Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nimegundua aliyeahidi kunioa tayari ana mke, nifanyeje?

November 6th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nina umri wa miaka 24 na nimekuwa katika uhusiano wa kimapenzi kwa mwaka mmoja na nusu. Mpenzi wangu alikuwa ameahidi kunioa lakini nimepata habari kwamba alioa kisiri kisha akampeleka mke wake kwao mashambani kusudi nisijue. Nimethibitisha habari hizo lakini sijamwambia. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Huo ni usaliti wa hali ya juu wa kimapenzi. Ni jambo la kushangaza kwamba mwanamume huyo amemchumbia na kumuoa mwanamke mwingine mkiwa pamoja na anataka uendelee kusubiri ndoa. Hata usimwambie. Wewe bado ni mdogo kiumri na unaweza kupata kwa urahisi mpenzi mwingine. Anza mara moja kutafuta na siku ambayo utampata umwaibishe mwanamume huyo kwa alivyokutendea kisha umteme.

 

Natamani mume ila wote wanaonitaka wasema nikubali kuwa mke wa pili!

Vipi shangazi? Nina umri wa miaka 25 na nina watoto watatu ingawa bado sijaolewa. Ninatamani sana kuolewa lakini nimekosa mwanamume ambaye hajaoa. Wanaume wote wanaonipenda wameoa na wanataka kunioa mke wa pili. Je, nitakosea kuolewa mke wa pili?

Kupitia SMS

Siku hizi wanaume wengi hawako tayari kuwajibika katika kugharimia malezi ya watoto. Ndiyo maana baadhi yao wanatoweka ghafla wakijua wamewapa mimba wapenzi wao. Ninaamini kuwa wanaume ambao hawajaoa wanakuepuka kwa sababu wanaogopa kujitwika mzigo wa kulea watoto wako. Ndoa ni chaguo la mtu kwa hivyo hutamkosea mtu yeyote ukiamua kuolewa mke wa pili. Kama umepata mwanamume unayempenda na yuko tayari kukuoa mke wa pili, kubali ombi lake.

 

Kuna kipusa namlipia kodi ya nyumba lakini sijui anakoishi, je ananihadaa au vipi?

Hujambo shangazi? Nina mwanamke mpenzi wangu na tunafanya kazi miji tofauti. Ajabu ni kwamba nimemtembelea mara kadhaa mjini anakofanya kazi lakini hajanionyesha nyumbani kwake ilhali mimi ndiye ninayemlipia hiyo nyumba. Je, ananichezea?

Kupitia SMS

Ninashuku iwapo mwanamke huyo kweli anakupenda. Hata kama hungekuwa unamlipia nyumba ni muhimu kwako kujua anakoishi kwa sababu ni mpenzi wako. Kama wewe ndiye unayemlipia kodi, hiyo ni sawa na nyumba yako na una haki ya kulala humo. Huenda ana mpenzi mwingine ambaye humtembelea na ndiyo maana hataki ujue kwake usije ukawafumania. Chunguza ujue ukweli.

 

Tabia yake yafanya nishuku ikiwa kweli ananipenda, nahisi siko peke yangu

Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 30 na nina mwanamke mpenzi wangu ambaye ninampenda kwa moyo wangu wote. Hata hivyo, ninahisi kuwa ana mwanamume mwingine. Sababu ni kwamba wakati mwingine kuna mambo anayonitendea ambayo hunifanya nishuku kama kweli ananipenda. Nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, huna ushahidi kuwa mpenzi wako ana mwingine, unamshuku tu kutokana na tabia yake kwako. Usaliti wa kimapenzi ni kosa baya katika uhusiano na mara nyingi suluhisho lake huwa ni kuvunja uhusiano huo. Lakini siwezi kukushauri umuache mpenzi wako kutokana na kumshuku tu. Kwa kuwa umeona dalili hizo, fuatilia kwa makini mienendo yake hadi uthibitishe jambo hilo ndipo uamue iwapo utamuacha au la.

 

Namtamani sana lakini sijui jinsi ya kumuelezea hisia zangu, nishauri

Shikamoo shangazi! Kuna msichana fulani ambaye ninampenda sana lakini ninashindwa kumwambia. Ni jirani yangu na huwa tunakutana mara nyingi tunazunguza na baadaye ninaachwa nikiumia moyoni kwa mapenzi niliyo nayo kwake. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Jinsi pekee ya kujua iwapo msichana huyo pia anakupenda ni kumwelezea hisia zako. Usipofanya hivyo utaendelea kuumia tu na ukichelewa apatikane na mwanamume mwingine. Unasema kuwa mnaonana na kuongea mara nyingi kwa hivyo una nafasi ya kumdokezea penzi lako kwake.