Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nimeacha mume wangu, mwalimu sasa anifuata

October 1st, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

NILIKUWA nimemuacha mume wangu alipoanza kunidhulumu. Nilirudi kwa wazazi wangu na wamejitolea kunigharimia masomo yangu ya chuo kikuu. Kuna mmoja wa walimu ambaye anataka tuwe wapenzi lakini nahofia uhusiano huo utaathiri vibaya masomo yangu ingawa pia nahitaji mume. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Nimekuwa nikishauri kwamba ni heri mtu kuishi bila mume au mke kuliko kuishi katika ndoa iliyo na dhuluma. Kama wazazi wako wamejitolea kugharimia masomo yako, zingatia zaidi hilo kwani ni kwa njia hiyo ambapo utaweza kujitegemea maishani. Ni vyema kuwa na mume lakini ni vyema zaidi kuwa na uwezo wa kuishi bila kumtegemea yeyote.

 

Bado napenda kijana aliyeniacha bila sababu, nashindwa kumsahau kabisa

Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 20 na kuna kijana ambaye nampenda tena sana. Tumekuwa wapenzi lakini tuliachana miezi miwili iliyopita aliponiambia kuwa ana mpezi mwingine kwa hivyo niachane na yeye. Tatizo ni kuwa hakuniambia sababu yake kuniacha. Nampenda sana na sijui nitafanya nini. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Hizo ni dalili za mtu ambaye ameamua kujiondoa katika uhusiano kwa vyovyote vile. Inaonekana hataki tena uhusiano nawe na ndiyo maana alikwambia wazi kuwa ana mwingine ingawa huenda hiyo si kweli. Ushauri wangu ni kwamba ukubali uamuzi wake tu huwezi kumlazimisha kuendelea na uhusiano huo ingawa unasema unampenda.

 

Alikuwa ameahidi kunioa lakini dalili za kufanya hivyo hazipo tena, nifanyeje?

Nina umri wa miaka 22. Kuna mwanamume tunayependana sana na amekuwa akiniambia kuwa atanioa nikimaliza masomo. Lakini naona ni kama amebadilika na sijui iwapo atatimiza ahadi yake. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Huna hakika kuwa mpenzi wako amebadili msimamo wake bali unashuku tu. Kama umeona dalili, ni muhimu uzunguzme naye ili ujue msimamo wake. Ukithibitisha hataki kuendelea na uhusiano hutakuwa na lingine ila kukubali ukweli huo na kuendelea na maisha yako.

 

Nimegundua yule niliyetaka kuoa ana watoto 2 nisiowajua

Hujambo shangazi? Nimekuwa na mwanamke mpenzi wangu kwa miaka miwili na tayari tumezaa mtoto pamoja. Nilikuwa nimepanga kumuoa lakini nimeshangaa kugundua kuwa ana watoto wengine wawili na hajawahi kuniambia. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ni kosa mkubwa kwamba mpenzi wako aliamua kuweka siri watoto wake hao na akakubali mpate mwingine huku ukiamini kuwa ndiye wa kwanza. Mambo ni mawili; umsamehe kosa lake hilo kisha umuoe na kuwakubali watoto wake hao ama umuache lakini uwajibike kugharamia malezi ya mtoto mliyezaa pamoja.

 

Niko shule ila kuna mwanamume mmoja anayetaka tuwe wapenzi; naogopa!

Mimi ni mwanafunzi wa shule ya upili. Kuna mwanamume ambaye amekuwa akiniandama kwa muda akitaka tuwe wapenzi. Ninampenda sana lakini naogopa kuhatarisha masomo na maisha yangu kwa kuingilia mapenzi wakati huu. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni muhimu kwamba unatambua hatari ya kushiriki mahusiano ya kimapenzi ukiwa bado shuleni. Ingawa unasema unampenda mwanamume huyo, ushauri wangu ni kwamba uweke kando suala hilo hadi utakapomaliza masomo. Mwelezee nia yako hiyo, kama kweli anakupenda atasubiri.

 

Mwanamume wangu haelewi mapenzi, nimsaidie kuelewa?

Nina uhusiano na mwanamume ambaye ninampenda kwa moyo wangu wote. Tatizo lake ni kuwa haelewi sana masuala ya mahaba na mara nyingi huniacha hali mbaya. Nahofia nikimwambia atahisi vibaya. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Watu wanapoamua kuwa wapenzi kila mmoja hufungua moyo wake kwa mwenzake na hawafai kufichana chochote. Ninaamini uhusiano wenu hatimaye utazaa ndoa na itakuwa vibaya kuanza maisha pamoja hali ikiwa hiyo. Shauriana naye na umsaidie kurekebisha mambo.