Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Ninaona ana mpango wa kunivurugia mapenzi

May 22nd, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nimekuwa na mpenzi kwa miaka mitano na tunapendana sana. Kuna jamaa mwingine ambaye amekuwa akinitaka lakini mimi simtaki. Juzi alinitumia SMS ya kimapenzi iliyoonyesha kana kwamba sisi ni wapenzi. Anaona vibaya kwa sababu nimemkataa na nina hakika anataka kuniharibia. Mpenzi wangu aliona ujumbe huo na amenikasirikia sana hataki hata kuzungumza nami. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni kweli kwamba mwanamume huyo ameamua kukuharibia uhusiano wako baada ya kumkataa. Hata hivyo, usikubali kumpa nafasi hiyo. Mwelezee ukweli mpenzi wako kwamba umemkataa mwanamume huyo na anataka tu kuwaharibia uhusiano wenu. Bila shaka ataelewa kwa sababu hana ushahidi kwamba una uhusiano na mwanaume huyo.

 

Kumbe tapeli wa mapenzi, nifanyeje?

Kwako shangazi. Juzi nilikagua simu ya mwanamume mpenzi wangu na nikapata jumbe nyingi za kimapenzi kutoka kwa wanawake tofauti. Nilipomuuliza aliungama kuwa hao ni wapenzi wake na akaniambia tuvunje uhusiano wetu tuwe marafiki tu. Ninaumwa sana moyoni nahisi sitaweza kuishi tena kwani sidhani nitawahi kumpenda mwanaume mwingine kama ninavyompenda huyo. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Umejua ukweli kuwa mwanaume huyo ni tapeli wa kimapenzi na hata yeye mwenyewe amekiri hilo. Ni bahati kwamba ulipata fursa ya kukagua simu yake la sivyo ungeendelea kuwa mmoja wa wapenzi wake wengi. Nashangaa kwamba bado unahangaika moyoni kwa mtu kama huyo eti huwezi kuishi bila yeye badala kumshukuru Mungu kwamba amekuepusha naye na sasa una nafasi nyingine ya kutafuta mwanamume anayekufaa.

 

Amenirudia na amekataa kupimwa

Vipi shangazi? Mpenzi wangu aliniacha akaolewa na mwanaume mwingine. Muda si mrefu aligundua kuwa mwanamume huyo tayari alikuwa ameoa na akamuacha. Alinipigia simu kuniomba msamaha turudiane na nikakubali kwa sababu bado ninampenda. Sasa yuko kwangu na nimemwambia ni lazima kwanza tukapimwe lakini amekataa. Nishauri.

Kupitia SMS

Mwanamke huyo ana bahati sana kama umekubali arudi kwako licha ya kwamba alikuacha akaolewa na mwanamume mwingine. Kwa sababu ndiye aliyeomba kurudi kwako, anafaa kukubali masharti unayompa. Ukweli ni kuwa amekuwa mke wa mtu na ni muhimu sana mpimwe kwanza ili muwe na hakika kuhusu hali yenu ya afya kabla ya kuanza maisha ya ndoa pamoja. Kama hataki usimbembeleze. Mwambie afunge virago arudi alikotoka.

 

Naogopa akijua si bikira ataniacha

Hujambo shangazi? Nina mpenzi anayenipenda nami pia nampenda sana. Hatujawahi kuonja asali na amekuwa akiniambia atanioa tu kama mimi ni bikira. Ninajua mimi si bikira lakini naogopa kumwambia asiniache. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Kama mpenzi wako amekuambia amepanga kuoa mwanamke bikira, huna budi kumwambia ukweli kwamba wewe si bikira. Haina haja usubiri akuoe kisha agundue kuwa ulihadaa na akuteme. Utakuwa umepoteza wakati wako na wake pia. Akijua ukweli sasa labda anaweza kubadili msimamo wake huo.

Ageuka hayawani na kutafuna mpwake

Shangazi nahitaji ushauri wako. Mume wangu amenikosea sana, sijui nitafanya nini. Tumekuwa tukiishi na binti ya dada yangu tangu akiwa na miaka mitatu na sasa ana miaka 12. Nilishtuka juzi aliponiambia kuwa kila nikitoka mume wangu humdhulumu kimapenzi kisha anamuonya asimwambie mtu yeyote akitishia kumwua. Mimi nimeokoka na kitendo cha mume wangu kimeniumiza vibaya moyoni hata simwamini tena. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Mume wako sasa amegeuka hayawani kama anamtendea hivyo mtoto wa dada yako ambaye ni sawa na wake tu. Huo ni uhalifu wa hali ya juu na akishtakiwa anaweza kufungwa jela maisha. Utaamua iwapo utaripoti kisa hicho kwa polisi akamatwe na kushtakiwa ama utanyamaza tu ili kumuepushia aibu kisha ujiondoe katika ndoa hiyo.