Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nitapata wapi mwanamke mwenye penzi la dhati?

September 11th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nina umri wa miaka 35 na sijapata mpenzi; bado ninatafuta. Hata hivyo, nina wasiwasi kuhusu iwapo nitampata mpenzi wa dhati kwani siku hizi si rahisi kumpata mwenye mapenzi ya dhati. Wanawake wengi wanafuata pesa tu. Nishauri.

Kupitia SMS

Nakubaliana nawe kuwa mapenzi ya dhati yameadimika katika enzi tunazoishi kutokana na tamaa ya pesa. Si wanawake pekee bali pia kuna wanaume wanaonyemelea wanawake matajiri kwa mapenzi bandia huku shabaha yao ikiwa pesa. Hata hivyo, wapo wachache wanaoheshimu nafsi zao na ambao wanatafuta mapenzi ya dhati. Ni juu yako kuwa makini sana unapotafuta usije ukatumbukia mikononi mwa tapeli.

 

Rafiki ataka kunioa

Vipi shangazi? Nina umri wa miaka 24 na bado sijapata mpenzi, lakini nina rafiki ambaye ananiambia atanioa na ananipenda sana kila kitu ninachotaka ananipa. Hata hivyo, nahisi siko tayari kwake ingawa siwezi kuelezea sababu. Nishauri.

Kupitia SMS

Hujui bahati uliyonayo kupata mtu ambaye unajua kwa hakika kwamba anakupenda kwa dhati. Kuna wengi wanaotamani kupata kama huyo na nakuonya kuwa ukichelewachelea atanyakwa na mwingine uachwe ukijuta. Shauri yako.

 

Mke ameolewa na mpango wa kando

Shikamoo shangazi! Nilikosana na mke wangu nilipogundua alikuwa na mpango wa kando. Hatimaye aliolewa na mwanamume huyo na sasa wamenikataza kumuona mtoto tuliyezaa pamoja. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Kama wewe ndiye baba mzazi wa mtoto huyo, basi una haki kwake na hakuna anayefaa kukataza kumuona. Kama unaona hamtaweza kusuluhisha wenyewe mvutano huo, tafuta suluhisho la kisheria kupitia kortini.

 

Nimeamua kuishi naye kama mume

Kwako shangazi. Nimekuwa na mpenzi kwa miaka miwili na tayari nimemjulisha kwa wazazi wangu. Amekuwa akiwasaidia wazazi kwa pesa ingawa hajanioa rasmi. Sasa nimeamua kuishi kwake ingawa sijawaambia wazazi. Je, nimefanya makosa?

Kupitia SMS

Hali kwamba wazazi wako walimkubali na huwa wanapokea pesa kutoka kwake ni ishara kuwa wamekubali na kuidhinisha uhusiano wenu. Unachofaa kufanya ni kuwafahamisha umeamua kuhamia kwake kuishi naye.

 

Nataka kuramba asali

Kwako shangazi. Kuna msichana ambaye nampenda sana na nimeamua kuonja asali. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Sijui ni kwa nini unaomba ushauri wangu ilhali unasema tayari umeamua. Isitoshe, asali unayosema unataka kulamba ina mwenyewe na utaweza kuipata kupitia kwake iwapo utamwelezea na aridhike kwamba unastahili.

 

Nina mimba ya yule tuliyeachana

Kwako shangazi. Niliachana na mpenzi wangu miezi miwili iliyopita na muda si mrefu nikapata mwingine. Sasa nimegundua nina mimba ya huyo tuliyeachana na nahofia kumwambia niliye naye kwani sijui atafanya uamuzi gani. Nishauri.

Kupitia SMS

Mimba si ugonjwa unaoweza kutibiwa na kutoweka, kwa hivyo hata usipomwambia hatimaye atajua tu. Ushauri wangu ni kwamba umwambie ukweli mapema ili afanye uamuzi wowote ambao atahisi unafaa. Ni heri umwambie badala ya kusubiri ajue mwenyewe baadaye.

 

Nina mke mzushi sasa atishia kuniua

Kwako shangazi. Nimekuwa na mke kwa miaka mitano sasa na tumepata mtoto mmoja. Mke wangu anapenda sana ugomvi na amekuwa vita nyumbani mara kwa mara bila sababu ya maana. Juzi tuligombana na kwa mara ya kwanza akanitishia maisha kwa kuniambia wazi kuwa siku moja ataniua. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Kuna usemi kuwa ndoa ni kuvumiliana. Hata hivyo, kuna kiwango ambacho mwenzako anaweza kufika akawa hawezi kuvumilika tena na nahisi kuwa hapo ndipo ndoa yenu imefika. Kama mke wako amekuonya wazi kuwa siku moja atakuua, hufai kusubiri hadi atekeleze mpango wake huo. Ningekuwa wewe ningejiondoa katika ndoa hiyo.