Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nimempenda mwanamume kupitia simu na mtandao tu

August 9th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nina uhusiano na mwanamume ambaye bado hatujaonana, tumekuwa tukiongea kwa simu tu. Alipata nambari yangu kutoka kwa msichana rafiki yangu na nimevutiwa na maumbile yake kutokana na picha yake ambayo ameweka kwenye mtandao. Nishauri.

Kupitia SMS

Huwezi kuwa na uhusiano na mtu ambaye hujakutana naye, unamjua kwa sauti tu na picha yake. Mtu anaweza kuweka picha ambayo si yake katika mtandao, kwa hivyo huna hakika kama iliyopo ni yake. Fanya juhudi muonane ana kwa ana ndipo uweze kuamua iwapo anakufaa au la.

 

Mama niliyezaa naye hataki mtoto anione

Hujambo shangazi? Nilikuwa nimeoa lakini nikaachana na mke wangu akarudi kwao na mtoto wetu. Ingawa sikuwa nimemlipia mahari, mtoto huyo amekuwa akitaka kuja kwangu tuishi pamoja lakini mama yake na wazazi wake wanamkataza. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Una haki juu ya mtoto huyo hata kama hukuwa umemlipia mahari mama yake. Hata hivyo, kama mtoto huyo hajahitimu miaka 18, hawezi kuachwa ajiamulie kuhusu ni nani anayetaka kuishi naye kwani kuna mambo mengi ambayo hawezi kuelewa. Mvutano wa aina hii hasa husuluhishwa kisheria kupitia kortini, kwa hivyo unaweza kuchukua hatua hiyo.

 

Ananitimizia mahitaji, shida anataka kuonja tunda nikiwa shuleni

Shikamoo shangazi! Mimi ni mwanafunzi na nina uhusiano na mwanamume anayefanya kazi. Amekuwa akinitimizia mahitaji yangu ya kifedha na ameahidi kunioa nikikamilisha safari yangu kielimu. Tatizo ni kuwa anataka tushiriki mahaba nami siko tayari. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Mahusiano ya kimapenzi ni haramu kwa watoto wa shule kama wewe kwa sababu yanawafanya washindwe kuzingatia ipasavyo masomo yao. Iwapo kweli unahitaji ushauri wangu, mwambie mwanamume huyo akuache kwanza umalize masomo ndipo muendelee na uhusiano wenu. Hatua yake ya kutaka mshiriki mahaba ni ishara kuwa hakujali sana kwani kuna hatari ya wewe kupata mimba na kulazimika kuacha shule.

 

Sitaki kuoa lakini nina haja ya kupata mtoto

Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 38 na nimeamua kwamba sitaoa kwa sababu sina uwezo wa kutunza familia. Hata hivyo, ninataka sana kupata mtoto hata kama sitamuoa mama yake. Naomba unisaidie kutafuta mwanamke anayetaka mtoto.

Kupitia SMS

Nitakwambia ukweli. Mpango wako huo hautafaulu kwa sababu hakuna mwanamke aliye tayari kuzaa na mwanaume asiye tayari kulea. Tunaambiwa kuzaa si kazi, kazi ni kulea. Endelea kutafuta tu lakini nakuhakikishia utaambuliwa patupu.

 

Nataka kuoa lakini mke wangu hataki mke mwenza kamwe

Shangazi mimi nimeoa na tuna mtoto mmoja. Nimekuwa na uhusiano wa pembeni na nimeishia kumpenda sana mwanamke huyo nataka kumuoa. Shida ni kuwa mke wangu hataki kuwa na mke-mwenza. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ni ajabu kwamba unamlaumu mke wako kwa kupinga mpango wako wa kuoa mke wa pili. Je, ulipomuoa ulimwambia kuwa baadaye utamtafutia mke mwenza? Wewe hasa ndiye umemkosea kwa kuanzisha uhusiano nje ya ndoa na sasa unataka kuhalalisha uhusiano huo. Mimi kamwe siungi mkono. Mimi sina ushauri kwako lakini ni onyo. Ni heri uondolee mbali mpango wako huo kwani hautafaulu kama mke wako hataki. Ukijaribu kumlazimisha atakuacha na huo mpango wako wa kando.

 

Msichana mpenzi wangu alipata kazi juzi, sasa hachukui simu wala kujibu SMS

Shangazi pokea salamu zangu. Msichana ambaye tumekuwa wapenzi tukisoma alipata kazi majuzi. Tangu hapo tabia yake kwangu imebadilika ghafla kwani hapokei simu wala kujibu SMS zangu. Ninashuku amenitema na hataki kuniambia. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Hizo ni ishara za kutosha kwamba msichana huyo ameamua kuvunja uhusiano kati yenu na labda ameshindwa kukwambia hivyo. Ni lazima ukubali ukweli huo kwanza ndipo uweze kumsahau na kuendelea na maisha yako.