Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nilitarajia harusi baada ya miaka 3, sasa asema nisubiri

May 10th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Kuna mwanamume ambaye tumekuwa wachumba kwa miaka mitatu sasa. Alikuwa ameniahidi kuwa tunaoana baada ya muda huo lakini sasa amebadili nia na kuniomba nisubiri kidogo. Ananiambia kuna jambo aliloahidi kuwatimizia wazazi wake na linahitaji kiasi kikubwa cha pesa. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ninaamini kuwa mchumba wako ana sababu nzuri ya kuwatimizia wazazi wake jambo hilo kabla hajakuoa. Kama ni jambo linalohitaji pesa nyingi, bila shaka anahisi kuwa akioa atapata majukumu mengi ashindwe kutimiza ahadi yake kwa wazazi wake. Sioni sababu yako kuwa na wasiwasi bora tu ana nia ya kukuoa akimaliza mradi huo. Isitoshe, furaha ya wazazi wake ya kutimizwa kwa ahadi hiyo itakuwa baraka kwenu wawili.

 

Nashuku mume angali na uhusiano na aliyezaa naye

Hujambo shangazi? Nimeolewa na nina watoto wawili. Ninamjua mpenzi wa awali wa mume wangu ambaye walizaa mtoto pamoja kabla hajanioa. Nimegundua wamekuwa wakiwasiliana na mume wangu amejitetea eti huwa anataka kujua hali ya mtoto. Ninashuku bado wako pamoja. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni haki ya mume wako kumjulia hali mtoto wake na anaweza kufanya hiyo tu kupitia kwa mama yake. Hata hivyo, kuna hatari ya mwanamke huyo kutumia fursa hiyo kumshawishi mume wako waendeleze uhusiano wao kisiri. Ni muhimu umuonye mume wako dhidi ya jambo hilo kisha ufuatilie kwa karibu mienendo yao ili ujue iwapo kuna zaidi ya mtoto.

 

Nampenda sana ila ananipuuza, ama nina ubaya fulani?

Kwako shangazi. Kuna mwanamke ninayempenda kwa moyo wangu wote na nimejaribu juu chini kumshawishi tuwe wapenzi. Nimekuwa nikimpigia simu na kumtumia SMS kuhusu hisia zangu kwake lakini anapuuza. Sielewi ameona ubaya gani kwangu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Uamuzi wa mwanamke huyo wa kupuuza simu na SMS zako ndilo jibu lake kwako na tafsiri yake ni kwamba ingawa wewe unampenda yeye hana haja nawe. Kwa hivyo kuendelea kumsukumia SMS na kumpigia simu ni kumsumbua. Tafuta mapenzi kwingine.

 

Mke amekuwa kero, vya jikoni hanipi, vya chumbani nalipia!

Shangazi pokea salamu zangu za dhati. Nahitaji ushauri wako tafadhali. Nimeoa kwa miaka mitatu sasa lakini ndoa yangu imeingia matatizo. Kisa ni kwamba mke wangu amekuwa akininyima chakula na pia huduma za chumbani bila sababu. Wakati mwingine yeye hudai pesa kutoka kwangu ndipo nipate haki yangu ya ndoa.

Kupitia SMS

Iwapo huyo ni mke wako halali, ni wajibu wake kukushughulikia jikoni na chumbani pia. Kamwe huna sababu ya kumhonga ndipo upate huduma hizo. Hayo ni mambo muhimu katika ndoa na kama hawezi kukutimizia kama mke wako basi hiyo kamwe si ndoa ni heri muachane utafute mke.

 

Nimekuwa na 2, sasa moyo umechagua, sijui nimueleze nini ninayemtema

Kwako shangazi. Nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na wasichana wawili kwa mwaka mmoja sasa. Lakini nimeanza kupoteza hisia kwa mmoja wao na najihisi nampenda mwenzake zaidi. Naona vigumu kumwambia kwa sababu sitaki anione kama mtu mlaghai ambaye alikuwa na nia ya kumtumia. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Mapenzi ya dhati ni kati ya watu wawili pekee. Ingawa unajaribu kujiondolea lawama, ukweli ni kuwa umekuwa ukiwalaghai wasichana hao wawili ili kukidhi tamaa yako na sasa umeamua kuungama uhuni wako. Itabidi umwambie ukweli huyo ambaye huna hisia kwake. Lakini usimwambia kuwa umekuwa na mpenzi mwingine. Badala yake mwambie tu kuwa unahofia uhusiano wenu hautaenda mbali na ni heri kuuvunja mapema. Ninaamini ataelewa.