Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nimeolewa na nimeshika mimba ya bosi wangu

March 12th, 2020 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 36 na nimeolewa. Nina uhusiano wa pembeni na bosi wangu na nimegundua kuwa nimepata mimba yake. Mume wangu anaishi mbali na ninajua haitakuwa rahisi kumshawishi kuwa mimba hiyo ni yake kwa sababu hatujaonana kwa miezi miwili. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hayo ndiyo matokeo ya mapenzi haramu. Ni matamu kama asali lakini pia yanaweza kugeuka na kuwa machungu kama shubiri. Huo wako ni ulaghai wa kimapenzi na sitakubali kuwa mshirika wako kwa kukushauri kuhusu jinsi ya kumhadaa mume wako. Maji uliyavulia nguo wewe mwenyewe. Sasa huna budi kuyaoga.

 

Amegeuka ghafla na kusema hataki penzi, wala ndoa yenyewe

Kwako shangazi. Nimekuwa na mchumba kwa miaka miwili na amekuwa akiniahidi kuwa atakuwa mke wangu. Sasa amebadili nia ghafla na kuniambia kuwa hana mpango wa kuolewa na pia anataka tuachane. Ninashuku kuwa amepata mwingine na uamuzi wake huo umeniudhi sana kwa sababu nimepoteza wakati na pesa zangu kwake. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Uhusiano wa kimapenzi ni sawa tu na mchezo wa bahati nasibu ambapo mtu hupata na wakati mwingine kupoteza. Inaumiza sana kwa mtu ambaye umempa moyo wako na kutumia wakati na pesa zako kwake kukuacha ghafla. Awe amepata mwingine au la, hakuna unaloweza kufanya. Ameamua iwe hivyo na itabidi ukubali ukweli huo ndipo uweze kuendelea na maisha yako.

 

Ndio nimeanza maisha rasmi na huyu tayari anasisitiza tuoane

Shikamoo shangazi! Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 24. Nilimaliza masomo ya chuo kikuu mwaka uliopita na tayari nimepata kazi. Mwanamume mpenzi wangu anataka tufunge ndoa lakini nahisi kuwa mimi bado ni mdogo. Nishauri.

Kupitia SMS

Sielewi unamaanisha nini ukisema kuwa wewe bado ni mdogo. Sababu ni kuwa mtu hutambuliwa kuwa mtu mzima akihitimu umri wa miaka 18. Wewe umepitisha umri huo, umemaliza masomo na pia umepata kazi, unajitegemea. Labda uwe na sababu nyingine ya kutotaka kuolewa sasa lakini kamwe si umri.

 

Tuliachana alipoanza kunisukuma nimpe asali; bado aniandama

Kwako shangazi. Niliachana na mpenzi wangu miezi mitatu baada ya kuanzisha uhusiano wetu. Sababu ni kwamba alitaka kunilazimisha tushiriki mapenzi ilhali mimi sijawahi kufanya hivyo na siko tayari kwa sasa. Miezi miwili baadaye amekuja kwangu kuniomba turudiane. Nishauri.

Kupitia SMS

Mtu anayempenda mwenzake kwa dhati hafai kumlazimisha kufanya mambo. Ulifanya vyema kushikilia msimamo wako huo na labda alikuacha akidhani utambembeleza akurudie. Kwa sababu amerudi mwenyewe, na iwapo bado unampenda, mpe nafasi tena lakini hakikisha kuwa uhusiano huo umedumu kwa maelewano, usikubali kulazimishwa kufanya jambo lolote usilotaka.

 

Nashuku anamgawia uhondo mkubwa wake kazini kwa jinsi wanavyoongea sana

Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 36 na nina mpenzi. Ninashuku kuwa mpenzi wangu ana uhusiano na mkubwa wake kazini. Sababu ni kuwa wamekuwa wakiwasiliana sana kwa simu na nikimuuliza ananiambia ni mambo ya kazi. Nina wasiwasi, naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni jambo la kawaida kwa watu wanaofanya kazi pamoja kushauriana kuhusu kazi yao hata wasipokuwa kazini. Kama mazungumzo kati ya mpenzi wako na bosi wake huwa yanahusu kazi, huna sababu ya kulalamika. Pili, kumbuka kuwa huyo ni mpenzi wako tu, si mke wako na ana haki ya kukuacha wakati wowote akitaka. Kwa kuwa bado mko pamoja na amekuambia hana uhusiano mwingine na bosi wake ila kazi, inakushauri umwamini.