Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nimegundua mke wangu alitoroka kwa mumewe!

October 15th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Nina mke ambaye nilimuoa mwaka uliopita. Tulipokutana aliniambia kuwa alikuwa na mpenzi na wakaachana. Lakini nimeshangaa kugundua kuwa alikuwa ameolewa na akamtoroka mume wake. Nimepata habari hizo kutoka kwa wanawake marafiki zake. Sijamwambia lakini nafikiria kumwambia kisha nimuache kwa sababu sitaki mgogoro kati yangu na mume wake. Nishauri.

Kupitia SMS

Iwapo habari hizo ni za kweli, ni wazi kuwa huyo si mwanamke mwaminifu kwani hakukwambia kuwa alikuwa ameolewa. Na iwapo alitoroka kutoka katika ndoa, mume wake akijua ameolewa na mwanamume mwingine anaweza kuzua balaa. Ni vyema uzungumze naye muachane ili kuepuka hali kama hiyo.

 

Mke amebadilika, akienda chama hurejea usiku na pia akinuka harufu ya pombe

Kwako shangazi. Nimeoa mke na tumezaa pamoja watoto wawili. Siku za hivi majuzi mke wangu ameingilia tabia isiyo nzuri na pia ameanza kunidharau. Amekuwa akitoka nyumbani mara kwa mara akisema anaenda chama na kurudi ni usiku. Juzi alirudi akinuka pombe na nilipomuuliza akaniambia kama simpendi nimwambie ajipange. Nampenda lakini siwezi kuvumilia tabia yake hiyo. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Mwanamume ndiye kichwa nyumbani kwake na anastahili heshima kutoka kwa watu wengine wote wa familia akiwemo mke wake. Tabia ya mke wako kuchelewa kurudi nyumbani na matamshi yake kwako yanakiuka kanuni hiyo na inaonekana yuko tayari kuondoka iwapo utaamua iwe hivyo. Kama umemkanya na hataki kujirekebisha, ni heri umuache aende.

 

Alirejea kwao na mie sikumfukuza, nifanyeje shangazi?

Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 22 na nimeoa. Hata hivyo, mke wangu alienda kwao mwezi mmoja uliopita. Akiondoka sikuwa nyumbani wala hakuniambia. Isitoshe, alipofika huko alibadilisha nambari yake ya simu. Niliweza kuipata kutoka kwa mwanamke rafiki yake lakini nikimpigia ama kumtumia SMS hajibu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kitendo cha mke wako kinaonyesha kuwa ameamua kukuacha. Sababu ni kwamba aliondoka wakati ambao hukuwepo nyumbani wala hakuwa amekwambia. Pili, amebadilisha nambari ya simu na hata baada ya wewe kuipata amekataa kuwasiliana nawe. Kilichobaki sasa ni wewe ufunge safari uende kwao ili mkazungumze akuelezee nia yake.

 

Huyu mume hupiga gumzo na wanawake kwa ploti, lakini mie nikiwepo hawaongei

Vipi shangazi? Nimeolewa na nina mtoto mmoja. Nina shida kuhusu tabia ya mume wangu. Ana mazoea ya kuongea na wanawake katika ploti tunamoishi wakati sipo karibu lakini nikiwa karibu huwa haongei nao. Tabia yake hiyo imenfanya nianze kumshuku. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Kauli yako ni kwamba unashuku kuwa mume wako ana uhusiano na baadhi ya wanawake majirani zenu. Si jambo la kawaida kwa mwanamume aliye na mke kutangamana na kupiga gumzo na wanawake katika ploti anamoishi. Isitoshe, unasema ukiwa karibu huwa hazungumzi nao. Ni muhimu umuulize ili ujue hasa huwa wanazungumzia nini kisha umwelezee wazi kuwa tabia yake hiyo inakutatiza. Ukifanya hivyo atajua kuwa unafuatilia mienendo yake na kama anathamini ndoa yenu, atakoma.

 

Ataka tuoane ilhali mie sijui kwao na yeye hajafika kwetu

Shikamoo shangazi! Mwanamume ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka miwili anataka kunioa kabla hajanipeleka kwao wala hajaenda kwetu. Nahisi itakuwa makosa kwangu kuolewa na mtu ambaye wazazi na jamaa zangu hawamjui na pia mimi sijulikani kwao. Nishauri.

Kupitia SMS

Kuna utaratibu ambao umewekwa na jamii kuhusu ndoa halali. Utaratibu huo hasa unatilia maanani kuhusishwa kwa wazazi na jamaa wa wahusika katika mipango ya ndoa. Sielewi ni kwa nini mpenzi wako anataka kukuoa kisiri bila kuhusisha jamaa zenu. Shikilia msimamo wako huo. Kama ana nia njema kwako, atakubali utaratibu huo.