Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nilijaribu kumuomba asali sasa hata simu hapokei!

October 3rd, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nilikuwa na mpenzi na tulikuwa tumekubaliana kuwa tutaoana. Siku moja nilimuomba asali lakini akakataa akisema kuwa imani yake haimruhusu kushiriki mapenzi kabla ya ndoa. Nilikuwa namjaribu tu kwani mimi pia ninajua ni makosa na nilimwambia hivyo. Ajabu ni kuwa tangu siku hiyo alikatiza kabisa mawasiliano, nikimpigia simu ama kumtumia SMS hajibu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kuna mambo ambayo hayafai kuingizwa mzaha na hilo ni mojawapo. Kama kweli unajua ni makosa kushiriki mapenzi kabla ya ndoa, kwa nini ulipendekeza kwa mpenzi wako? Ninahisi kuwa ulikuwa na nia hiyo lakini ukaibadili baada ya mpenzi wako kukataa ombi lako. Hatua yake ya kukatiza mawasiliano ni ishara kuwa hakuamini maelezo yako. Ukiweza mtafute akuelezee uamuzi wake.

 

Hunipa vidonge kila tunapoamua kushiriki mapenzi

Vipi shangazi? Nina mchumba na ameniahidi kuwa tutafunga ndoa hivi karibuni. Lakini kuna jambo moja linalonishangaza kuhusu mwenzangu. Amekuwa akiniletea dawa za kumeza kila tunapoamua kula vya chumbani. Je, hayo ni mapenzi gani?

Kupitia SMS

Amini usiamini, hayo hasa ndiyo mapenzi. Nyinyi ni wapenzi tu na sidhani mnataka kupata watoto kabla hamjaoana. Ninaamini kwamba dawa anazokuletea mpenzi wako ni za kukinga mimba. Kama hujawahi kumuuliza, ni muhimu ufanye hivyo ili uthibitishe. Ukigundua kuwa dawa hizo ni za kuzuia mimba, basi ujue mwenzako anakupenda. Hata mjitwike mzigo ambao hamuwezi kubeba kwa sasa.

 

Nateseka moyoni hisia zangu zimekita kwake lakini haamini

Shikamoo shangazi! Nilimdokezea hisia zangu msichana ambaye nampenda lakini akaniambia niache kujisumbua kwa sababu haiwezekani. Juzi nilimtuma rafiki yake amwambie jinsi ninavyoteseka moyoni kwa ajili yake akamwambia niende kwake mimi mwenyewe nimwambie. Nishauri.

Kupitia SMS

Uhusiano wa kimapenzi huanzishwa na kudumishwa kupitia maelewano, hauwezi kulazimishwa. Iwapo msichana huyo alikwambia wazi kwamba hakutaki, sidhani amebadili msimamo wake huo baada ya kutumana kwake. Hata hivyo, haitakuwa vibaya kujaribu tena kwani atafutaye hachoki. Rudi kwake uone iwapo ana jipya la kukwambia.

 

Nashangaa kwa nini hapokei simu zangu na nilimueleza kuwa nampenda sana

Shikamoo shangazi! Kuna mrembo niliyekutana naye majuzi na akapendeza moyo wangu. Nilimwelezea na akanipatia nambari yake ya simu ili tuendeleze mazungumzo. Jambo la kushangaza ni kuwa amekataa kabisa kujibu simu zangu. Nikimpigia na simu ya mtu mwingine anajibu na akijua ni mimi anakata. Ni kwa nini?

Kupitia SMS

Ninaamini unajua maana ya kitendo cha mwanamke huyp ila tu hutaki kukubali. Ukweli ni kwamba hakutaki na ndiyo maana amepuuza simu zako. Unasema pia ukimpigia kwa kutumia namba nyingine akisikia sauti yako anakata. Unahitaji ushahidi gani zaidi ya huo kujua kuwa mwanamke huyo hana haja na wewe? Achana naye utafute mwingine.

 

Aliniwacha akaolewa kwingine lakini mie nimeshindwa kabisa kumtoa akilini

Hujambo shangazi? Mwanamke aliyekuwa mpenzi wangu aliniacha akaolewa na mwanamume mwingine nilipomwambia kuwa sikuwa tayari kumuoa. Nilitaka anipe muda zaidi lakini akakataa. Nampenda sana na nimeshindwa kumtoa katika moyo na mawazo yangu. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Hatua ya mpenzi wako ilitokana na hali kwamba mlitofautiana katika mipango ya maisha yenu. Alifanya uamuzi wake huo kwa sababu aliamini kuwa wakati wake wa kuolewa ulikuwa umewadia nawe hukuwa tayari na hakutaka kungojea. Huwezi kumlaumu kwa sababu alikupatia nafasi ya kuwa mume wake lakini hukuwa tayari. Ingawa unasema unampenda, ni lazima ukubali kuwa yeye sasa ni mke wa mtu.