Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nimependa mwenye umri sawa na mama yangu…

November 7th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nina umri wa miaka 28 na nimependana na mwanamke ambaye kwa umri anaweza kuwa mama yangu. Kwa sababu hiyo, tumeficha sana uhusiano wetu na hata yeye mwenyewe hapendi tukionekana pamoja hadharani kwa sababu ya tofauti hiyo ya umri. Nimemwambia wazi kuwa siwezi kumuoa lakini hataki tuachane. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Kwa kawaida, uhusiano wa dhati wa kimapenzi unafaa kuzaa ndoa. Hiyo si kweli katika uhusiano wenu kwa sababu umesema wazi kwamba huwezi kumuoa mwanamke huyo. Amegundua kuwa itakuwa vigumu kwake kupata mume kutokana na umri wake huo kwa hivyo ameamua kukutumia kwa manufaa yake bila kujali maisha yako. Kama una nia ya kuoa, unapoteza wakati wako kwa mwanamke huyo. Achana naye utafute mke.

 

Nilijitambulisha kwa mke wa mpenzi wangu ambaye yuko tayari kunioa

Kwako shangazi. Nimekuwa nikishuku kuwa mwanamume mpenzi wangu ana mke na nimechunguza hadi nikathibitisha. Nilipomuuliza aliungama. Katika harakati za kuchunguza, nilijuana na mke wake na sasa anajua kuwa mume wake ni mpenzi wangu. Ninampenda sana mwanamume huyo naye vile vile ananipenda na yuko tayari kunioa mke wa pili. Nishauri.

Kupitia SMS

Hali kwamba mke wa mpenzi wako anajua kuhusu uhusiano wenu na mume wake yuko tayari kukuoa ni ishara kuwa wameshauriana kuhusu mpango huo na hana pingamizi. Wewe pia unasisitiza kuwa unampenda mwanamume huyo hata baada kujua kuwa ana mke. Kama uko tayari kuolewa mke wa pili, kubali ombi lake.

 

Nimependana na mwanamke tajiri ila shida ni kuwa hana uwezo wa kunizalia

Hujambo shangazi? Nimependana na mwanamke ambaye ana pesa sana na hata yuko tayari kunigawia sehemu ya mali yake ili tuishi pamoja. Tatizo lake ni kwamba hana uwezo wa kupata watoto. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Uamuzi wako utategemea na unachohisi ni muhimu maishani mwako. Kama ni pesa, utazipata kupitia kwa mwanamke huyo bora tu ukubali ombi lake. Kama ni watoto, itabidi umsahau yeye na utajiri wake utafute mwingine anayeweza kukuzalia watoto.

 

Mpenzi amefanya nimchukie sana kwa kunitusi, sioni nikivumilia hali hiyo

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 26 na niko katika uhusiano wa kimapenzi. Hivi majuzi tulikosana na mpenzi wangu na akanitusi vibaya sana hata ninamchukia. Bado ninafikiria iwapo nitaweza kuendelea na uhusiano huo kwani siwezi kuvumilia matusi ya aina hiyo. Nishauri.

Kupitia SMS

Kila uhusiano unafaa kuwa na masharti ambayo ni lazima kila mhusika ayazingatie ili kuudumisha. Matokeo ya ukiukaji wa masharti ni kuvunjika kwa uhusiano. Unasema kuwa matusi ya mpenzi wako yalikuchoma sana moyoni na huwezi kuyavumilia. Kwa sababu hiyo, ni muhimu umwelezee ili liwe mojawapo la masharti katika uhusiano wenu, kwamba hatawahi kukutukana tena. Uamuzi wako utategemea na iwapo au la atakubali.

 

Nimetekwa na kipusa mwenye mtoto lakini sijui kama nitaweza kumjali kama wangu

Shikamoo shangazi! Kuna mwanamke ambaye ameteka moyo wangu na niko tayari kumuoa. Lakini kuna kikwazo ambacho kimetokea. Ameniambia kuwa ana mtoto kutokana na uhusiano wa awali. Nampenda sana lakini sina hakika iwapo nitaweza kumlea na kumpenda mtoto huyo kama wangu. Nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Kuna mambo mawili ambayo unafaa kuzingatia kuhusiana na hali hiyo. Kwanza, huwezi kumtenganisha mwanamke huyo na mtoto wake. Pili, ukimuoa mwanamke huyo atatarajia kwamba utamkubali na kumpenda mtoto huyo kama wako. Kama unajua hutaweza, ni heri uachane naye kwa sababu hatavumilia kuona ukimbagua mtoto huyo dhidi ya wengine ambao mtazaa pamoja.