Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nilimfumania na dume, nitampendaje kama awali?

May 24th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HABARI zako shangazi? Mimi nina mpenzi niliyempenda kwa moyo wangu wote hadi siku aliyonisaliti. Nilimfumania na mwanamume mwingine na akaniomba msamaha. Nilimsamehe lakini kila nikikumbuka ninaumwa sana moyoni na kumchukia kwa kitendo chake hicho. Nitafanya nini ili nimpende kama awali?

Kupitia SMS

Majeraha kutokana na usaliti wa kimapenzi huchukua muda kupona. Kwa sababu ulikubali kumsamehe mpenzi wako, ondoa chuki moyoni na ujipe muda wa kutosha na hatimaye mapenzi ya awali kati yenu yatarejea.

 

Sitaki mtu kwa sasa

Vipi shangazi? Mimi sina mpenzi na sitaki yeyote kwa sasa. Hata hivyo, wanaume wanaonitaka nikiwakataa huniambia eti nina maringo. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hivyo ndivyo walivyo wanaume. Kwao hakuna mwanamke anayewakataa kwa sababu nzuri, isipokuwa tu maringo. Wapuuze tu kwani madai yao ni sawa tu na maji moto yasiyoweza kuteketeza nyumba.

Nililazimishiwa penzi

Vipi shangazi? Kuna msichana tunayeishi pamoja kama mume na mke. Ananipenda sana lakini mimi simpendi bali nililazimishwa na wazazi wake walipojua kuhusu uhusiano wetu. Nishauri.

Kupitia SMS

Unajikosea wewe binafsi na mwenzako pia kwa kuishi katika ndoa ya lazima. Ungemwambia ukweli yeye na wazazi wake na hata sasa unaweza kuwaambia kuwa humpendi na huwezi kuishi naye kama mke wako. Usipochukua hatua hiyo utaendelea kuishi kwa majuto na majonzi.

Naona hajabadilika

Niliolewa kwa miaka mitatu lakini nikaachana na mume wangu kwa kuwa na wanawake wengine nje. Isitoshe, hakuwa akigharamia mahitaji ya nyumbani. Alinifuata kwetu baada ya mwaka mmoja lakini naona bado hajabadilika. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Nimesema katika ukumbi huu mara nyingi kuwa ni heri mtu kuishi peke yake kuliko kuishi katika ndoa yenye mateso. Umempa mume wako nafasi ya pili na kama hajabadilika una haki ya kutoka katika ndoa hiyo ukiamua kufanya hivyo.

Mume haniamini

Nina umri wa miaka 28, nimeolewa na nina watoto wawili. Mume wangu naye ana umri wa miaka 45. Shida yake ni kuwa haniamini na amekuwa akidai eti ninaleta wanaume wengine nyumbani wakati hayupo. Mimi ninampenda kwa dhati na siwezi kufanya mambo kama hayo. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ninaamini wasiwasi wake unatokana na tofauti yenu ya umri kwani amekuwa mzee na labda ameanza kulemewa na shughuli za chumbani na anahofia huenda ukaanza kutafuta nje. Itabidi uwe ukimhakikishia mara kwa mara kuwa wewe ni mwaminifu kwake na pia dini yako imekufunga kufanya mambo kama hayo.

Bado namtamani sana lakini hataki mambo yangu

Shikamoo shangazi! Kuna mwanamume tuliyekuwa wapenzi lakini tukaachana na kila mmoja wetu akapata mwingine. Shida ni kuwa kila nikimuona ninapandwa na hisia za kimapenzi mpaka nahisi kumuacha niliye naye. Nampenda sana lakini naye hataki kuongea nami. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni wazi kuwa ulipuuza hisia zako kwa mwanaume huyo ukakubali muachane na sasa unajuta kwa sababu moyo wako bado uko kwake. Hata hivyo, maji tayari yalimwagika kwa sababu ana mwingine nawe pia una wako. Itabidi ukubali ukweli huo na ujaribu uwezavyo kuepuka kukutana naye kama unataka kumsahau.

Nimegundua anatoka familia iliyolaaniwa

Kwako shangazi. Nina mpenzi lakini ninajuta kuwa naye kwani nimegundua ametoka familia ya watu wa ukoo ambao umelaaniwa. Nishauri.

Kupitia SMS

Sijui umetoa wapi habari kuwa familia yao ni ya ukoo uliolaaniwa na iwapo umethibitisha hilo. Hata hivyo, iwapo unaamini na unahisi huwezi kuendelea naye, mwambie ili muachane mapema.