Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nilienda ng’ambo kurudi nikapata amesonga

March 28th, 2018 2 min read

Na SHANGAZI SIZARINA

Vipi shangazi. Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 21 na nimekuwa na uhusiano na mwanamume fulani kwa miaka saba. Miaka miwili iliyopita nilipata safari ya ghafla ya kwenda ng’ambo kwa miaka miwili. Mpenzi wangu alinihakikishia kuwa angekuwa mwaminifu kwangu kwa muda ambao sikuwepo. Nilishangaa sana niliporudi majuzi nikapata ashapendana na msichana mwingine na tayari wamezaa pamoja. Sasa anadai eti bado ananipenda. Nishauri.
Kupitia SMS

Ni ajabu kwamba bado unahitaji ushauri kuhusu mwanamume kama huyo ilhali umehakikisha kwamba hana msimamo na hawezi kuwa mwaminifu kwako. Ukisafiri alikuhakikishia kuwa atakuwa mwaminifu kwako. Muda si mrefu akamhadaa msichana wa wenyewe kuwa anampenda akampa mimba. Sasa anataka kumuacha arudi kwako. Utamruhusu aendelee na karata yake hiyo? Utaamua mwenyewe!

 

Alinitema bila sababu,sasa anitaka
Vipi shangazi? Nilikuwa na uhusiano na mwanamume fulani na nilimpenda kwa moyo wangu wote. Lakini siku moja mwaka uliopita alinipigia simu akaniambia tuachane tu bila sababu yoyote. Nilikubali uamuzi wake wala sikumuuliza hata swali moja. Sasa ameanza kunitafuta kwa simu nafikiri anataka turudiane na mimi sitaki hata kumuona. Nishauri.
Kupitia SMS

Ninaunga mkono kwa dhati msimamo wako kuhusu mwanaume huyo. Ni dharau na ujeuri mkubwa kwa mtu anayedai kumpenda mwenzake kuamka siku moja na kukatiza uhusiano bila sababu. Inaonekana amegundua hawezi kupata mwingine kama wewe na ndiyo maana ameanza kukutafuta. Muondoe kabisa katika mawazo yako kwa kubadilisha nambari yako ya ama kufunga simu zake.

 

Alinichukia alipopata mimba yangu
Kwako shangazi. Kuna msichana tuliyependana sana na nilikuwa nimepanga kumuoa. Lakini alipopata mimba yangu alinichukia hata akanifungia kumpigia simu. Nampenda sana na sijui nitafanya nini. Nishauri.
Kupitia SMS

Kitendo cha msichana huyo ni ishara kwamba hakuwa ameamua moyoni mwake kwamba utakuwa mumewe. Hiyo ndiyo sababu alitoweka maishani mwako licha ya wewe kumhakikishia kuwa utamuoa na pia kupata mimba yako. Haina maana uendelee kuhangaisha moyo wako kuhusu mtu ambaye hana shughuli nawe na ameamua kuishi bila wewe.

 

Aliniahidi kunipeleka kwao, miaka minne sasa imeisha
Shangazi nilipata mpenzi na kwa bahati nzuri au mbaya nikapata mimba yake. Aliahidi kunipeleka kwao akanitambulishe kwa wazazi wake kisha anioe lakini huu sasa ni mwaka wa nne na bado hajatimiza ahadi yake hiyo. Amekuwa akiniambia nisubiri tu hadi umefika wakati nahisi kuwa ananichezea akili. Lakini pia nampenda sana sidhani ninaweza kumuacha. Nishauri.
Kupitia SMS

Ni hali ya kusikitisha sana kwamba baadhi yetu sisi wanawake huzuzuliwa na mapenzi tukawa hatuoni, hatusikii wala hatufikirii. Ni ajabu sana kuwa mpenzi wako huyo amekuhadaa kwa miaka minne kuwa atakuoa na bado unaendelea kusubiri ilhali tayari una mtoto wake. Na kama kwamba hayo si kitu si chochote, unasema huwezi kumuacha! Mimi sitasema zaidi, endelea kuubiri.

 

Rafiki ameniambia mpenzi wangu anamtongoza
Shikamoo shangazi. Nimegundua kuwa mwanamume mpenzi wangu amekuwa akimuandama msichana rafiki akitaka wawe na uhusiano wa pembeni. Rafiki yangu ameamua kuniambia kwa sababu hawezi kunisaliti kwa njia hiyo tena amemchukia sana mwanamume huyo kwa tabia yake hiyo. Nifanye nini?
Kupitia SMS

Bila shaka sasa umejua kuwa mpenzi wako huyo si mwaminifu kwako na mkiendelea na uhusiano huo hatimaye atakucheza tu. Ni bahati nzuri kwamba amemjaribu rafiki yako ndipo ukajua tabia yake hiyo. Ushauri wangu ni kwamba umkabili ukiwa pamoja na rafiki yako umzome kisha umteme.