Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nimepata fununu mke ana mimba na sidhani ni yangu…

November 13th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nina mke na tumejaliwa watoto wawili. Ninafanya kazi mbali na nina mwaka mmoja sasa kabla sijafika nyumbani. Ajabu ni kwamba nimepata habari kuwa mke wangu ana mimba. Nina hakika hiyo mimba si yangu na hiyo ina maana kuwa mama watoto amekuwa akitembea nje. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hilo ni suala zito na linaweza tu kutatuliwa kati yako na mke wako. Kama hujawa nyumbani kwa mwaka mzima na mke wako ana mimba, bila shaka mimba hiyo ni ya mwanamume mwingine. Hali hiyo ni mojawapo ya changamoto za ndoa na pia mahusiano ya kimapenzi ambapo mtu anaishi mbali na mwenzake. Ni muhimu uzingatie jambo hili katika uamuzi ambao utachukua.

 

Nilikataa penzi lake sasa namtamani sana, lakini naona aibu kumuelezea

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 19. Kuna kijana ambaye alikuwa akimtuma rafiki yake kwangu kuniambia kuwa ananipenda lakini nikamkataa kwa sababu nilidhani kuwa ulikuwa mzaha. Ukweli ni kwamba ninampenda lakini naona aibu kumwambia hivyo ilhali nilimwambia simtaki. Nishauri.

Kupitia SMS

Kama umechunguza na kugundua kuwa mapenzi yake kwako ni ya dhati na wewe pia unampenda, usione aibu kumwelezea ukweli. Unaweza kumwambia wewe mwenyewe ama umtume huyo rafiki yake ili amwambie. Baada ya hapo mtakutana mzungumze zaidi kuhusu hisia zenu.

 

Naogopa kumuacha mpenzi ambaye ni mwanafunzi kama mimi, nifanyeje?

Shikamoo shangazi! Mimi ni mwanafunzi wa shule ya upili na nina uhusiano wa kimapenzi na msichana mwanafunzi mwenzangu. Walimu wamegundua kuhusu uhusiano wetu na wanataka tuachane. Ninampenda sana msichana huyo na nikimuacha nitaumia sana moyoni. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Walimu wenu wana nia nzuri kwenu kwa kuwataka mvunje uhusiano wenu na mimi pia ninawaunga mkono. Sababu ni kwamba mapenzi yanaweza kuchukua sehemu kubwa ya mawazo yako na hivyo kuathiri masomo yako. Nina hakika wazazi wenu pia wakijua watapinga uhusiano huo. Ushauri wangu ni kwamba mvunje uhusiano huo kwa sasa na badala yake mzingatie masomo. Mkimaliza masomo mtaendeleza mapenzi yenu.

 

Naishi mashambani na wakwe na nahofia manung’uniko yao yatanivunjia ndoa

Shikamoo shangazi! Nimeolewa kwa miaka miwili sasa. Mume wangu pekee ndiye anayefanya kazi ilhali mimi ninaishi nyumbani mashambani na wazazi wake. Tatizo ni kwamba wazazi wake hao hawatosheki licha ya mambo yote ninayowafanyia, ikiwemo kuwapikia na kuwafulia nguo mbali na shughuli zingine nyingi za nyumbani. Wamekuwa wakilalamika kwake eti nimewatelekeza na nahofia kuwa udaku wao huo hatimaye utazua ugomvi kati yangu na mume wangu. Nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Hiyo si hali ya wazazi wa mume wako tu bali ni hali ya binadamu kwa jumla. Binadamu ni kiumbe ambaye ni vigumu sana kumtosheleza. Jinsi pekee ya kuepuka fitina hiyo ni kujitenga na wakwe zako. Shauriana na mume wako kuhusu jambo hilo kwa lengo la kutafuta makao yenu mbali kidogo na nyumbani kwa wazazi wenu. Badala yako, mnaweza kuajiri mfanyakazi wa kuwatunza kisha muwe mkiwatembelea tu kuwajulia hali.

 

Nimeanza kutumia mbinu za upangaji uzazi na sasa sipati hedhi, shida ni nini?

Hujambo shangazi? Nimeolewa na nina watoto wawili. Nimeamua kwamba sitaki kupata mtoto mwingine kwa hivyo ninatumia dawa za kupanga uzazi. Tangu nianze kutumia dawa hizo, huu sasa ni mwezi wa tatu na sijapata hedhi. Je, shida ni nini?

Kupitia SMS

Siwezi kujua shida iliyopo kwa sababu mimi sina ujuzi wa kimatibabu. Ninaamini kwamba ulimuona mtaalamu wa afya ya uzazi kabla hujaanza kutumia dawa hizo kwa hivyo itakuwa bora urudi kwake ili umwelezee shida yako. Ninaamini atakutafutia suluhisho.