Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nimezaa naye ila ni mume wa mtu na ni mhubiri pia

May 15th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHANGAZI hujambo? Kuna mwanamume ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka minne sasa hata nimezaa naye mtoto mmoja. Hata hivyo, yeye ni mume wa mtu tena ni mhubiri wa kanisa ninakoabudu. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ni jambo la ajabu tena lenye aibu kwamba umekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mume wa mwenyewe tena ni mhubiri wako. Je, hayo ndiyo maadili ya maisha anayowapa katika kanisa lake? Yeye pia ni mhubiri mnafiki kwani vitendo vyake ni kinyume kabisa na maadili ya kidini. Unayofanya ni makosa makubwa na kama kweli unahitaji ushauri wangu, basi nakuambia umkome kabisa mwanamume huyo kwani ni mume wa mwenyewe na unahatarisha ndoa yake.


Natamani mwalimu wangu wa zamani

Shikamoo shangazi! Kuna mwanamume aliyekuwa mwalimu wangu ambaye namtamani ingawa tayari ameoa. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ashakum si matusi lakini naona wewe umekosa adabu. Kama mwanamume huyo alikuwa mwalimu wako unafaa kumheshimu kwa sababu ni sawa na mzazi wako kwani alikulea kimasomo. Isitoshe, huyo sasa ni mume wa mwenyewe. Wanaume wamo tele duniani; tafuta wako.


Ameoa na ananitaka, nimechanganyikiwa

Shangazi nina umri wa miaka 27 na kuna mwanamume anayenipenda sana nami pia nampenda. Tatizo ni kwamba ana mke na watoto wawili. Anataka sana kunioa na hivi sasa anasisitiza twende kwa wazazi ili aanzishe mipango ya ndoa. Nitafanya nini na sitaki kumuacha?

Kupitia SMS

Inaonekana umeamua kuolewa mke wa pili kwani unajua mwanamume huyo ana familia na unasema hutaki kumuacha. Hata hivyo, kabla hamjaanza hiyo mipango ya ndoa ni muhimu ashauriane na mke wake ili ajue msimamo wake kuhusu suala hilo. Itakuwa kazi bure kwako kuolewa kisha upelekwe katika boma ambako hutakuwa na amani kwa sababu ya vikwazo vya mke wake.

 

Kumbe atembelea mpenzi si shangazi!

Shikamoo shangazi! Nimekuwa na mpenzi kwa miezi miwili sasa na nimekuwa nikimpa chochote anachotaka. Amekuwa akisafiri mara kwa mara akisema anamtembelea shangazi yake, lakini nimegundua amekuwa akienda kwa mwanamume mwingine. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Sasa umejua kwa hakika kuwa msichana huyo si mwaminifu kwako kama kweli amekuwa akimtembelea mwanamume mwingine na kukuhadaa kuwa anaenda kwa shangazi yake. Utaamua mwenyewe kama utaendeleza uhusiano na mtu asiye mwaminifu kwako.

 

Amenikosha moyo lakini hanipi nafasi

Kwako shangazi. Kuna mrembo amevutia moyo wangu na sijui nitamwelezea vipi kwani hataki hata kunipa nafasi ya kujieleza. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Hata kama unampenda mwanamke huyo kushinda nafsi yako, juhudi zako ni sawa na kumkama maziwa kuku kwani hata nafasi ya kujieleza hataki kukupa. Unapoteza wakati wako bure. Achana naye.

 

Nina HIV na nasaka mke, utanitafutia?

Shangazi pokea salamu zangu. Mimi nina virusi na sijaoa ingawa nimehitimu umri wa kuwa na mke. Tafadhali nakuomba unitafutie mwanamke aliye katika hali sawa na yangu kiafya ili nimuoe kwani ninaamini ninaweza kuwa na familia. Sitajali hata kama atakuwa na mtoto. Mungu akujalie uzidi kutushauri.

Kupitia SMS

Ni jambo la kutia moyo kwamba umekubali hali yako hiyo na unaamini kuwa unaweza kuishi maisha ya kawaida ukipata mwenzako. Ninaamini kuna wanawake walio katika hali na mipango sawa na yako maishani. Hata hivyo, sina uwezo wa kukutafutia kwani mke au mume huwa chaguo la mtu binafsi. Isitoshe, kazi yangu katika ukumbi huu ni kutoa ushauri tu. Ni matumaini yangu kuwa walio katika hali hiyo watasoma ujumbe wako huu na atakayevutiwa kuwasiliana nawe. Kila la heri.