Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nina virusi ilhali yeye hana, naogopa kumpa tunda!

November 26th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi kwa miaka miwili na mwanamume ninayempenda sana. Hata hivyo, nina Ukimwi na hali hiyo imenifanya nimnyime tunda nisije nikamuambukiza. Nimeshindwa kumwelezea hali yangu hiyo kwa sababu nampenda sana na sitaki aniache. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Inaonekana mapenzi mazito uliyo nayo kwa mwanamume huyo yamekufumba macho hivi kwamba huwezi kuona athari za kumficha hali yako. Sijui umepanga kuweka siri hiyo hadi lini kwa sababu uhusiano wenu hatimaye utaishia katika ndoa na itabidi umpe haki yake ya ndoa. Ni heri umwambie ukweli mapema ili afanye uamuzi unaofaa.

 

Ataka kunioa lakini nahofia mke wake waliyeachana

Vipi shangazi? Kuna mwanamume tuliyekutana katika hafla fulani na tukapendana. Nilimpa nambari yangu ya simu na tumekuwa tukiwasiliana. Ameniambia kwamba alikuwa na mke lakini wakaachana. Hakika ananipenda na hata yuko tayari kunioa. Hofu yangu ni kuwa atanioa kisha mke wake arudi baadaye. Naomba ushauri wako tafadhali.

Kupitia SMS

Uamuzi wa mwanamume huyo kuoa tena ni ishara kuwa hana mpango wa kurudiana na mke wake na ameamua kuendelea na maisha yake. Hata hivyo, ni muhimu uzungumze naye umwelezee hofu yako hiyo ili akupe hakikisho kwamba mkewe waliyeachana hatarudi kuvuruga maisha yenu.

 

Nilimkosea mpenzi akanyakuliwa ila bado namhitaji anirudie

Hujambo shangazi? Kuna msichana tuliyekuwa wapenzi tukiwa mwaka wa kwanza wa chuo kikuu. Nilimpenda kwa moyo wangu wote lakini baadaye nilimkosea na tukaachana. Muda si mrefu alishikana na mwanamume mwingine. Bado nampenda na namhitaji sana maishani mwangu. Nitafanya nini ili nimpate?

Kupitia SMS

Umechukua muda mrefu kuamua kumrudia msichana huyo. Kama kweli unampenda, ungemuomba msamaha wakati ulipomkosea. Inaonekana ulichelea kufanya hivyo na kwa njia hiyo ukampa nafasi ya kumkaribisha mwingine maishani mwake. Hata hivyo unaweza kujaribu bahati yako. Mtafute umwelezee nia yako ili ujue msimamo wake.

 

Nina haki ya kudai mwanangu aliyeenda na mpenzi wangu?

Shangazi pokea salamu zangu. Natumai wewe u mzima. Nina jambo ambalo linahitaji ushauri wako. Nilizaa mtoto na msichana tuliyekuwa wapenzi lakini tukaachana. Hatimaye aliolewa na mwanamume mwingine. Je, nina haki ya kudai mtoto wangu?

Kupitia SMS

La, hasha! Huyo sasa ni mtoto wa wenyewe ingawa ulimzaa wewe. Kumbuka kuwa ulipomzaa mama yake alikuwa mpenzi wako tu wala si mke wako. Hatimaye uliachana naye na akaolewa na mwanamume mwingine akiwa na mtoto huyo. Sasa yeye na mtoto ni mali ya mwanamume huyo.

 

Mawasiliano na demu wangu yamekatika

Shikamoo shangazi. Nina umri wa miaka 20 naye mpenzi wangu ana miaka 23. Alinizungumzia vibaya majuzi nikakasirika na tangu hapo tumenyamaziana, akinipigia simu napuuza naye pia nikimpigia hajibu. Sasa amenifungia kuwasiliana naye kupitia kwa mtandao. Nifanyeje?

ROZZIE

Kulingana na maelezo yako, wewe ndiye uliyeanza vita hivyo baridi dhidi ya mwenzako naye ameamua kulipiza kisasi. Inaonekana pia uko tayari kusuluhisha jambo hilo lakini hutaki kumuonyesha wazi. Si vyema kuruhusu tofauti ndogo kuharibu uhusiano wenu. Mtafute mwenzako mzungumze ana kwa ana ili kumaliza ugomvi huo.

 

Mke wangu ana mpango wa kando

Hujambo shangazi? Nimeoa kwa mwaka mzima sasa. Nimeshangaa sana kugundua kuwa mke wangu ana mpango wa kando na amekuwa akimtembelea ninapokuwa kazini ilhali hakuna kitu anachokosa kwangu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Huo ni usaliti mkubwa wa kimapenzi hasa kutoka kwa mtu unayemuita mke wako. Hata kama kuna chochote ambacho amekosa kutoka kwako anafaa kukuelezea kwa sasa wewe ndiye mumewe. Tabia yake hiyo ni hatari kwa ndoa na ni sababu ya kutosha kuachana naye. Hata hivyo wewe ndiye mwenye uamuzi wa mwisho kuhusu jambo hilo.