Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nilikuta kidosho kwake, akaniambia ni dadake

October 11th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nina umri wa miaka 22 na nimekuwa na mpenzi kwa mwaka mmoja sasa. Juzi nilimtembelea nyumbani kwake na nikampata na msichana mwingine. Nilipomuuliza aliniambia eti ni dada yake. Nilitaka kuzungumza na msichana huyo ili nimjue zaidi lakini aliondoka ghafla huku akionekana kuwa na wasiwasi. Ninashuku sana iwapo kweli huyo ni dada yake, labda ana mwingine. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kitendo cha msichana huyo cha kuondoka ghafla baada ya wewe kufika kinatia shaka. Kama kweli angekuwa dada ya mpenzi wako, yeye pia angetaka sana mjuane. Kuna uwezekano mkubwa kwamba ana uhusiano na mpenzi wako na ndiyo maana aliondoka ghafla kwa hofu kwamba ugegundua na kuzua ugomvi. Ushauri wangu ni kuwa usimuonyeshe wala kumuuliza tena mpenzi wako kuhusu uhusiano wao. Badala yake, endelea kuchunguza mienendo yao. Kama kweli ni wapenzi, hatimaye utawafumania kisha utajua hatua ya kuchukua.

 

Nipo kwenye utandu wa mapenzi na wanawake watatu

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 23 na nina wapenzi watatu. Mmoja ni mwanafunzi wa chuo kikuu na ndiye ninayempenda zaidi. Mwingine anafanya kazi lakini simpendi ingawa yeye ananipenda hata huwa ananiletea asali nyumbani. Yule wa tatu ni mtoto wa bosi wangu na simpendi ingawa ana pesa nyingi. Tatizo ni kwamba anatishia kuwa nisipomuoa atanifanya nifutwe kazi. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Naona umejifanya hodari wa mapenzi kwa kuwachanganya wasichana wa wenyewe ukijua kwa hakika kwamba huwapendi. Kama huna habari, ningependa ufahamu kwamba mapenzi yana kanuni zake na usipozifuata yanaweza kukugeuka. Kumbuka kwamba njia ya muongo ni fupi na ujanja wako huo hautaenda mbali. Muda si mrefu watagundua mchezo wako na utakuwa mashakani. Tayari mmoja wao ametishia kazi yako na itabidi usalimu amri ama ufutwe. Sina namna ya kukusaidia. Umejiingiza mwenyewe katika hali hiyo na ni wewe tu utajua namna ya kujitoa.

 

Nahisi hanipendi kwa jinsi alivyokatalia asali akijua naitaka sana

Shikamoo shangazi! Nimekuwa katika uhusiano wa kimapenzi kwa miaka mitatu sasa. Kwa muda wote huo, mpenzi wangu amekataa ombi langu la kutaka tuonje asali na hali hiyo inanifanya nihisi kuwa hanipendi kwa sababu hajali hali yangu. Nishauri.

Kupitia SMS

Iwapo unaamini kwamba ni lazima uonje asali ndipo uamini kuwa mwenzako anakupenda, basi inaonekana huelewi maana hasa ya mapenzi. Huna haki kabisa ya kupata huduma kutoka kwa mpenzi wako hadi utakapomuoa. Ninaamini amekupatia sababu yake ya kutotaka kushiriki jambo hilo kwa sasa. Kama kweli unampenda, heshimu uamuzi wake.

 

Ananitaka ingawa marehemu dadake alikuwa mpenzi wangu

Vipi shangazi? Nilikuwa na mpenzi lakini aliaga dunia mwaka uliopita kupitia kwa ajali ya barabarani. Dada yake ambaye walikuwa wakinitembelea kwangu pamoja amekuwa akinipigia simu mara kwa mara na pia kuja nyumbani kwangu. Kuna kila dalili kwamba ananitaka. Sijui kama itakuwa sawa kuwa na uhusiano naye ilhali dada yake alikuwa mpenzi wangu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ninaelewa utata ulio nao kuhusu jambo hilo. Kwa maoni yangu, sidhani kuna ubaya wowote wa kuwa na uhusiano na dada ya marahemu mpenzi wako. Ingekuwa makosa kama angekuwa hai kisha ushikane na dada yake labda baada ya nyinyi kukosana. Ukweli ni kuwa hayupo tena na hatawahi kuwepo. Kama dada yake ameamua kuendeleza uhusiano huo kupitia kwake, hiyo ni sawa.

 

Alioa bila kuniambia

Kuna kijana tuliyependana sana kwa miaka miwili lakini hatimaye akaoa mwanamke mwingine bila hata kuniambia. Sasa hata sioni haja ya kuingia kwa uhusiano tena.

Kupitia SMS

Naelewa unavyohisi. Hata hivyo, ni haki ya mtu kuchagua anayetaka kuishi naye kama mume ama mke. Pili, uhusiano wa kimapenzi si kibali cha ndoa kwani mahusiano huvunjika. Kama huna habari, ni watu wachache sana wanaopata wake au waume kupitia uhusiano wa kwanza. Jipe moyo na uwe tayari kupenda tena.