Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nimempenda msichana lakini anavuta sigara sana

May 16th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Kuna msichana fulani tunayependana na nataka kumuoa. Tatizo ni kuwa anavuta sigara sana na ninajua sigara zina madhara mengi ikiwemo kuathiri vibaya uwezo wa mwanamke wa kuzaa. Nishauri.

Kupitia SMS

Mtu huchagua mchumba kwa kuzingatia maumbile na tabia. Kama tabia ya mpenzi wako ya kuvuta sigara inakuchukiza, bila shaka utaendelea kuchukizwa ukimuoa. Mambo ni mawili – ukubali kumuoa na kumpenda na tabia yake hiyo ama umuache utafute mwingine.

 

Mpenzi hunipa kila kitu lakini hapokei simu na SMS hajibu

Shangazi mimi ninamshuku mpenzi wangu. Sababu ni kuwa nikimpigia simu au kumtumia SMS hajibu. Nikimuuliza anasema hapendi kuzungumza sana. Hata hivyo ananitimizia mahitaji yangu ya kifedha. Nishauri.

Kupitia SMS

Madai yake ni kisingizio tu, ni lazima kuna sababu zinazomfanya asijibu simu zako, labda ana mwingine. Haiwezekani kwa wapenzi kuishi bila kuwasiliana. Chunguza ujue ukweli ili uchukue hatua inayofaa.

 

Kidosho wa mume bado anampigia simu

Vipi shangazi? Nimeolewa kwa miezi mitatu sasa lakini naona muda si mrefu nitajiondoa katika ndoa. Sababu ni kwamba aliyekuwa mpenzi wa mume wangu amekuwa akimpigia simu kumwambia bado anampenda. Juzi niliamua kumpigia kujua anachotaka kutoka kwa mume wangu akanitukana vibaya na kunionya kuwa alimjua kabla yangu. Nimelalamika mara kadhaa kwa mume wangu lakini hajafanya chochote kumkanya. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ni jambo la kushangaza kwamba mume wako hataki kumkomesha mpenzi wake wa zamani anayetishia kuvunja ndoa yenu. Nahisi wawili hao hawajaachana kabisa na ndiyo maana amepata ujasiri wa kukutukana kwa sababu anajua mume wako hawezi kumfanya chochote. Sitakulaumu ukichukua hatua unayofikiria.

 

Nilidhani penzi langu kwake limekolea kumbe ana mwingine!

Kwako shangazi. Tafadhali nisaidie kwani nina maumivu makubwa moyoni kutokana na mahaba. Nimekuwa na mpenzi kwa miaka miwili sasa na nilikuwa na mpango wa kumuoa. Hata hivyo nimebadili nia yangu hiyo baada ya kupata ujumbe wa kimapenzi kwa simu yake ambao amemtumia mwanamume mwingine. Nishauri.

Kupitia SMS

Hizo ni dalili za mtu ambaye si mwaminifu. Fuatilia jambo hilo ujue huyo mwanamume ni nani na uhusiano uliopo baina yao. Ukijua ukweli utafanya uamuzi unaofaa.

 

Ataka kunioa ila ana kipusa aliyemzalisha akamuacha, naogopa

Hujambo shangazi? Kuna mwanamume tunayependana sana lakini nimegundua alizaa mtoto na mwanamke aliyekuwa mpenzi wake ingawa waliachana. Ameahidi kunioa lakini jambo hilo limeniingiza baridi. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Sidhani una sababu ya kuwa na wasiwasi kwa sababu wawili hao waliachana hata baada ya kuzaa mtoto pamoja. Mwanamke huyo alikuwa mpenzi wake tu, hakuwa mke wake.

 

Jamani sioni mume anayefaa kunioa!

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 28 na nimekuwa nikitafuta mpenzi kwa miaka kadhaa. Nimekutana na wanaume wengi waliodai kunipenda lakini hatimaye ninagundua ni walaghai wa kimapenzi wasioweza kudumisha mpenzi mmoja. Nimeanza kuona kama nitaishi bila mume. Nishauri.

Kupitia SMS

Tunaishi wakati ambao kuna walaghai wengi wa kimapenzi, si wanaume pekee bali pia wanawake. Kulingana na umri wako, wewe bado ni mchanga na ni mapema sana kukata tamaa. Ukiwa na subira hatimaye utampata mwanaume anayekufaa.

 

Natamani turudiane

Shikamoo shangazi! Nilikuwa na mpenzi niliyempenda sana lakini tuliachana mwaka uliopita. Ninateseka sana moyoni kwa kumkosa na natamani sana turudiane. Tafadhali nisaidie.

Kupitia SMS

Wewe ndiye unajua kilichowafanya muachane na kama unafikiri ni jambo ambalo mnaweza kurekebisha, basi mweleze.