Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Ninashuku anamgawia mpenziwe wa zamani

October 19th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nina mpenzi na huu ndio mwaka wa pili wa uhusiano wetu. Nimekuwa nikimuona na vitu vya bei ghali, yakiwemo mavazi na vifaa vya nyumbani na kushangaa kwa sababu ninajua mshahara anaopata hauwezi kugharimia vitu kama hivyo. Nililazimika kumuuliza na akaniambia mwanamume aliyekuwa mpenzi wake bado ni rafiki na amekuwa akimpa zawadi. Lakini siamini kwani nimechunguza na kugundua kuwa mwanamume huyo ana mke na ninashuku kuwa yeye na mpenzi wangu wana uhusiano wa pembeni. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Mpenzi wako amekuhadaa. Kama umethibitisha kuwa mpenzi wake wa awali ni mwanamume aliye na familia, basi umechezewa. Nahisi kuwa ilifika wakati mpenzi wako akaamua kwamba anahitaji uhusiano wenye matumaini ya ndoa na ndiyo maana alikubali kuwa wako. Lakini hajaachana na mwanamume huyo na ndiyo maana amekuwa akimnunulia zawadi hizo za bei ghali. Madai yake eti bado ni marafiki yananuiwa kukufunga macho tu. Hata kama si wapenzi, ni makosa kwake kupokea zawadi kutoka kwa mwanamume aliyekuwa mpenzi wake ilhali ameshapata mwingine. Kama amejitolea kuwa mwenzako maishani, basi mwambie avunje kabisa uhusiano wake na mume wa mwenyewe.

 

Tumeongea kwenye Facebook na naamini mambo yako shwari

Shikamoo shangazi! Nimekuwa nikitafuta mpenzi na hatimaye ninaamini nimempata. Kuna mrembo ambaye tumejuana kupitia kwa ‘Facebook’ na tumependana hata yuko tayari nimuoe. Ameniahidi kuwa hivi karibuni tutapanga tukutane ili tuzungumze zaidi. Je, inawezekana kwamba ananihadaa?

Kupitia SMS

Mahusiano ya kupitia kwa mtandao na simu hayawezi kuaminika. Ninashangaa ukisema kwamba mwanamke huyo amekubali umuoe ilhali hamjakutana. Umeona picha yake tu kwenye mtandao. Utajua kwa hakika umepata mpenzi mtakapokutana, muongee kisha mkubaliane. Siwezi kujua kama anakuhadaa au la. Kama ameahidi kuwa mtakutana, subiri uone iwapo atatimiza ahadi yake.

 

Umri wangu miaka 27 na nammezea mama wa umri wa miaka 39

Shangazi natumai wewe ni mzima. Nina umri wa miaka 27 na nimependana na mwanamke mwenye umri wa miaka 39. Alikuwa ameolewa lakini akaachana na mume wake na akarudi kwao na watoto wao watatu. Huyo aliyekuwa mume wake ameoa mwanamke mwingine. Je, nitakosea kumuoa?

Kupitia SMS

Kama umempenda mwanamke huyo na umetosheka kuwa anakufaa kama mke wako, hiyo ni sawa kabisa. Ninaamini kuwa uko tayari kuwakubali na kuwalea watoto wake kama wako. Iwapo wasiwasi wako ni kwamba alikuwa mke wa mtu, jambo hilo halifai kuwa kikwazo kwa sababu tayari aliyekuwa mume wake ameoa mwanamke mwingine. Hiyo ina maana kwamba amekata kauli kuwa ndoa yao imefikia kikomo.

 

Penzi limechipuza kati yangu na dada ya mke, nifanyeje?

Habari yako shangazi. Nina mke na tuna mtoto mmoja. Kuna dada yake mdogo ambaye tumekuwa tukiishi naye na hatimaye tumekuwa wapenzi. Kusema kweli ninampenda hata kushinda mke wangu na natamani sana kama ningemuoa yeye. Mapenzi kati yetu yamenoga sana na nahofia muda si mrefu mke wangu atagundua. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hayo unayoita mapenzi kati yako na dada ya mke wako ni upuuzi mtupu. Huyo ni mdogo wa mke wako kwa hivyo umemzuzua akili tu, si kwamba anakupenda. Ukweli ni kwamba unaongozwa na tamaa na ndiyo maana umeshindwa kujizuia mbele yake. Kama una akili, basi nakwambia uvunje mara moja uhusiano huo uhakikishe dada ya mke wako ametoka nyumbani kwenu. Usipofanya hivyo, mke wako hatimaye atagundua mchezo wenu na itakuwa balaa kwenu wawili.

 

Mke aninyima asali

Hujambo shangazi? Nina mke ninayempenda lakini huninyima haki yangu ya ndoa. Nisaidie.

Kupitia SMS

Ni makosa kwa mkeo kukunyima unyumba kwa sababu kama mume wake una haki ya tendo hilo. Jaribu kuzungumza naye ikishindikana muite wazee.