Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Ninampenda ajabu lakini naye amezidi kwa wivu

April 18th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nimekuwa na mpenzi kwa mwaka mmoja sasa. Kusema kweli, ninampenda kwa dhati mwanamume huyo na ninaweza kufanya chochote ili kudumisha uhusiano wetu. Tatizo pekee ni kuwa mwenzangu ana wivu kupita kiasi. Kila nikipigiwa simu hata na wasichana marafiki zangu yeye hudhani ni wanaume. Tumekosana mara nyingi kuhusu jambo hilo. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Maisha ambayo mpenzi wako anataka uishi hayawezekani. Wewe ni binadamu na una haki ya kuwa na marafiki wa kike na wa kiume pia. Kama kweli mwanamume huyo anakupenda na anakuamini, hafai kukuwekea masharti kama hayo. Ninaamini yeye mwenyewe ana marafiki na huwa wanampigia simu. Ukihisi imekuwa vigumu kumvumilia unaweza kumuondokea.

 

Nimechumbiwa na aliyefiwa na mkewe, lakini ushauri wa marafiki wanikwaza

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 29 na nimependana na mwanamume mwenye umri wa miaka 42 ambaye alikuwa ameoa lakini mke wake akafariki muda mfupi baada yao kufunga ndoa. Yuko tayari kunioa lakini marafiki zangu wameanza kunisema eti ninaolewa mke wa pili. Hiyo ni kweli?

Kupitia SMS

Ukisikiza uzushi wa marafiki utapotea. Wewe ni mtu mzima na una uwezo wa kuamua mambo muhimu kuhusu maisha yako. Iwapo mwanamume huyo alikuwa ameoa na mkewe akafariki, akikuoa utakuwa mkewe wa pekee wala si mke wa pili. Hao wako si marafiki, ni mahasidi, wapuuze.

 

Nimebana chungu cha asali sasa sipati  wa penzi la dhati

Hujambo shangazi? Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 30 na nimeshindwa kudumisha uhusiano wa kimapenzi na wanaume. Kila ninayekutana naye hutaka tushiriki mapenzi na nikikataa anatoweka. Kwangu mimi tendo hilo ni halali tu katika ndoa na nimeamua sitawahi kushiriki kabla. Nishauri.

Kupitia SMS

Msimamo wako huo ni sawa kabisa na inafaa kuwa hivyo ingawa hivyo sivyo ilivyo kwa watu wengi. Mwanamume anayekupenda kwa dhati hawezi kukuacha kwa sababu ya jambo hilo. Mara nyingi wanaume wanaoweka mbele tendo hilo huwa wanaongozwa na tamaa tu wala si mapenzi. Usitie shaka, siku moja mwanamume wa ndoto zako atafika.


Alinizuzua sana ila sasa simu hapokei na SMS hazijibu!

Vipi shangazi? Kuna mwanamke ambaye tumekuwa wapenzi kwa mwezi mmoja pekee na amenipumbaza kwa penzi lake. Hata hivyo, sijamuona kwa wiki moja sasa na nikimpigia hapokei wala SMS hajibu. Nina wasiwasi sana kwani ninampenda kuliko nafsi yangu na sitaki kumpoteza. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Inaonekana kuwa mwanamke huyo ameamua kuvunja uhusiano wenu ghafla kutokana na sababu zake mwenyewe. Sababu yake kupuuza simu zako ni kuwa hataki maswali mengi. Huo ndio ukweli na itabidi uukubali badala kuhangaika bure ilhali yeye anaendelea na maisha yake. Huenda hata tayari amepata mwingine.

 

Nilimtoroka baada ya kumpachika mimba, nataka kumuona lakini nimejaa aibu

Kwako shangazi. Nilimuacha mpenzi wangu baada ya kumpa mimba kwa sababu sikuwa na uwezo wa kugharamia malezi ya mtoto. Hatimaye alijifungua akiwa kwao na sasa mtoto huyo ana miaka miwli. Namtamani sana kumuona mtoto huyo lakini naona aibu kwa sababu sina mchango wowote katika maisha yake. Nishauri.

Kupitia SMS

Ulipanda mbegu kisha ukatoweka wala hukujali itanyunyiziwa maji wala kupaliliwa na nani. Sasa unaona mazao yake mazuri unatamani kuvuna. Huna hata aibu mwanamume wewe! Ulimtoroka mtoto huyo akiwa tumboni, hukujali iwapo atazaliwa akiwa hai au maiti. Kwa sababu hiyo, huna haki yoyote juu yake. Thubutu kukanyaga kwao uone kama hutachinjwa kama mbuzi.