Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Rafiki yangu aliyeolewa wakaachana, ataka nimuoe

March 26th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Kuna msichana tuliyependana tukisoma shule ya upili lakini akakataa masomo akaolewa na rafiki yangu. Hata hivyo, waliachana punde tu baada ya kupata mtoto. Sasa msichana huyo amerudi kwangu akitaka nimuoe. Ninampenda lakini naogopa huenda mwanamume huyo akachukua mtoto wake. Je, nitakosea kumuoa?

Kupitia SMS

Kama umeamua kumuoa mwanamke huyo, suala la mtoto halifai kukutatiza kwa sababu si wako na baba yake ana haki ya kumchukua bora tu wakubaliane na mama yake. Hata hivyo, itakuwa muhimu kwanza uthibitishe kuwa wameachana kabisa wala sio kutengana tu ili usije ukalaumiwa kwa kuoa mke wa wenyewe.

 

Kipusa ninayemezea hunionyesha dharau

Shikamoo shangazi! Kuna msichana ninayempenda na nimekuwa nikimfuata kwa muda sasa nikimuomba tuwe na uhusiano. Lakini kila nikiongea naye hunionyesha maringo na dharau. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Maringo na dharau anayokuonyesha msichana huyo ni ishara kwamba hana mapenzi kwako na hakutaki. Kwa sababu hiyo haina maana kwako kuendelea kupoteza wakati wako ukimfuata. Wasichana ni wengi, tafuta mwingine.

 

Mwanamume ninayetaka anioe ni jirani yetu

Shangazi naomba ushauri wako. Nina mwanamume ambaye tunapendana na yuko tayari kunioa. Tatizo ni kuwa kwao ni karibu sana na kwetu.

Kupitia SMS

Hakuna shida yoyote kwa mtu kuolewa ama kuoa katika eneo anamoishi. Kama mnapendana na hamna uhusiano wowote wa damu, ujirani haufai kuwa kizuizi kwenu.

 

Nimesikia mtoto wa mwisho si wangu

Hujambo shangazi? Nimekuwa na mke kwa miaka sita sasa na tumejaliwa watoto sita. Hata hivyo, kumekuwa na uvumi kijijini kuwa mtoto wetu wa mwisho si wangu na jambo hilo linanitia tumbo joto kwa sababu kama ni kweli ina maana kuwa mke wangu alitembea nje. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ninaelewa kuwa jambo hilo linaweza kukuumiza sana moyoni iwapo ni la kweli. Hata hivyo, umesema kuwa umepata uvumi tu wala huna hakika. Kama unataka kujua iwapo mtoto huyo ni wako, tumia njia ya kitaalamu kupitia hospitalini.

 

Ameniomba ruhusa atafute wa kumpoza hadi nikamilishe elimu ya chuo

Shikamoo shangazi. Mimi ni msichana mwanafunzi wa chuo kikuu na nimekuwa na mpenzi kwa miaka mitatu. Mpenzi wangu anaishi mbali nami na analalamika kuwa anaumia sana kwa upweke. Sasa ananiomba nimruhusu atafute mwingine wa kumuondolea upweke hadi atakaporudi karibu nami. Nishauri.

Kupitia SMS

Mwanamume huyo anakuhadaa tu kuwa anakupenda lakini anajipenda zaidi tena ni mchoyo. Sababu ni kuwa anajali hali yake tu, hajali kwamba wewe pia unakumbwa na upweke. Mapenzi ya dhati ni wawili kuvumiliana katika kila hali, wawe karibu au mbali. Je, una hakika gani kwamba akitafuta mwingine aliko baadaye atamuacha akurudie? Kama hivyo ndivyo anavyotaka, mwambie pia wewe utatafuta wako uone kama atakuruhusu. Akikuruhusu, basi ujue hakupendi.

 

Wazazi wamekataa mume niliyechagua, hata nina mimba yake

Shikamoo shangazi. Niko katika uhusiano wa dhati na kijana tunayependana sana. Amejitolea kunioa lakini mama yangu na baba yangu mdogo wamemkataa kabisa. Kwa sasa nina mimba yake na nimemwambia mama yangu lakini haniamini. Sijui nitafanya nini kwa sababu siwezi kumuacha kijana huyo. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Ninaamini kuwa wewe ni mtu mzima aliyetimu umri wa kuolewa. Kama ndivyo, una haki ya kuchagua unayempenda na ambaye unataka kuishi naye kama mume wako. Kama wazazi wako hawana sababu nzuri ya kumkataa mpenzi wako, usikubali waingilie mipango yenu. Waambie wazi kuwa huyo ndiye chaguo la moyo wako na hutamuacha. Kama mama yako anashuku kuwa unamhadaa kuhusu mimba, bila shaka ataamini ikifikia kiwango cha kuonekana.