Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nitaishi vipi na mke na mie hujikojolea kitandani?

October 30th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Nina umri wa miaka 30 na nimekuwa na mchumba kwa miaka mitatu. Tumepanga kufunga ndoa hivi karibuni lakini kuna jambo linalonisumbua. Nina tatizo la kukojoa kitandani nikiwa nimelala usiku. Ajabu ni kwamba hali hiyo imenipata miaka miwili tu iliyopita na nimeiweka kuwa siri yangu nikidhani kuwa itamalizika lakini bado. Kusema kweli itakuwa changamoto kubwa kuishi na mke nikiwa na hali hiyo. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ni mkosi mkubwa kwamba umepatikana na hali hiyo wakati ambao umeamua kupiga mojawapo ya hatua muhimu zaidi katika masiha yako. Ninaamini kuwa hali yako hiyo imetokana na hitilafu fulani ndani ya mwili wako na inaweza kushughulikiwa kimatibabu. Nenda hospitalini ili uone iwapo inaweza kushughulikiwa kabla ya wewe kufunga ndoa.

 

Niko shule ya upili na nina mpenzi, ingawa mimi nataka kusoma yeye hataki kuniacha

Shikamoo shangazi! Mimi ni mwanafunzi wa shule ya upili. Nina uhusiano na kijana fulani na sijui nitafanya nini kwa sababu nimemwambia tuachane lakini amekataa. Mimi ninataka kusoma kwanza. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Uliingia mwenyewe katika uhusiano huo wala hukulazimishwa. Pili, huo ni uhusiano haramu kwa sababu wewe ni mtoto wa shule. Kama umegundua kuwa ulifanya makosa, una haki ya kujiondoa wala huhitaji idhini ya mtu yeyote yule. Sielewi unamaanisha nini ukisema kuwa unataka kuacha lakini mpenzi wako amekataa. Mwelezee wazi kuhusu uamuzi wako huo kisha ujitenge naye na kukatiza mawasiliano kati yenu.

 

Ameninyima asali sasa nimeamua kutafuta mwingine, kuna makosa?

Hujambo shangazi? Msichana ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka miwili amenikataza kulamba peremende. Nimeamua kumuacha nitafute mwingine. Nishauri.

Kupitia SMS

Uamuzi wako huo unaonyesha kuwa lengo lako kuu katika uhusiano ni hiyo peremende. Lakini unafaa kujua kuwa hiyo peremende si haki yako na haipatikani kwa urahisi kama inayonunuliwa dukani. Kuwa tayari kuvunja mahusiano zaidi ukiitafuta.

 

Amenipunguzia uhondo chumbani sasa nashuku ana wa pembeni

Vipi shangazi? Tafadhali nahitaji ushauri wako. Ninashuku kuwa mwanamume mpenzi wangu ana mpango wa kando. Sababu ni kuwa kazi yake chumbani imepungua sana ikilinganishwa na hapo awali. Wakati huo alikuwa akinipa dozi hadi mimi mwenyewe namwambia ni basi! Lakini siku hizi anaonja tu na kuniacha hoi nikidondokwa na mate. Nikimuuliza husema yeye pia hajui shida ni nini. Naumia sana lakini nafsi yangu hainiruhusu kutembea ovyo na wanaume. Nisaidie.

Kupitia SMS

Hujaelezea sababu yako ya kushuku kuwa mpenzi wako ana mwingine wa pembeni. Kama umeona dalili za kutosha, itakuwa vyema uchunguze mienendo yake ndipo uweze kuthibitisha na kuchukua hatua inayofaa. Kama hana uhusiano na mwanamke mwingine, inawezekana kwamba hali hiyo inatokana na mabadiliko fulani ndani ya mwili wake ambayo yanaathiri uwezo wake na anaweza kutafuta msaada hospitalini.

 

Mpenzi ana kila kitu nilichokitamani, kasoro ni moja tu, amejaa hasira

Kwako shangazi. Nina mpenzi ambaye amekamilika kwa hali zote lakini kasoro yake ni moja pekee. Tukikosana kidogo tu, anaweza kukaa hata mwezi mzima bila kuongea nami. Ninalazimika kutumia wakati mwingi kumbembeleza ili kurekebisha mambo. Ingawa nampenda hasira hizo zake pia zinanitia baridi. Nishauri.

Kupitia SMS

Hali ya mwenzako ni ushahidi wa kutosha kwamba hakuna binadamu aliye mkamilifu. Hata wewe ambaye unamlaumu kwa kasoro yake hiyo una upungufu wako. Inatarajiwa kwamba mtu akimpenda mwenzake anafaa kumkubali pamoja na kasoro zake bora tu awe anaweza kumvumilia kwa lengo la kudumisha uhusiano. Jinsi pekee ya kukabiliana na hali hiyo ni kujaribu uwezavyo kuepuka kumkosea mwenzako.