Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nina mume lakini namuwaza sana 'ex' wangu

December 3rd, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nimeolewa na nina mtoto mmoja. Tatizo langu ni kuwa mara nyingi nimekuwa nikimfikiria sana aliyekuwa mpenzi wangu na mawazo hayo yamepunguza mapenzi yangu kwa mume wangu hata amegundua ingawa hajui ni kwa nini. Nimejaribu sana kumsahau mwanaume huyo lakini nimeshindwa.

Kupitia SMS

Hali yako hiyo ni thibitisho kwamba unampenda mpenzi wako wa zamani kuliko mume wako. Ndiyo sababu hisia zako kwa mume wako zimepungua na bila shaka hali hiyo itaathiri vibaya ndoa yenu kwani tayari amegundua. Ni heri umwambie ukweli ili mshauriane na kuchukua hatua inayofaa kwani hakuna haja ya kuendelea na ndoa isiyo na mapenzi.

 

Nimevunja uhusiano mara mbili kwa ‘tunda kulibania’

Hujambo shangazi? Nimewahi kuwa katika uhusiano na wanaume wawili lakini kila tuliyeshikana aliniacha nilipokataa kushiriki mapenzi naye. Naogopa kuingia katika uhusiano mwingine hali iwe iyo hiyo. Nishauri.

Kupitia SMS

Usijute kwa kuachwa kwa sababu ya msimamo wako mkali kuhusu jambo ambalo hujawa tayari kwalo. Mwanamume anayekupenda kwa dhati hawezi kukuacha kwa sababu ya jambo hilo. Inaonekana waliokuacha walitaka kukutumia tu. Usiogope kuingia tena katika uhusiano kwani ni kwa njia hiyo ambapo utapata anayekupenda bila masharti.

 

Mume sasa akana watoto, eti si wake

Za kwako shangazi? Niliolewa na tukaishi kwa miaka mitano bila kupata watoto lakini hatimaye tumejaliwa watoto wawili. Sasa mume wangu ameanza kuwakataa na kunifukuza nyumbani akisema watoto hao si wake. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Iwapo mume wako anashuku kuwa ulipata watoto hao kutoka nje na wewe unaamini ni wake, mwambie agharimie ukaguzi wa kimatibabu ukweli ujulikane badala ya kudai tu kuwa watoto si wake. Jaribu pia kuwahusisha jamaa wa familia zenu katika kutatua suala hilo.

 

Tuliyehusiana miaka 2 ameoa mwingine ila ataka tuendelee

Vipi shangazi? Mwanamume ambaye tumekuwa na uhusiano kwa miaka miwili ameoa mwanamke mwingine lakini ameniomba tuendelee na uhusiano akisema bado ananipenda. Mimi pia nampenda sana na nilitarajia kuwa angenioa. Nishauri.

Kupitia SMS

Sidhani unaamini madai ya mwanamume huyo ilhali mlikuwa wapenzi na akakuacha akaoa mwingine. Kama amekuzuzua kwa mapenzi yake kiasi cha kutofikiria ni sawa tu lakini kuwa tayari kwa masaibu yoyote yanayoweza kutokana na uhusiano kama huo kwa sababu utakuwa haramu.

 

Mama ya mwanadada nimpendaye ataka penzi langu

Hujambo shangazi? Ninapendana na msichana tunayesoma pamoja chuo kikuu na pia sisi ni majirani mtaani. Mama yake amekuwa akinifuata akitaka tuwe wapenzi na mimi sitaki. Nishauri.

Kupitia SMS

Sasa unataka ushauri gani kutoka kwangu na tayari unajua analotaka kwako mama yake haliwezekani? Kama hana habari mwambie kuwa binti yake ni mpenzi wako na huwezi kumpa anachotaka.

 

Dume langu ni tapeli

Vipi shangazi? Nimependana na mwanamke fulani kwa mwaka mmoja sasa. Tunasaidiana kwa hali na mali. Lakini nimegundua ni muongo sana, hunidanganya peupe hata kwa mambo ninayojua kwa hakika na nahisi kuwa ni hatari sana kuishi na mtu kama huyo. Je, nimuache au niendelee naye?

Kupitia SMS

Ni wazi kuwa tabia yake hiyo ya uongo inakukera na hali itakuwa mbaya zaidi akiendelea kuwa hivyo hasa atakapokuwa mke wako. Kama unahisi huwezi kuvumilia tabia yake hiyo itabidi uachane naye. Lakini kabla hujachukua hatua hiyo, mwelezee kuwa tabia yake inakuudhi na umshauri ajirekebishe. Akishindwa kujirekebisha itabidi umuache na hatua yako hiyo haitamuathiri kwa sababu tayari utakuwa umemuonya mapema.

 

Sijawahi kuambia mchumba kwamba nina mtoto!

Shikamoo shangazi! Nina mchumba aliye tayari kunioa. Pili, nina mtoto na sijawahi kumwambia. Je, nimwambie?

Kupitia SMS

Hilo ni mojawapo la mambo ambayo huleta shida katika ndoa yakiwekwa siri na kufichuka baadaye. Ni muhimu umwambie ukweli ili ujue msimamo wake.