Habari Mseto

SHANGAZI AKUJIBU: Nilimuacha nilipomfumania akiwa na dadangu

December 28th, 2018 2 min read

Kwako shangazi. Nililikuwa nimeaolewa lakini nikamuacha mume wangu baada ya kumfumania ndani ya nyumbani yetu akiwa na dada yangu. Huu sasa ni mwaka wa pili akiniomba msamaha na kunishawishi nimrudie lakini sijapata nafasi moyoni mwangu ya kuweza kumsaheme kwa kitendo chake. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Siwezi kukulaumu kwa hatua uliyochukua ya kujiondoa katika ndoa hiyo. Mume wako alikosa adabu kwa kuanzisha uhusiano na dada yako na kama hiyo haikutosha wanaendesha mambo yao nyumbani kwako. Ingawa mafundisho ya kidini yanasema hakuna kosa lisilosamehewa, ninaelewa unavyohisi kwa kuwa wewe ni binadamu si malaika. Kama umeamua humtaki tena, mwambie hivyo na uendelee kushikilia msimamo wako.

Mwezi mmoja tu na anadai kupakuliwa

Shangazi nimejipata katika njiapanda na nakuomba unisaidie. Mwanamume ambaye tumejuana kwa mwezi mmoja pekee anataka tushiriki mahaba lakini nahisi itakuwa haraka sana. Tatizo ni kuwa nampenda sana na sitaki kumpoteza. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Mimi kamwe siamini kuwa tendo la ndoa ndilo thibitisho pekee kuwa mtu anampenda mwenzake. Mwezi mmoja ni muda mfupi sana na nashuku mwanaume huyo hakupendi kwa dhati na shabaha yake ni hiyo tu. Unaweza kumtimizia ombi lake kisha akuteme uachwe ukijuta. Mwambie wazi kuwa unahitaji muda zaidi kumjua. Kama kweli anakupenda atangojea.

Nimeshindwa kabisa kupata mchumba

Vipi shangazi? Tafadhali nakuomba unisaidie. Mimi nimeshindwa kabisa kupata mchumba na sina kasoro yoyote ya kimwili. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kutafuta mchumba si jambo rahisi na mtu anahitaji kuwa na subira. Endelea kutafuta kwani ninaamini kuna yule ambaye Mungu amekutengea na wakati ukifika utampata utulie.

Nimeambiwa yule nimpendaye ni mwanamke kahaba

Hujambo shangazi? Nilikutana na mwanamke fulani miezi miwili iliyopita akateka moyo wangu na nilipomdokezea akanikubali. Sasa nimesikia kutoka kwa watu kadhaa kuwa mwanamke huyo ni kahaba na nimechanganyikiwa. Nishauri.

Kupitia SMS

Ingawa huwezi kuamini mara moja uliyoambiwa kumhusu, ushauri wangu ni kuwa uchukulie uhusiano huo kwa tahadhari huku ukichunguza mienendo yake. Kama uliyoambiwa ni kweli utajua na ukithibitisha hutakuwa na budi kumwondokea.

Mume wa wenyewe amehepa baada ya kunipachika mimba

Shangazi kuna jambo linalonitatiza moyoni na ninaamini utanisaidia. Nina umri wa miaka 22 na nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mume wa mtu kwa karibu mwaka mmoja. Akinitaka huwa tunakutana. Kwa bahati mbaya, nimepata mimba na nilipomuelezea akaniambia nisiwe na hofu. Sasa huu ni mwezi wa tatu sijamuona, hakuna mawasiliano wala hanitumii pesa za matumizi kama awali. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hiyo ni mojawapo ya hatari zinazoambatana na mahusiano haramu. Naona wewe bado ni msichana mchanga na sielewi ni kwa nini uliamua kushikana na mume wa mwenyewe badala ya kutafuta wako. Isitoshe, umepuuza umuhimu wa kutumia kinga na kwa sababu hiyo umepata mimba. Hali kwamba mwanaume huyo ametoweka baada ya kujua una mimba yake ni thibitisho kuwa hayuko tayari kuwajibika. Bahati mbaya ni kwamba huwezi kumlazimisha kufanya hivyo hata kisheria kwa sababu uhusiano wenu umekuwa haramu. Itabidi ujitayarishe kulea mtoto huyo.

Tumempenda wawili

Shikamoo shangazi? Kuna kijana fulani ambaye nampenda kwa moyo wangu wote ingawa sisi ni marafiki tu. Sasa nimegundua kuna msichana mwingine ambaye pia anampenda. Nifanye nini?

Hilo sasa litategemea uamuzi wake mwenyewe. Kama mnampenda nyote wawili kuwa tayari kwa lolote kwani anaweza kukuchagua wewe ama huyo msichana mwingine.