Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Niliondoka tu dakika kadhaa akaoa mke mwingine!

May 25th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Nimeolewa na ninampenda sana mume wangu. Mwaka uliopita nilisafiri kwenda mashambani kuwajulia hali wazazi wangu. Tulikubaliana na mume wangu kuwa angekuja kunichukua baada ya wiki moja. Siku mbili baadaye alinipigia simu akaniambia ameoa mke mwingine. Tangu hapo amekatiza mawasiliano hata ameacha kugharamia mahitaji ya mtoto. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ni wazi kwamba mume wako aliamua kuchukua njia ya mkato kukutaliki. Ni jambo ambalo amekuwa akipanga na hatimaye amefaulu kwa sababu sasa uko kwa wazazi wako naye ameoa mke mwingine. Ingawa amekuacha, unaweza kumchukulia hatua za kisheria ili alazimishwe kugharamia malezi ya mtoto wenu.

 

Hataki kuniamini

Hujambo shangazi? Nina mpenzi ninayempenda kwa dhati. Ninaishi mbali naye na amekuwa akinishuku kuwa nina wanaume wengine. Nimemhakikishia kuwa ni yeye tu lakini hataki kuniamini. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Sijui mwenzako anataka umwambie nini tena kama umemhakikishia huna mwingine ni yeye tu na hataki kuelewa. Mwambie kama hakuamini ahamie unakoishi ili athibitishe mwenyewe.

 

Sitosheki na burudani hadi natafuta pembeni

Hujambo shangazi. Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 32 na sina mpenzi kwa sasa. Sababu ya kukosa mpenzi ni kuwa ninapenda sana burudani na kila ninapokuwa na uhusiano huwa siridhiki inabidi nitafute pembeni na nikigunduliwa ninatemwa. Je, nina kasoro?

Kupitia SMS

Siwezi kuita tabia yako hiyo kasoro kwa sababu watu wameumbwa kwa namna tofauti na labda hayo ndiyo maumbile yako. Hata hivyo ni tabia mbaya kuweka mbele mambo hayo katika uhusiano. Kuna tofauti kubwa kati ya mapenzi ya dhati na tamaa.

 

Alinitusi vibaya kisha akaanza kunitafuta

Shikamoo shangazi! Mwanaume ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka miwili tuligombana majuzi na akanitusi akisema mimi ni sura mbaya hata hajui amekuwa akitafuta nini kwangu. Nilimpenda kwa moyo wangu wote na matamshi yake hayo yaliniuma sana moyoni na nikaapa kuwa sitawahi kuongea naye tena maishani. Siku mbili baadaye nilishangaa aliponipigia simu kuomba msamaha eti matamshi yake yalitokana na hasira. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Mtu anaweza kusema chochote anapokuwa na hasira. Kama mwenyewe ndiye aliyeomba uhusiano huo na kuungama kuwa anakupenda haiwezekani kwamba umegeuka kuwa sura mbaya baada yenu kukosana. Isitoshe, amekuomba msamaha na kukwambia hayo yalitokana na hasira. Jaribu kumuelewa.

 

Mwanamume amekana kabisa kuwa ameoa

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 24 na kuna mwanamume tunayependana sana. Tulipokutana mara ya kwanza nilimuuliza iwapo ameoa akaniambia hajaoa. Hata hivyo, hivi majuzi mtu fulani aliniambia ameoa na nilipomuuliza tena akakana kabisa. Sasa nimechanganyikiwa, sijui ni nani anayesema ukweli. Nishauri.

Kupitia SMS

Kutokana na maelezo yako, mpenzi wako amekuambia mara mbili sasa kuwa hajaoa na unafaa kumwamini hadi utakapothibitisha habari za aliyekwambia kuwa ameoa. Jinsi pekee ya kujua ukweli ni kwenda kwao nyumbani na kuwauliza jamaa zake. Ikiwezekana, fanya hivyo.

 

Nimetendwa wacha tu!

Hujambo shangazi? Mwanamke ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka miwili alihama ghafla mtaani bila kuniambia. Mwanaume rafiki yangu pia amehama na nimechunguza nikagundua wameenda kuishi pamoja. Sikujua kuwa wamekuwa na uhusiano hata mwanamke huyo ana mimba ya mwanaume huyo! Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kutokana na maelezo yako, ni wazi mwanamke huyo amekuwa akikudanganya kuwa ni wako huku akimgawia asali rafiki yako. Hatua yake ya kushikana na rafiki yako huyo na kupata mimba yake ni ishara kamili kuwa amemchagua yeye na hana haja nawe. Huo ni uamuzi wake na huwezi kumlazimisha akurudie.