Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Rafiki ya mpenzi ataka kuniona chemba

April 27th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nina umri wa miaka 20 na nina mpenzi ninayempenda kwa dhati. Kuna rafiki yake ambaye nilimpa namba yangu ya simu baada ya kunisumbua kwa muda akiitaka. Sasa juzi alinipigia simu akitaka tukutane mahali faraghani eti kuna kitu anataka kuniambia. Ni rafiki mkubwa wa mpenzi wangu, lakini ninashuku nia yake kwangu. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni wazi kuwa huyo rafiki wa mume wako anakutaka na ndiyo maana anasisitiza mkutane faraghani. Hakuna jambo lingine ambalo hawezi kukwambia hata mkikutana barabarani. Mwepuke kabisa.

 

Naota vioja kumhusu

Kwako shangazi. Nina mwanamume mpenzi wangu ambaye nampenda kwa moyo wangu wote, lakini siku za hivi majuzi nimekuwa nikiota akiwa na uhusiano wa pembeni na nimeingiwa na wasiwasi. Nishauri.

Kupitia SMS

Huwezi kutumia ndoto kama ushahidi kwamba mwenzako anakudanganya. Labda unaota ndoto za aina hiyo kwa sababu unampenda sana mwenzako na hungependa kumpoteza kwa mwanamke mwingine. Ondoa wasiwasi.

 

Nikimwambia haelewi

Kwako shangazi. Kuna msichana fulani ambaye nimempenda lakini nikimueleza haelewi. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Badala ya kunichanganya akili, ni heri ukubali ukweli kuwa msichana huyo anajua unamtaka lakini yeye hakutaki. Kwa nini uendelee kung’ang’ana? Achana naye utafute mwingine.

 

Nimekwama kwake

Kwako shangazi. Kuna mwanamume tunayependana sana ingawa ana wake wengine wawili na watoto sita. Kwa sasa anaishi na mke wa pili na hayuko tayari kuniacha. Nishauri.

Kupitia SMS

Sielewi ni kwa nini unataka kukwama kwa mwanamume ambaye tayari ana wake wawili kama kwamba wanaume wameisha ulimwenguni. Pili, uamuzi wa kuachana haumhusu yeye tu bali pia wewe. Ni juu yako uamue iwapo mtaendelea au la.

Miaka 22 na amezaa

Shangazi pokea salamu zangu. Nimekuwa na uhusiano na msichana fulani kwa miaka mitatu sasa. Tunapendana sana na ninaamini anaweza kuwa mwenzangu maishani. Lakini nimeshangaa kugundua kuwa ana mtoto. Singedhania hilo kwa sababu ana umri wa miaka 22 pekee wala hajaniambia. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kwa kuwa sasa umejua mpenzi wako ana mtoto, ni juu yako uamue iwapo unataka kuendelea na uhusiano huo ama utamuacha. Kama unampenda na unaamini anaweza kuwa mke mzuri kwako mkubali pamoja na mwanawe.

 

Mjeuri wa kuchukiza

Hujambo shangazi? Nina mwanamke mpenzi wangu ambaye nampenda na ninaamini yeye pia ananipenda kwa dhati. Lakini ana tabia ambayo inanichukiza. Mara nyingi amekuwa akinionyesha ujeuri na dharau na nahofia nikimuoa tutaishi kugombana. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Mtu anayekupenda hawezi kukuonyesha dharau. Tabia yake hiyo ni dalili kwamba hakupendi wala hakuheshimu. Nahisi kuwa unapoteza wakati wako na ningekuwa wewe ningejiondoa katika uhusiano huo.

 

Aligawa akaachwa

Kwako shangazi. Kuna msichana tuliyependana na tukaamua hatutaonja asali kabla ya ndoa. Hata hivyo, alisaliti penzi letu akazaa na mwanamume mwingine. Muda si mrefu alitemwa na sasa anataka turudiane. Nampenda lakini siwezi kusahau alivyonifanya. Nishauri.

Kupitia SMS

Utaonekana mjinga kumrudia mwanamke aliyekuacha na kushikana na mwanamume mwingine. Sasa ameona mteremko kwako! Ningekuwa wewe singepoteza wakati naye.

Bado nasaka mpenzi

Nimetuma ujumbe mara kadhaa katika ukumbi wako nikitafuta mchumba na bado sijafanikiwa.

Kupitia SMS

Kutafuta mchumba kunahitaji mtu awe na subira kwa hivyo endelea kutafuta wala usife moyo. Pili, usitegemee ukumbi huu pekee bali wewe mwenyewe pia jaribu kutafuta kwingine.