Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nina umri wa miaka 28 lakini sijapata mpenzi wa kunisisimua

March 7th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHANGAZI pokea salamu zangu. Mimi ni mwanamume mwenye umri wa miaka 28 na bado sijapata mpenzi ingawa natamani sana kuwa naye. Nimekutana na wanawake watatu ambao wamenasa moyo wangu lakini wote wamenikataa. Kwa upande mwingine, kuna wengine wengi ambao wananiandama lakini sina hisia kwao. Nifanye nini ili nipate ninayempenda?

Kupitia SMS

Ni desturi ya binadamu kutaka kilicho bora zaidi maishani, hata katika kutafuta mume au mke. Wanawake wazuri kimaumbile na kitabia hawapatikani kwa urahisi, kwa hivyo itabidi uwe na subira. Wanaokufuata wanahisi kuwa unawafaa ilhali nawe unahisi hawajafikia kiwango unachotaka. Kuwa na msimamo na subira katika kutafuta mwenzi wako maishani. Hakuna kizuri kinachopatikana kwa urahisi.

 

Mke anataka tulee mtoto wa pembeni

Shangazi natumai wewe ni mzima. Mke wangu amenizidi umri kwa miaka mingi. Huu ni mwaka wa tatu tangu nilipomuoa na bado hajanipa mtoto. Mwaka uliopita nilipendana na mwanamke wa makamo na tumezaa mtoto pamoja. Mke wangu amejua na ananiambia nichukue huyo mtoto kisha niachane na mama yake. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Kulingana nawe, mke wako ameshindwa kupata mtoto kwa sababu ya umri wake mkubwa ingawa hujasema ni miaka mingapi. Huenda hata si umri, labda ni tatizo la kiafya ambalo linaweza kutatuliwa. Lakini kwa kuwa uliamua kuzaa na mwingine, itabidi uchague kuishi na uliye naye ama kumchukua huyo mwingine kwani sidhani atakubali kunyang’anywa mtoto wake.

 

Nina mpenzi ila ni mraibu wa mihadarati na sasa amenichosha

Kwako shangazi. Ninasoma shule ya upili na nina uhusiano na kijana aliye na uraibu wa kutumia dawa za kulevya. Nimemshauri kwa muda mrefu akome lakini amekataa. Isitoshe, mimi ndiye humpa pesa kila wakati na nikikosa ananikasirikia. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Kwanza, wewe ni mwanafunzi na hufai kabisa kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi. Pili ni makosa makubwa kuchagua kuwa na uhusiano na mtu asiyejali maisha yake mwenyewe na unatarajia kwamba atajali maisha yako.Isitoshe, anatumia dawa za kulevya na umekubali akutegemee wewe kifedha. Iwapo kwa hakika unahitaji ushauri wangu, basi nakwambia uvunje mara moja uhusiano huo la sivyo utakuja kujuta.

Aliniwacha akaoa rafiki yangu, sasa anadai turudiane na mie pia nilichukuliwa

Vipi shangazi? Mwanamume niliyempenda kwa dhati aliniacha bila sababu ya maana akashikana na mwanamke rafiki yangu. Sasa mwanamke huyo amemuacha akaolewa na mwanamume mwingine. Nilishangaa sana juzi mwanamume huyo aliponipigia simu kuniambia eti nimsamehe ili turudiane. Aliponiacha nilipata mwingine na nimemwambia hivyo ila hataki kuamini. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Usemi kuwa malipo ni papa hapa duniani umethibitishwa katika kisa chako hicho. Aliyokufanyia mwanamume huyo sasa yamempata yeye mwenyewe. Ninashangaa kwamba unapokea simu kumsikiliza! Kama haamini una mpenzi, mualike mahali aje amuone ndipo aamini na aache kukusumbua.

Tumeoana miaka 3 sasa lakini mke amesisitiza kwetu hafiki hadi nitakapojenga

Kwako shangazi. Nilioa miaka mitatu iliyopita na tumejaliwa mtoto mmoja. Bado sijajenga nyumba yangu kwetu mashambani na mke wangu ameapa kuwa hataenda huko hadi nijenge. Je, hiyo ni haki?

Kupitia SMS

Hiyo ni sababu ya kutosha ya mke wako kukataa kwenda kwenu mashambani na ninamuunga mkono kikamilifu. Mwanamume akiamua kuoa ni lazima kwanza ajenge nyumba ambamo ataishi na mkewe na watoto watakaozaliwa. Ni dharau kubwa kwa mwanamume mzima aliye na mke na watoto kulala ndani ya nyumba ya wazazi wake. Kama unajiheshimu, mjengee nyumba mke wako.