Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nilimnyima asali uhusiano wetu ukaingia baridi

September 18th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 28 na nilikuwa nimeolewa lakini tukaachana na mume wangu nikiwa na mtoto mmoja. Nimependana na mwanamume mwingine lakini nimekataa kushiriki mahaba naye kwa hofu kuwa ataniacha. Msimamo wangu huo umeingiza baridi katika uhusiano wetu na nina wasiwasi kuwa anaweza kuniacha. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Hujaelezea ni kwa nini unafikiria kuwa ukimpa mahaba atakuacha ilhali unasema mnapendana. Jambo muhimu la kufanya ni kujua anataka nini kwako hasa. Kama anatafuta mke ni muhimu ujue. Ukiona kwamba nia yake ni kukutumia ni heri ujiondoe mapema kwani akitimiza lengo lake hutamuona tena.

 

Bado anawasiliana na mpenzi wa awali

Shikamoo shangazi! Nina mwanamke mchumba wangu ambaye nampenda sana. Lakini nimeshangaa kugundua kwamba bado huwa anawasiliana kwa simu na mpenzi wake wa awali. Ninajua ananipenda kwa dhati lakini pia nina wasiwasi kwani sijui huwa wanazungumzia nini. Nishauri.

Kupitia SMS

Mapenzi na urafiki ni mambo mawili tofauti. Inawezekana waliachana kama wapenzi lakini bado ni marafiki. Hata hivyo, una sababu ya kuwa na wasiwasi ikizingatiwa kuwa walikuwa wapenzi. Itakuwa vyema umuulize kinachoendelea kati yao ili kuondoa wasiwasi.

 

Nimempa mimba mwanafunzi, hofu ni sijui ni hatua gani nitakayochukuliwa

Shangazi nahitaji ushauri wako. Nimekuwa na uhusiano na msichana mwenye umri wa miaka 19, mwanafunzi wa shule ya upili. Kwa bahati mbaya nimempa mimba na sasa anatishia kuwaambia wazazi wake. Uamuzi wake huo unanipa tumbojoto kwa sababu sijui wazazi wake wakijua watachukua hatua gani. Nishauri.

Kupitia SMS

Iwapo huna habari, ni muhimu ujue kwamba kila kitendo kina matokeo yake na mhusika ni lazime awe tayari kuwajibika kwa matokeo yoyote yale. Ni wewe mwenyewe uliyemwambia msichana wa wenyewe kwamba unampenda kisha ukamshawishi mshiriki mapenzi. Mimba anayobeba ni mzigo wako ambao huwezi kuepuka. Kuwa tayari kwa uamuzi wowote ambao wazazi wake watafanya kuhusu suala hilo.

 

Alinitupa baada ya kunipachika mimba, eti sasa anataka turudiane anioe

Shikamoo shangazi! Mwanamume niliyempenda sana aliniacha baada ya kunipa mimba. Hatimaye nilipata mtoto ambaye sasa ana umri wa miaka minne. Nilishangaa juzi aliponipigia simu akisema bado ananipenda na kwamba yuko tayari turudiane kisha anioe. Bado ninampenda lakini sidhani ninaweza kumwamini kwa sababu aliniacha wakati nilipomhitaji sana. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Sidhani kuwa mwanamume huyo anakupenda kwa dhati na kwamba yuko tayari kuishi nawe kama mtu na mkewe. Sababu ni kuwa alikuacha alipojua una mimba yake na akaishi kwa miaka kadhaa bila kukujulia hali. Sasa amejitokeza ghafla na anataka mrudiane ilhali hujui amekuwa wapi kwa muda wote huo. Ningekuwa wewe ningeachana naye niendelee na maisha yangu.

 

Nimekutana na wa awali penzi likanoga, nahofia huenda ndoa yangu ikaathirika

Hujambo shangazi? Nimeoa kwa miaka miwili sasa. Hata hivyo, mwaka uliopita nilikutana na mwanamke aliyekuwa mpenzi wangu tukiwa shuleni na tumefufua uhusiano wetu. Kusema kweli penzi lake limenizuzua na nimeishia kumpenda hata kuliko mke wangu. Nahofia hali ikiendelea hivyo nitaharibu ndoa yangu na sijui nitafanya nini ili kumuepuka. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Penzi haramu ni tamu lakini athari zake ni kali kama pilipili. Mtu akioa au kuolewa huwa ameamua kuachana na wengine wote na kutulia katika ndoa. Uhusiano huo unaosema umekunasa kiasi cha kuharibu ndoa yako umeutafuta mwenyewe na ni wewe tu unayefaa kuuvunja la sivyo utavunja ndoa yako. Hali itakuwa mbaya zaidi mke wako akigundua kuwa unamchezea.