Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Rafiki ananiambia nimuache mpenzi ila sijui sababu

October 2nd, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka 25 na nina mpenzi ninayempenda sana. Hata hivyo, kuna rafiki yangu ambaye amekuwa akiniambia nimuache msichana huyo lakini hanipi sababu ya maana. Nashuku kuwa anamtaka kwa hivyo ni yake ni kututenganisha kisha amnyakue. Nishauri.

Kupitia SMS

Kuna watu wasiowatakia wenzao mema na inaonekana rafiki yako ni mmoja wao. Huenda ni kweli anammezea mate mpenzi wako na anataka umuache ili apate nafasi ya kumtongoza. Jambo la kufanya ni kumpuuza. Hatimaye atagundua kuwa uhusiano wenu ni imara na atakoma kujipenyeza.

 

Anasema picha ya msichana niliyoona ni rafiki yake tu

Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 21 na nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamume ambaye nimempenda kwa moyo wangu wote. Hata hivyo tulikosana hivi majuzi nilipopata picha ya msichana mwingine katika simu yake. Nilipomuuliza alidai eti ni rafiki yake. Sijaamini madai yake hayo lakini bado nampenda. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Kuna uwezekano kuwa mpenzi wako ana uhusiano wa pembeni na msichana huyo. Hata hivyo, picha uliyoona katika simu yake si ushahidi wa kutosha wa jambo hilo na huenda pia ikawa ni marafiki kama alivyokwambia. Kwa sababu hiyo itabidi umwamini kwa sasa hadi utakapopata ushahidi wa kutosha kuwa ni wapenzi ndipo uweze kuchukua hatua inayofaa.

 

Simtaki mwanamke huyu lakini hasikii

Vipi shangazi? Kuna mwanamke ambaye ananipenda lakini mimi simpendi. Nimemwambia hivyo mara kadhaa lakini bado anaendelea kunisumbua kwa kunipigia simu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Mapenzi ni hiari, hayalazimishwi. Kama umemwambia humtaki na hasikii, unaweza kumuepuka kwa kumzima katika simu yako ili asiweze kukupigia ama ubadilishe nambari yako.

 

Ninashuku nambari zilizo katika simu yake ni za wapenzi wake

Kwako shangazi. Nimekuwa na uhusiano na mwanamume fulani kwa miaka miwili. Ninampenda sana lakini juzi nilipata nambari za simu za wanawake wengine kwenye simu yake. Nilimuuliza lakini hakunipa jibu la kuridhisha. Ninashuku kuwa hao wapenzi wake. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hujaelezea jibu alilokupa mpenzi wako kuhusu wanawake hao ambalo unasema halikukuridhisha. Inawezekana kwamba hao ni marafiki zake tu wala si wapenzi wake. Hata hivyo, kama moyo wako unakuonyesha kuwa mwenzako si mwaminifu ni heri ukatize uhusiano huo badala ya kuishi na dukuduku.

 

Nimegundua kipusa mpenzi wangu anao wanaume wengi mno

Vipi shangazi? Nimekuwa na mpenzi kwa miaka miwili sasa lakini nimegundua kuwa msichana huyo ana wapenzi wengine kadhaa. Nampenda lakini sitaki kuwa na uhusiano na mwanamke asiye mwaminifu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kama huwezi kumvumilia mpenzi asiye mwaminifu kwako, basi unajua la kufanya na sielewi ni kwa nini unahitaji ushauri wangu. Mteme utafute mwingine. Na iwapo hujali tabia yake hiyo, basi kubali kuwa mmojawapo wa wapenzi wake wengi.

 

Mume wangu anadai eti kifungua mimba wetu si mtoto wake

Hujambo shangazi? Mimi niliolewa kwa harusi na nimejaliwa watoto wawili. Ajabu ni kwamba mume wangu anadai eti mtoto wangu wa kwanza, ambaye ni wa kiume, si wake na sasa anataka nimpeleke kwa mama yangu aishi naye. Sijui mawazo yake hayo yametokana na nini ilhali mimi nina hakika kuwa huyo ni mtoto wake. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ni jambo la kushangaza kwamba mume wako anashuku kuwa wewe si mwaminifu kwake na kwamba ulimpata mtoto wenu wa kwanza kutokana na uhusiano wa pembeni. Kuna jinsi moja tu mnayoweza kutumia ili kujua ukweli wa jambo hilo. Kwa kuwa ndiye anayekushuku, mwambie afanye mpango mwende hospitalini mkapimwe ili kujua iwapo kweli mwana ni wake au la.