Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nimepata wa kunioa ila nasubiri niliyezaa naye akahepa

November 5th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nina umri wa miaka 23 na nina mtoto ingawa bado sijaolewa. Mwanamume tuliyezaa pamoja alikuwa ameahidi kunioa lakini akatoweka pindi tu nilipomwambia kuwa nina mimba yake. Tangu wakati huo sijamuona na pia hapatikani kwa simu; nafikiri alibadilisha nambari yake. Nimekuwa nikisubiri kwa matumaini kwamba siku moja atajitokeza na kunioa. Kuna mwanamume mwingine anayenitaka na yuko tayari kunioa. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Unajidanganya kwa kutarajia kwamba mwanamume mliyezaa pamoja atakurudia ilhali alitoweka wakati ambao ulimhitaji zaidi. Kitendo chake hicho kinaonyesha kuwa hakuwa na mapenzi ya dhati kwako na ahadi yake ya kukuoa ilikuwa uongo mtupu. Kama umepata mwingine ambaye unaamini anakufaa katika maisha yako, mkubali ili uweze kuendelea na maisha yako.

 

Ameniambia nisijali kuhusu umri wala mtoto niliyezaa, yeye anipenda jinsi nilivyo!

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 24 na nina mtoto niliyemzaa na mpenzi wangu wa awali. Kuna mwanamume mwenye umri wa miaka 20 ambaye anataka tuwe wapenzi na pia yuko tayari kunioa. Mimi pia nampenda sana ila nahisi kuwa ni mdogo kwangu. Nimemwelezea na ameniambia nisijali kuhusu tofauti ya umri wala mtoto niliye naye. Hiyo ni sawa kweli?

Kupitia SMS

Nimeelewa kuwa hofu yako ni tofauti ya umri kati yako na mwanamume huyo. Hiyo kamwe haifai kuwa pingamizi kwa uhusiano wenu kwani tofauti iliyopo ni ndogo sana. Iwapo, mbali na kumpenda, unaamini anatosha kuwa mume wako, hiyo ni sawa. La ziada ni kwamba amemkubali mtoto wako.

 

Nampenda na yuko tayari kunioa, hofu ni wazazi wangu kwani anatoka jamii tofauti

Shikamoo shangazi! Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 25. Mpenzi wangu ambaye tumekuwa pamoja kwa miaka miwili amesubiri hadi nikamaliza chuo kikuu. Sasa anataka kunioa huku nikitafuta kazi na pia kuendelea na masomo ya ziada. Ninataka kuwafahamisha wazazi lakini naogopa kwa sababu anatoka jamii tofauti na yangu. Nishauri.

Kupitia SMS

Huna sababu ya kuogopa kuwafahamisha wazazi wako kuhusu mpango wa maisha yako. Wewe sasa ni mtu mzima na una uwezo na haki ya kuamua mwenyewe kuhusu mwelekeo wa maisha yako. Si lazima uolewe na mwanamume kutoka jamii yako. Unaweza hata kuolewa na mtu wa taifa ama rangi tofauti na yako. Ninaamini wazazi wako wanaelewa hivyo.

 

Mpenzi aishiye mbali anataka nimtumie nauli ndiyo tuonane, kweli atakuja?

Vipi shangazi? Nina umri wa miaka 21 na nina mpenzi ambaye nampenda sana. Anaishi mji tofauti na hatujaonana kwa muda mrefu. Sasa ananiambia nimtumie nauli ili anitembelee lakini ninashuku iwapo atakuja. Waonaje?

Kupitia SMS

Hujaelezea ni kwa nini unamshuku mpenzi wako. Kama amewahi kukudanganya hapo awali, una sababu ya kumshuku. Kama hajawahi kutumia uongo kwako, unafaa kumwamini na kumtumia nauli anayotaka kwani huenda anatamani sana kukuona.

 

Nimegundua mume ana mke na watoto wengine na hata amewajengea, mie sitaki mke mwenza

Kwako shangazi. Ni miezi minane sasa tangu niolewe. Nimegundua kuwa mume wangu ana mke mwingine na watoto ambao amewajengea nyumba mahali pengine lakini hajaniambia. Nilipomuuliza alinifokea na kuniambia nisiwahi kumuuliza kuhusu jambo hilo. Ingawa nampenda, siwezi kukubali mwanamke mwingine katika maisha yangu ya ndoa. Nishauri.

Kupitia SMS

Kauli yako ya mwisho inaonyesha kuwa tayari umepata suluhisho la tatizo lako. Unasema hutamkubali mwanamke mwingine katika ndoa yako. Umethibitisha kuwa mume wako ana mke mwingine na kwamba hayuko tayari kuachana naye. Hiyo ina maana kuwa huna linguine la kufanya ila tu kutoka katika ndoa hiyo.