Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nilimpendea sauti tu sasa natamani kumuona

July 17th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHANGAZI ninatumai hujambo. Tafadhali nahitaji ushauri wako. Kuna mwanamke tuliyejuana mwaka jana kupitia kwa simu aliponipigia kimakosa. Sauti yake ilinasa hisia zangu na tangu wakati huo tumekuwa tukiwasiliana. Natamani sana kumuona lakini shida ni kwamba minaishi mbali sana na anakoishi yeye. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Wewe ndiye unayemtaka mwanamke huyo kwa hivyo mipango yote kuhusu jinsi mtakavyokutana ni juu yako. Itabidi umweleze nia yako na mkikubaliana, umtumie nauli mkutane mahali ama wewe mwenyewe usafiri hadi anakoishi.

 

Mrembo wangu kanichoma mtima

Shikamoo shangazi! Nimekuwa na uhusiano na mrembo fulani kwa mwaka mmoja sasa na nampenda sana. Lakini juzi nilimpata na kijana mwingine. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Uamuzi wako kuhusu uhusiano wenu utategemea na uliwapata wakifanya nini. Kama uliwafumania wakipulizana mahaba, basi huna mpenzi tena bali huyo ni tapeli wa kimapenzi kwa hivyo itabidi umuepuke. Iwapo uliwapata wakizungumza, itakuwa makosa kwako kukata kauli kwamba mwenzako anakusaliti kimapenzi kwa sababu huna ushahidi.

 

Kuna kijana afanya moyo kudundadunda

Vipi shangazi? Mimi ni mrembo mwenye umri wa miaka 22. Sijawahi kuwa na mpenzi maishani na kuna kijana fulani ambaye amenasa moyo wangu. Nishauri.

Kupitia SMS

Tafuta namna ya kumdokezea hisia zako kwake hata kama ni kupitia kwa marafiki wako au wake. Huenda yeye pia ana hisia kwako na hajapata nafasi nzuri ya kukuelezea. Hata hivyo, mwendee taratibu. Usifumbwe macho na hisia za kimapenzi utumbukie mikononi mwa mtu asiyekupenda ambaye atakutumia kisha akuteme.

 

Mpenzi wangu ni mkware ajabu

Kwako shangazi. Nimependana na mwanamke aliyekuwa na mpenzi lakini wakaachana. Aliniambia mpenzi wake alikuwa na wivu sana na walikuwa wakigombana kila mara akimshuku kuwa na wanaume wengine. Sasa nimegundua kuwa hiyo hasa ndiyo tabia yake. Siku za hivi majuzi nilihisi kuwa penzi lake kwangu limepungua na nikaamua kumuuliza. Aliungama kuwa ana mwingine kisha akiniomba msamaha akisema ananipenda sana na kuapa kuwa ataacha tabia hiyo. Nimechanganyikiwa kabisa, sijui nitafanya nini. Tafadhali nisaidie.

Kupitia SMS

Sasa umejua sababu iliyomfanya mpenzi wake amuache na kwamba alikuhadaa kuwa alishukiwa bure. Inaonekana tabia yake hiyo imekuwa mazoea na haitakuwa rahisi kwako kumbadilisha. Tayari uhusiano wenu umeingia doa kwa sababu umejua kuwa si mwaminifu kwako. Sidhani ungetaka kumuoa mwanamke ambaye atakuwa kitoweo cha kila mwanamume mtaani. Ushauri wangu ni kuwa umuondokee mapema.

 

Baada ya miaka 3 ameniruka, nishauri

Vipi shangazi? Nimekuwa na mpenzi kwa miaka mitatu lakini sasa ameniruka. Sijui nitafanya nini. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Sijui unamaanisha nini ukisema kuwa amekuruka. Kama amekatiza uhusiano, huo ni uamuzi wake na bila shaka ana sababu na haki ya kufanya hivyo. Itabidi ukubali uamuzi wake na uendelee na maisha yako.

 

Ninaye wangu ila macho hayana pazia

Shikamoo shangazi! Nimekuwa na msichana mpenzi wangu ambaye ninampenda kwa dhati. Miezi mitatu iliyopita nilisafiri mjini kutafuta kazi na wiki mbili baadaye nimekutana na mwingine ambaye ni mrembo hata zaidi. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ni haki yako kuwa na mpenzi anayeridhisha moyo wako. Hata hivyo, ukizingatia urembo pekee utachanganyikiwa kwa sababu kila siku ukitembea mjini utakutana na wengi warembo hata zaidi. Ni muhimu uwe na msimamo la sivyo utaishi bila mke.