Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nina ushahidi mke wa jirani anagawa asali ajabu

October 28th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Kuna mwanamke jirani yangu ambaye ameolewa lakini anagawa asali kwa wanaume wengine. Nina ushahidi wa kutosha kuhusu uhusiano wa pembeni kati yake na mwanamume mwingine lakini naogopa kumwambia mume wake kwa sababu anamwamini sana na ninajua kuwa nikimwambia hataamini. Waonaje?

Kupitia SMS

Kwa kawaida, mimi huwa siungi mkono mapenzi ya pembeni hasa kwa watu walio katika ndoa, lakini pia sitakushauri ujiingize katika mambo yasiyokuhusu. Huyo si mke wako na hata akiwa na wapenzi chungu nzima wa pembeni hilo halikuhusu ndewe wala sikio. Isitoshe, unasema kuwa mume wake anamwamini kwa hivyo huenda ukamwambia yakakugeukia wewe. Kama mumewe hajui ni sawa, akigundua, hiyo itakuwa kati yao.

 

Nipo shuleni na kijana fulani ananiandama

Vipi shangazi? Niko katika mwaka wa tatu shule ya upili. Kuna kijana ambaye amekuwa akiniandama akitaka tuwe wapenzi lakini mimi sitaki kwa sababu niliwaahidi wazazi wangu sitajiingiza kwa mambo kama hayo nikiwa shuleni. Nishauri.

Kupitia SMS

Usikubali kabisa kuvunja ahadi yako kwa wazazi wako. Uamuzi wako ni wa maana sana kwa sababu masomo yako ndiyo muhimu zaidi kwa sasa. Mpuuze na kumuepuka kijana huyo kwa vyovyote vile hadi umalize masomo yako. Akiona kwamba huna shughuli naye ataachana nawe.

 

Amenipa mimba na sasa asema niitoe

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 29 na kuna mwanamume ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka mitano. Mwanamume huyo amenipa mimba na nilipomwambia aliniambia nitoe ama nikubali kuwa mke wa pili. Nimeshangaa sana kwa sababu kwa muda wote ambao tumekuwa pamoja hajawahi kuniambia kuwa ana mke. Nimechanganyikiwa, sijui nitafanya nini?

Kupitia SMS

Hayo ndiyo matokeo ya kuweka raha mbele na ndoa nyuma katika uhusiano wa kimapenzi. Jamii ya kisasa imejaa walaghai wa kimapenzi ambao kazi yao ni kuwatumia na kuwatema wenzao. Uhusiano wa kimapenzi kamwe si kibali cha ndoa. Ndiyo maana nimeshikilia msimamo kwamba wapenzi wanafaa kusubiri hadi ndoa la sivyo watumie kinga ili kuepuka magonjwa na mimba. Kutoa mimba ni hatia. Chagua kati ya kumlea mtoto wako peke yako ama kuolewa mke wa pili.

 

Amevunja ahadi nzito na hili laniuma sana

Kwako shangazi. Kuna msichana tuliyependana sana tukisoma pamoja chuo kikuu na alikuwa ameniahidi kuwa tutaoana tukimaliza masomo. Huu ni mwaka wa pili tangu tumalize na nimemtafuta bila kufaulu kwani nikimpigia simu ama kumtumia SMS hajibu. Hatimaye nimegundua kuwa tayari ameolewa. Nampenda kwa dhati na nahisi amenikosea sana. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Sasa umejua ni kwa nini msichana huyo amekuwa akipuuza simu zako. Alipata mwingine na akakubali kuwa mke wake. Ukweli ni kwamba huna nafasi tena katika moyo wake na itabidi umsahau licha ya mapenzi uliyo nayo kwake.

 

Kipusa mrembo ila ni wazi uhusiano wetu hautaenda popote

Shangazi ni matumaini yangu kuwa wewe ni mzima. Nina mpenzi wangu ambaye ni mrembo sana lakini sidhani uhusiano wetu utaenda mbali. Sababu ni kwamba ni mjeuri kwangu na pia ananidharau. Kuna siku ambayo nilimpata akimpakulia asali rafiki yangu na nikanyamaza. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Haina haja kwako kuendelea na uhusiano unaokuletea mateso na mahangaiko moyoni kutokana na tabia za mpenzi wako. Kama mwanamke huyo anakudharau mkiwa wapenzi, itakuwaje atakapokuwa mke wako? Isitoshe, umethibitisha kuwa si mwaminifu kwako. Hayo kamwe si mapenzi, ni balaa. Tafuta namna ya kumuepuka, utafute mwingine.