Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nilidhani baada ya mke kumuacha angenioa mimi

April 11th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nilianzisha uhusiano wa kimapenzi na mwanamume aliyeoa na kwa bahati mbaya mkewe akagundua uhusiano wetu kisha akamuacha. Aliahidi kunioa lakini sasa hazungumzii tena jambo hilo, na pia naona hisia zake kwangu zimepungua ikilinganishwa na hapo awali. Je, inawezekana kuwa anataka kumrudia mkewe? Nishauri.

Kupitia SMS

Mapenzi yanayohusisha mtu aliyeoa ama aliyeolewa huongozwa na tamaa wala si ya dhati. Mapenzi ya mwanamume huyo kwa mke wake aliyemuacha kwa ajili yako ni ya dhati na ni lazima aliingiwa na baridi alipoachwa. Tabia yake ya sasa kwako ni ishara kuwa huenda anafikiria namna ya kumrudia mke wake. Usiweke Imani sana kuhusu ahadi yake ya kukuoa.

 

Amebadilika sana baada ya kupata kazi

Vipi shangazi? Mimi na mwanamke mpenzi wangu tulimaliza masomo ya chuo kikuu mwaka uliopita. Mapema mwaka huu mwenzangu alibahatika akapata kazi. Tangu aajiriwe, mpenzi wangu amebadilika ghafla, mara nyingi nikimpigia simu huwa hajibu ama anajibu kwa dharau. Nafikiri amepata mwingine na nina uchungu sana moyoni. Nishauri.

Kupitia SMS

Hizo ni dalili za kutosha kwamba mpenzi wako amebadili nia yake kwako, awe amepata mwingine au la. Haina haja ya kuendelea kuhangaika kuhusu mtu asiyekujali la sivyo utaendelea kuumiza bure moyo wako. Itabidi umsahau na uendelee na maisha yako.

 

Niliolewa lakini wa zamani ananitafuta

Hujambo shangazi? Kuna mwanamume tuliyekuwa wapenzi wa dhati tukiwa katika chuo kikuu na kwa wakati fulani tuliamini kuwa hatimaye tutaoana. Lakini baada ya kumaliza masomo nilipendana na mwingine na akanioa. Sasa mpenzi huyo wa awali amekuwa akinipigia simu akitaka tukutane. Mimi sasa ni mke wa mwenyewe na nahofia tukikutana kuna hatari ya kupandwa na hisia za awali nimkosee mume wangu. Nishauri.

Kupitia SMS

Kama kweli mlipendana jinsi unavyoelezea, ninaamini kuwa mwanamume huyo bado ana hisia kwako na ukimpa nafasi mkutane hata wewe zitakupanda na huenda ukamkosea heshima mume wako na ndoa yenu. Mwambie wazi kuwa wewe sasa ni mke wa mtu na huoni sababu yenu kukutana.

 

Mfanyakazi niliyemuajiri ananirushia ndoano

Kwako shangazi. Nimeoa na mimi na mke wangu tunafanya biashara ya kuuza nguo. Tumeajiri wanawake wawili na mmoja wao ananitaka kimapenzi. Ukweli ni kuwa ni mrembo sana kiasi cha kunasa moyo wangu lakini sitaki kusaliti ndoa yangu. Juzi alikuja afisini mwangu akaniambia ni lazima tutakuwa wapenzi hata ikichukua miaka mingapi. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ushauri wangu ni kuwa ufanye juu chini kumuepuka mwanamke huyo la sivyo atavuruga ndoa yako. Njia pekee ni kumfuta kazi. Wewe ni bosi wake na sielewi ametoa wapi ujasiri wa kukufuata afisini mwako kutangaza penzi lake kwako. Ukimpa nafasi atampiga hata mke wako.

 

Anataka nimzalie na hata hatujaenda kwao wala kwetu

Shikamoo shangazi! Natumai wewe ni mzima na nimekuja kwako unipe ushauri. Kuna mwanamume ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka miwili sasa na amekuwa akiniambia atanioa. Pili, anataka nimzalie mtoto na nimekataa kwa sababu hata sijui kwao wala hajanitambulisha kwa jamaa zake. Nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Kabla ya watu kuoana ni lazima kwanza wafahamiane vyema wao wenyewe, wazazi wao na jamaa zao wengine. Kwa sababu hiyo, si haki wala haifai kwa mwenzako kutaka umzalie ilhali wazazi wenu hawana habari kuhusu uhusiano wenu. Iwapo anatamani sana kuwa na familia, mwambie afuate utaratibu unaofaa.

 

Nataka kusubiri amalize masomo

Nimependana na msichana mwanafunzi wa shule ya upili. Niko tayari kusubiri amalize masomo kisha nimuoe. Naona ni heri umuache kwanza amalize masomo ndipo uwafahamishe watu wenu kuhusu mipango yako ya kumuoa.