Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nilikawia kumwambia nampenda, sasa katwaliwa

July 25th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Kuna mwanamume ambaye amekuwa akinitaka na mimi pia nampenda sana. Nimekuwa nikiona vigumu kuungama penzi langu kwake lakini nilipanga kumwambia hivi karibuni. Juzi nilishtuka nilipokutana naye akiwa na msichana mwingine na baadaye nilipomuulizia nikaniambia ni mpenzi wake. Habari hizo zimeniacha hoi, sijui nitafanya nini. Nishauri.

Kupitia SMS

Bila shaka umejitakia mwenyewe masaibu hayo kwa kuchelewa kufuata moyo wako na kumkubali mara moja mwanamume huyo wakati unajua unampenda. Sasa amepata mwingine na itabidi umsahau.

 

Nimenyakua mpenzi wa rafiki yangu

Nina umri wa miaka 22 na bado sijapata mpenzi. Hata hivyo, nina uhusiano wa pembeni na kijana mpenzi wa msichana rafiki yangu mkubwa. Tatizo ni kuwa ana mazoea na kumpigia simu rafiki yangu huyo hata tukiwa pamoja. Kitendo chake hicho hunitia wivu na kunifanya nihisi kuwa hanitambui. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Nashangaa kwamba unamuonea wivu rafiki yako kwa kupendwa na mpenzi wake ambaye umenyakua. Kitendo cha kijana huyo kumpigia simu rafiki yako mkiwa pamoja ni thibitisho kuwa huyo ndiye mpenzi wake halisi, wewe ni mpango wa kando tu. Jinsi pekee na kuepuka hali hiyo ni kutafuta wako.

 

Nataka asali tu!

Kwako shangazi. Natumai kwamba wewe ni mzima. Nina jambo ambalo linahitaji ushauri wako. Kuna msichana ambaye nampenda sana na nimeamua kuonja asali. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Sijui ni kwa nini unaomba ushauri wangu ilhali unasema tayari umeamua. Isitoshe, asali unayosema unataka kulamba ina mwenyewe na utaweza kuipata kupitia kwake iwapo utamwelezea na aridhike kwamba unastahili.

 

Nampenda lakini rafiki amenionya niachane naye

Vipi shangazi? Kuna mwanamume tunayeishi mtaa mmoja ambaye anataka tuwe wapenzi na nina hisia kwake. Tumejuana majuzi tu kwa hivyo simfahamu vyema. Hata hivyo, mwanamke rafiki yangu amenionya akisema tabia ya mwanamume huyo ni kuwatumia wanawake kisha kuwatema. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni vyema kwamba umetafuta ushauri kutoka kwa rafiki yako. Hata hivyo, wakati mwingine marafiki wanaweza kukupotosha kwa sababu zao binafsi. Ushauri wangu ni kuwa ujipe muda wa kutosha ujuane na watu zaidi wanaomfahamu mawanaume huyo ili pia wakupe habari kumhusu ndipo uweze kufanya uamuzi wa busara.

 

Ananipa kila kitu lakini simpendi

Nina umri wa miaka 25 na bado sijapata mpenzi. Kuna mwanamume rafiki yangu wa miaka mingi ambaye ananipenda sana na amekuwa akinipa kila kitu ninachotaka. Lakini nahisi siko tayari kwake ingawa siwezi kuelezea sababu. Nishauri.

Kupitia SMS

Una bahati sana kupata mtu ambaye unajua kwa hakika kwamba anakupenda kwa dhati. Kuna wengi wanaotamani kupata kama huyo na nakuonya kuwa ukichelewa atanyakwa na mwingine uachwe ukijuta.

 

Hataki nifanye kazi, ahofia nitanyakuliwa

Nimeolewa na nina watoto wawili. Tatizo ni kuwa mume wangu amenikataza kufanya kazi na pia biashara kwa hofu kwamba nitanyakuliwa na wanaume wengine. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Maisha tunayoishi leo yanahitaji watu kusaidiana. Mume wako anafaa kujua kuwa hao wanaume ambao anahofia watakunyakua hawapatikani mahali kwa kazi tu bali hata mtaani mnakoishi. Kama ameamua iwe hivyo kubali tu bora atimizie mahitaji yote ya nyumbani.

 

Msichana anataka tuwe marafiki ila nataka penzi lake

Kuna msichana ninayemtaka kimapenzi lakini anasisitiza tuwe marafiki tu. Mimi sitaki urafiki, haja yangu ni mapenzi. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Uhusiano wa kimapenzi unatokana na maelewano kati ya wawili. Kama unayempenda hana hisia kwako, huwezi kumlazimisha. Pili, mara nyingi uhusiano hutokana na urafiki. Huenda mwenzako anataka muwe marafiki kwanza, akujue vizuri ndipo ajue kama unafaa kuwa mpenzi wake.