Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nilimfumania peupe na sasa ataka nimsamehe

March 9th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mrembo fulani kwa miaka miwili lakini nimegundua kuwa amekuwa akinichezea na kijana mwingine rafiki yangu. Juzi niliwafumania peupe nyumbani kwa kijana huyo. Baadaye mpenzi wangu alinipigia simu kuniomba msamaha akiniambia ilikuwa mara ya kwanza na hatawahi kurudia. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Inawezekana kuwa mpenzi wako aliteleza tu akatumbukia kwenye mtego wa kijana huyo siku uliyowafumania. Kama ndivyo, ni lazima alishtuka sana, anajuta na hatawahi kurudia. Inawezekana pia hayo ni mazoea yake na hakuwa na budi ila kuapa kuacha ili kujitoa katika hali hiyo., kisha aendeleze tabia yake hiyo kwa uangalifu zaidi. Ni juu yako uendelee kumchunguza kwa makini sana ili ujue iwapo ameacha au la. Kama hajaacha bila shaka utaona dalili.

 

Nimependana na dada ya mpenzi wangu wa kwanza

Shikamoo shangazi! Kuna msichana niliyemdokezea penzi langu tukiwa wanafunzi wa shule ya upili. Alikubali na akaniahidi kuwa atakuwa mke wangu tukimaliza masomo. Ajabu ni kuwa tulipomaliza shule alishikana na mwanamume mwingine. Sasa nimependana na dada yake mkubwa na ninapanga kumuoa. Je, kuna makosa?

Kupitia SMS

Sioni makosa yoyote katika hatua yako hiyo. Msichana aliyekuacha alikuwa mpenzi wako tu, hakuwa mke wako. Isitoshe, ndiye aliyevunja uhusiano wenu kwa hivyo hawezi kukulaumu. Kama umempenda dada yake na umeamua kumuoa, endelea na mipango yako.

 

Anadai kupakuliwa miezi miwili pekee baada ya kujuana

Vipi shangazi? Nilikutana na mwanamume fulani miezi miwili iliyopita na tukapendana. Nilidhani ananipenda kwa dhati lakini nimeanza kumshuku kwani hatujafahamiana vizuri na tayari ameanza kudai asali. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Ni muhimu sana kuwa na tahadhari kwa wanaotaka uhusiano kwa sababu baadhi yao huwa na nia mbaya. Huyo anayedai asali ilhali mmejuana kwa miezi miwili pekee anaweza kuwa tapeli wa kimapenzi ambaye nia yake ni kukutumia kisha atoweke. Usikubali ombi lake, endelea kumpima hadi utakapojua lengo lake kwako. Kama nia yake ni hiyo asali, ukiendelea kumkazia atajiondoa mwenyewe akaitafute kwingine.

 

Napanga kumuacha kwani hanitimizii mahitaji yangu

Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 28 na nimekuwa na uhusiano na mwanamume mwenye umri wa miaka 42 ambaye ameoa. Tulijuana nikiwa na mtoto kutokana na uhusiano wa awali na anampenda tu kama mtoto wake. Tatizo pekee ni kuwa hanitimizii mahitaji yangu. Sasa kuna kijana anayenipenda na yuko tayari kunioa pamoja na mtoto wangu. Waonaje?

Kupitia SMS

Uhusiano kati ya mwanamke na mwanamume aliye na mke ni haramu na una changamoto zake. Ni bahati kubwa kwako kumpata mwanamume aliye tayari kukuoa na ninashangaa eti unahitaji ushauri wangu. Msahau mume wa mwenyewe na umchukue haraka huyo aliye tayari kukuoa kabla hajabadili nia yake.

 

Niko na uhusiano na mwanafunzi wa shule ya sekondari

Shikamoo shangazi! Nina uhusiano na msichana mwanafunzi wa shule ya upili. Juzi tulipokuwa tukiongea kwa simu nilimsikia mama yake akimfokea kisha simu ikakatika. Tangu siku hiyo simu yake imezimwa, nimempigia mara nyingi bila kufaulu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ilivyo ni kwamba mama yake aliyasikia mliyokuwa mkiongea na akajua kuwa binti yake yuko katika uhusiano wa kimapenzi. Kumbuka kuwa huyo unayemuita mpenzi wako ni mwanafunzi na mama yake hatakubali mapenzi yavuruge masomo yake. Hali kwamba hapatikani tena kwa simu ni ishara kuwa alipokonywa simu hiyo ili kukatiza mawasiliano kati yenu. Achana na mtoto wa wenyewe asome.