuna rafiki yake mkubwa ambaye anataka tuwe na uhusiano wa pembeni kwa sababu ameoa. Ninampenda lakini mke wake ananijua na nahofia atagundua. Nishauri.

Kupitia SMS

Ninaelewa kuwa umeingiwa na upweke baada ya kuachana na mume wako. Hata hivyo, mapenzi ya pembeni na waume wa wenyewe ni ya muda tu tena ni hatari. Sababu ni kwamba mke wake atagundua na hujui atachukua hatua gani. Naona wewe bado ni mwanamke mchanga na unaweza kuolewa tena bora tu uwe na nia na subira.

 

Mama anapinga vikali penzi langu la pembeni

Hujambo shangazi? Nina mwanamume ambaye tunapendana sana ingawa ameoa nami pia nimeolewa. Sababu yangu ya kuwa na mpango wa kando ni kwamba nimegundua kuwa simpendi mume wangu. Mama yangu anamjua mwanamume huyo na pia kuhusu uhusiano wetu na anaupinga vikali. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Ndoa isiyo na mapenzi na maelewano haiwezi kuitwa ndoa. Unasema kuwa umeanza uhusiano nje ya ndoa yako kwa sababu humpendi mume wako. Hiyo ina maana kuwa mawazo yako hayamo tena kwenye ndoa yako ingawa mume wako hajui. Mama yako anapinga uhusiano wako na mwanamume huyo kwa sababu anajua ni haramu na utaharibu ndoa yako. Kama umechoka na ndoa hiyo, ni heri umwambie mume wako ili muachane kwa amani kisha utafute mwanamume mwingine akuoe badala ya kuwa na uhusiano wa kando na mume wa wenyewe.

 

Aligawa nikamtema, ila sasa namtaka tena

Shikamoo shangazi! Nilikuwa na mwanamke niliyempenda sana lakini nikamuacha nilipogundua kuwa alimgawia asali mwanamume mwingine. Sasa anataka turudiane. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Usaliti wa kimapenzi hasa kutoka kwa mtu unayempenda kwa dhati huuma sana. Uamuzi wako utategemea iwapo bado unampenda msichana huyo na iwapo unaweza kumsamehe kosa lake bora tu akuahidi kuwa hatawahi kurudia. Zingatia hayo kisha ufanye uamuzi unaofaa.

 

Naona nimwache ingawa nampenda

Vipi shangazi? Nina mpenzi ninayempenda kwa dhati. Hata hivyo nimesikia fununu kuwa ana uhusiano na mwanamke mwingine. Nafikiria kumuacha kwani sitakubali kuchezewa. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Si vyema kuchukua hatua kwa kuzingatia fununu. Inawezekana kwamba wanaoeneza habari hizo ni maadui zake na nia yao ni kvuruga uhusiano wenu. Itakuwa bora ukimuuliza mwenyewe.

 

Mahaba na mume wa mtu yamenoga ajabu!

Hujambo shangazi? Nina uhusiano na mume wa mtu na tunapendana sana. Huu ni mwaka wa pili sasa na kusema kweli amenizuzua kwa penzi lake. Hofu yangu ni kwamba mke wake atajua na kuvuruga uhusiano wetu. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ni ajabu kuwa unahofia kuwa mke wa mpenzi wako atagundua na kuvuruga uhusiano wenu haramu ilhali wewe unataka kuvuruga ndoa yao halali. Ukweli ni kuwa hatimaye atajua na utajipata mashakani. Achana na mume wa wenyewe utafute wako.

 

Niliyemtema sababu ya ukware wake ameanza kuvuruga mambo yangu

Nilikuwa na mpenzi lakini nikamuacha nilipogundua alikuwa akinichezea na wanaume wengine wakiwemo marafiki zangu. Nilibahatika nikapata mwingine ambaye tunapendana sana na nimepanga kumuoa. Sasa huyo niliyemuacha ameanza kuingilia uhusiano wetu kwa kumpigia simu mpenzi wangu akidai bado ananipenda na atafanya chochote kile kuhakikisha amenipata tena. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni makosa kwa mpenzi wako wa zamani kuanza kuingilia uhusiano wenu ilhali mliachana tena kutokana na tabia zake mbovu. Ingawa hujasema alitoa wapi nambari ya simu ya mpenzi wako, itabidi umtafute umkanye vikali akome.